Daniel Samson
Dunia inashuhudia maendeleo makubwa ya teknolojia ambapo matumizi ya simu za mkononi yameongezeka. Kutokana na teknolojia kuwa njia rahisi ya kutoa huduma, taasisi za fedha kama benki zinatumia fursa hiyo kusogeza huduma karibu kwa wateja wao.
Watu hawalaziki tena kutembea au kutunza fedha nyumbani kwasababu dhamana hiyo iko mikononi mwa benki na kampuni za simu. Kwa kutumia simu ya mkononi mtu anaweza kufanya miamala ya fedha akiwa mahali popote.
Kulingana na ripoti ya shirika la GSMA State of Industry (2017) inaeleza kuwa mwaka 2016 pekee kulikuwa na watumiaji wa simu bilioni 4.8 na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hadi kufikia watumiaji bilioni 5.7 mwaka 2020. Huduma za kifedha kupitia simu kwa sasa zinapatikana katika nchi 92 duniani ikiwa na jumla ya huduma 277 kwa ujumla wake.
Licha ya teknolojia ya kutunza fedha kuwanufaisha watumiaji wa mtandao bado kuna watu wanaitumia fursa hiyo kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu. Katika maeneo mbalimbali nchini matukio ya wizi wa mtandaoni yamekuwa yakiripotiwa sana na vyombo vya habari.
Wizi wa mtandaoni kwa Tanzania umekuwa ukijitokeza zaidi kwenye uhamishaji wa fedha katika benki (Bank money transfer), mashine za kutolea fedha (ATM) na huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi.
Kulingana na ripoti ya Jeshi la Polisi (2017) ya matukio ya wizi mtandaoni kutoka mwezi oktoba 2016 hadi machi 2017 inaeleza kuwa kulikuwa na matukio 5,869 ambayo yalitokea katika mikoa 18 ya Tanzania Bara na mkoa 1 wa Zanzibar.
Wizi wa fedha kwa njia ya ATM ulikuwa na matukio 368, simu za mkononi 5,253 na uhamishaji wa fedha benki 248. Fedha zilizoibwa kwa kutumia njia hizo zilikuwa ni zaidi ya bilioni 4.523 na zilizookolewa ni milioni 131.7.
Kwa tafsiri nyepesi katika miezi sita ya matukio 5,869, kulikuwa na wastani wa matukio 84 kila mwezi na tukio 1 hadi 3 kwa siku. Kwa muktadha huo kila siku kulikuwa na watu wanaopanga na kutekeleza uharifu huo wa mtandaoni ili kujipatia fedha kwa udanganyifu.
Tofauti inayojitokeza katika mikoa yalikotokea matukio hayo ni kwamba mikoa mingine ilikuwa na matukio mengi zaidi kuliko mingine. Mathalani mikoa ya Mwanza, Dar es salaam, Mjini Magharibi (Zanzibar), Dodoma na Arusha inatajwa kuwa na matukio mengi zaidi ikilinganishwa na mikoa ya Tabora, Geita, Mtwara, Tanga, Iringa na Manyara ambayo ilikuwa na matukio machache.
Katika kundi la wizi wa fedha kupitia ATM mikoa ya Dar es salaam, Mwanza, Dodoma na Mjini Magharibi ilikuwa katika nafasi ya juu. Kundi la wizi wa uhamishaji wa fedha katika benki mikoa ya Dar es salaam, Mwanza, Mjini Magharibi, Katavi na Kigoma ilikuwa vinara.
Mikoa ya Dar es salaam, Mwanza, Mjini Magharibi, Dodoma na Arusha ilikuwa inaongoza kwa wizi wa fedha kwa njia ya simu za mkononi. Ipo mikoa ambayo iko nafasi za juu katika makundi yote na mingine inajitokeza katika kundi moja na makundi mengine iko katika nafasi za chini kabisa.
Dar es salaam, Mwanza na Mjini Magharibi iko katika nafasi za juu katika makundi yote matatu. Lakini Kigoma iko miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa wizi wa fedha za benki lakini katika makundi mengine iko katika nafasi ya chini.
Hali hii inaweza kuashiria tofauti iliyopo ya matumizi ya simu, ukuaji wa miji, upatikanaji wa huduma za benki na kiwango cha elimu miongoni mwa wananchi wa mikoa hiyo.
Kwa mfano Mwanza, Dodoma, Mjini Magharibi na Dar es salaam ni mikoa inayokuwa kwa kasi na watumiaji wa huduma za kifedha kwa njia ya benki na simu za mkononi ni wengi ikilinganishwa na Geita, Iringa na Mtwara.
Kutokana na matukio hayo Jeshi la Polisi liliwakamata watuhumiwa 1,276 na kesi 5,914 zilifunguliwa na kufikishwa mahakamani huku nyingine zikiwa chini ya upelelezi.
Wadau mbalimbali zikiwemo taasisi za fedha na kampuni za simu nchini wameendelea kukabiliana na matukio hayo ili kuhakikisha watumiaji wa mtandao wanakuwa salama wakati wote. Baadhi ya benki nchini zinachukua hatua kuwalinda wateja wao kwa kuwatumia ujumbe mfupi wa simu (simu banking) kila muamala unapofanyika na kumtaka mteja athibitishe kama anatambua muamala husika.
Pia matumizi ya teknolojia ya neno siri (one time password) kwa kila mteja kuwa na neno la siri ambalo analitumia afanyapo muamala. Lakini teknolojia hii inatajwa na wataalamu kuwa sio salama sana.
Kwa upande wake Mtaalamu wa Usalama Mtandaoni, Yusuph Kileo anasema wahalifu wa mtandao wanabuni mbinu mpya kila siku na hivyo kuzitaka taasisi za fedha kuhakiki taarifa za wateja wao na kutoa elimu itakayowasaidia watumiaji wa huduma za fedha kuwa salama.
“Hili linathibitishwa na wataalam wa mtandao kutokana na ongezeko kubwa la uhalifu ambapo mhalifu anakaa baina ya watu wawili wanaofanya mawasiliano hasa miamala ya kibiashara na kufanikiwa kusoma na kuchukua taarifa zinazosafirishwa na baadae kuzitumia taarifa hizo kuiba pesa kwenye mitandao”. Anasema Kileo.
Pia taasisi za fedha zimeshauriwa kutumia teknlojia mpya ikiwa ni pamoja na kuzifanyia marekebisho mashine za kutolea fedha mara kwa mara ili kupunguza wizi wa mtandaoni.
“Matumizi ya teknolojia mpya zinazoweza kusaidia kupunguza wizi huu ikiwa ni pamoja na kutotumika kwa program ya kompyuta ‘Windows XP’ katika mashine za kutolea fedha (ATM) kwani matukio kadhaa ya hivi karibuni yamebainika yamejiri kutokana na matumizi ya vifaa chakavu na vilivyopitwa na wakati vya ulinzi katika taasisi za kifedha pamoja na kuwa na umakini mdogo katika vifaa vinavyosaidia ulinzi ndani ya taasisi za kifedha”. Anashauri Kileo.
Kila mwaka dunia inapoteza zaidi ya bilioni 400 Dola za Kimarekani kutokana na wizi wa fedha mtandaoni.