Chaki ni bidhaa inayohitajika sana katika soko la Tanzania hasa kipindi hiki ambacho serikali imeweka mkazo kuinua ubora wa elimu kwa kuandikisha wanafunzi wengi.
Chaki hutengenezwa kwa kutumia madini aina ya Jisa. Jisa ni madini ambayo hutumiwa katika shughuli mbalimbali ikiwemo ujenzi na kutengeneza bidhaa kama chaki ambazo hutumiwa katika shule na vyuo.
Tanzania ni miongozi mwa nchi zenye kiwango kikubwa cha madini ya jisa (pypsum) ambayo yanaweza kutumiwa kwa miaka mingi ijayo lakini ubovu wa miundombinu ya barabara na reli ni kikwazo kwa wachimbaji wa madini hayo.
Kiwanda cha Dober Color kilichopo Singida ni miongoni mwa viwanda vya chaki nchini ambavyo vinazalisha chaki yenye ubora ambayo husafirishwa katika mikoa mbalimbali nchini. Kwa sasa inazalisha tani hamsini (50) kwa siku na soko likipanuka wataweza kuzalisha tani mia mbili kwa siku.
Shule za msingi na sekondari mkoani Singida zimeshauriwa kutumia chaki inayozalishwa na viwanda vya ndani ili kutekeleza sera ya viwanda ambayo inalenga kujenga uchumi wa kati na kuboresha maisha ya wananchi.
Sera ya viwanda ni kufufua viwanda vya ndani na kuviwezesha kuzalisha bidhaa zenye ubora zitakazotumiwa na wananchi wa ndani na kuuzwa katika soko la kimataifa.
Imebainika kuwa shule za mkoa wa Singida zinatumia chaki inayoagizwa kutoka jijini Dar es salaam na kusababisha viwanda vinavyozalisha chaki mkoani humo kukosa soko la uhakika.
Licha ya kuagiza chaki hiyo nje ya mkoa, shule hizo hulazimika kutumia muda mrefu na gharama kubwa za usafiri kabla chaki hizo hazijafika Singida na kusambazwa kwenye shule mbalimbali.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi ametoa maagizo hayo wakati akitembelea viwanda viwili vinavyozalisha chaki katika Halmashauri ya Itigi na kusema kuwa viwanda hivyo vinazalisha chaki yenye ubora na vinahitaji soko ili viweze kukua na kuajiri watu wengi zaidi.
“Hawa wenye viwanda wamejitahidi kuzalisha chaki bora haina vumbi na inauzwa kwa bei sahihi lakini shule zetu badala ya kuja kununua hapa ambapo ni karibu wanaagiza Dar es salaam na mikoa mingine”, amesema.
Ili kukuza soko la chaki, Mkuu huyo wa Mkoa amekubaliana na viongozi wa viwanda hivyo kutokuwatoza wateja walio nje ya mkoa huo gharama za usafiri ili kupanua wigo wa soko na kuongeza uzalishaji. Amezitaka shule zote mkoani humo kununua chaki katika viwanda hivyo ili kukuza uchumi wa mkoa huo na kuongeza pato la taifa.
“Yaani mnasubiri chaki hii iende Dar es salaam halafu mnainunulia kutoka huko, hii haikubaliki, kuanzia leo shule zote zinunue chaki hapa hapa ili tupunguze gharama pamoja na kuinua viwanda vyetu” amesema.
Licha ya viwanda hivyo vya chaki kukosa soko la uhakika, bado zinakabiliwa na changamoto ya usafiri hasa ubovu wa miundombinu ya barabara zinazoelekea katika machimbo ya jasi (gypsum) inayotumika kutengeneza chaki.
Kutokana na changamoto hizo Mkuu wa Mkoa huo, amezitaka halmashauri ambazo ziko karibu na eneo la machimbo hayo kuboresha miundombinu ili kuwawezesha wawekezaji wa ndani kufanya shughuli zao za kiuchumi.
Kwa upande wake, Meneja wa kiwanda cha chaki cha Doer Color kilichopo Itigi, Abdul Mahamoud amesema hatua hiyo ya serikali kupiga marufuku chaki kuagizwa kutoka nje ya mkoa huo itasaidia kiwanda chake kuongeza uzalishaji na kuajiri watu wengi zaidi.
“ Mkuu wa Mkoa tunashukuru kwa katazo hilo kwa kuwa litafanya viwanda vyetu vikue na kuongeza uzalishaji, ajira na kodi tunayolipa itaongezeka hivyo kukuza uchumi wa Singida” amesema Mahamoud.
Mkakati wa serikali kuinua viwanda
Serikali imesema inaangalia namna ya kudhibiti uingizwaji wa bidhaa aina ya Chaki ili kuongeza thamani ya viwanda vya ndani vinavyozalisha na pia iwapo itajiridhisha na uwezo wa kukidhi mahitaji ya soko la ndani kwa kuziuzia shule zote na vyuo vikuu itakuwa na uwezo wa kufanya maamuzi.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage akizungumza na vyombo vya habari mwezi Agosti mwaka jana alisema nia ya serikali ni kufufua viwanda vya ndani ili kutengeneza ajira nyingi, ambapo kwa sasa Tanzania ina viwanda zaidi ya 52,000 vinavyofanya kazi na 197 vimetelekezwa baada ya wenye viwanda kushindwa kuviendeleza.