ASILIMIA 15 ya Watanzania ndio wanaopata nishati ya umeme, kiwango ambacho hakitoshelezi na hakiendani na kasi ya maendeleo inayotarajiwa, FikraPevu imebaini.

Kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia za mwaka 2011, umeme kidogo unaopatikana hautoshelezi mahitaji ya taifa kwa ujumla.

Idadi hiyo ni ndogo ukilinganisha na nchi jirani za Kenya na Msumbiji ambapo kwa mwaka huo huo wa 2011, asilimia 19 ya Wakenya wote na asilimia 20 ya wananchi wa Msumbiji walikuwa wamefikiwa na nishati ya umeme.

Upatikanaji wa uhakika wa nishati ndio unaochangia kukua kwa uchumi mahali popote duniani, kwani nishati hiyo ndiyo inayotumika hata viwandani kwa ajili ya kuzalisha bidhaa mbalimbali.

Lakini kwa mataifa yanayoendelea ikiwemo Tanzania, suala la nishati ya uhakika limekuwa kitendawili huku ikikumbwa na kukatika kwa umeme mara kwa mara pamoja na mgawo ambao umeathiri maendeleo ya uchumi.

Kumbukumbu zilizopo, ambazo FikraPevu inazo, zinaeleza kwamba, hali hiyo inatokana na ukweli kwamba, asilimia kubwa ya nishati ya umeme nchini Tanzania inatokana na maji, hivyo ukame unapotokea ama shughuli za binadamu zikijitokeza katika maeneo mengine ikiwemo kilimo, huathiri uzalishaji wa umeme kwenye mabwabwa kadhaa yaliyopo.

Mwanzoni mwa mwaka 2014, Wakala wa Nishati Vijijini Tanzania (REA) ilisaini makubaliano ya kusambaza umeme kwenye mikoa 14 nchini ili kuhakikisha idadi kubwa ya wananchi inafikiwa na huduma hiyo muhimu.

Mikoa iliyoko kwenye mpango huo, kwa mujibu wa taarifa ambazo FikraPevu imezipata kutoka Wizara ya Nishati na Madini, ni Simiyu, Katavi, Shinyanga, Njombe, Tabora, Mwanza, Mtwara, Singida, Kilimanjaro, Iringa, Mara, Dodoma, Arusha and Ruvuma ambapo hadi kufikia mwaka 2017 Serikali itatumia kiasi cha Dola za Marekani milioni 300 kwa ajili ya usambazaji wa umeme vijijini.

Mipango hiyo inajumuisha kutengeneza mabwawa ya kuzalisha umeme kwenye maporomoko ya Darakuta Babati, Lingatunda Songea, Luswisi Ileje, Macheke Ludewa, Mwago Kasulu na Nole-Ihalula Njombe.

Katika kipindi cha miaka 10, matumizi ya nishati nchini Tanzania yameongezeka kwa asilimia 34 kutoka tani milioni 14.92 za mafuta mwaka 2002 mpaka tani milioni 22.16 za mafuta mwaka 2012. Takwimu za Wakala wa Kimataifa wa Nishati (IEA), zinaeleza kwamba matumizi ya nishati yameongezeka kutoka tani 0.42 mwaka 2002 mpaka tani 0.46 kwa mtu mwaka 2012. Hii ni pungufu ya kiwango cha nchi jirani ya Kenya ambacho ni tani 0.48 kwa mtu.

Wakati takwimu hizo zinatolewa, ilielezwa kwamba chanzo kikubwa cha matumizi ya nishati Tanzania kilikuwa ni mkaa na kuni, ambayo ni sawa na asilimia 85 ya nishati yote inayotumika nchini. Asilimia 14 inatokana na mafuta na gesi asilia wakati asilimia iliyobaki inazalishwa kwa nguvu za maji.

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka huo 2012, nusu ya umeme nchini ulizalishwa kwa kutumia gesi asilia, asilimia 29 ilitokana na uzalishaji unaotumia maji, na asilimia 20 ya umeme ulizalishwa kwa kutumia mafuta wakati ambapo asilimia iliyobaki ilizalishwa kwa kutumia malighafi za kibaolojia (miti na uchafu utokanao na wanyama) na nguvu ya jua. Lakini uzalishaji wa jumla wa nishati umeongezeka kwa zaidi ya asilimia 30 kutoka mwaka 2002 mpaka 2012.

Ingawa tafiti mbalimbali zinaendelea kufanyika, lakini Tanzania haizalishi mafuta na mpaka sasa hakuna mafuta yaliyogunduliwa nchini. FikraPevu inaamini uzalishaji wa gesi asilia unaendelea vizuri na unaleta matumaini.

Kwa mwaka 2012 pekee, Tanzania ilizalisha futi za ujazo bilioni 33 za gesi asilia, ambayo ilitumika kwa matumizi ya ndani ya nchi na uzalishaji huo unategemewa kuongezeka kutoka eneo la uzalishaji la Mnazi Bay linaloendeshwa na kampuni ya Maurel and Prom Tanzania, lililopo kusini mashariki mwa Tanzania kwenye Bonde la Ruvuma. Gesi hiyo ndiyo inayotegemewa kusafirishwa kupitia Bomba la Gesi kutoka Mnazi Bay kwenda Dar es Salaam ambako mbali ya kutumiwa kwa matumizi ya nyumbani na viwandani, pia kiasi kikubwa kitatumika kuzalisha umeme na kupunguza tatizo la mgawo.

Historia ya Utafiti wa Mafuta na Gesi

Wizara ya Nishati na Madini inaeleza kwamba, utafiti wa mafuta na gesi Tanzania ulikuwepo tangu mwaka 1952, na ugunduzi wa kwanza wa gesi asilia ulifanywa mwaka 1974 kule Songo Songo, wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi. Miaka nane baadaye (1982), ugunduzi wa pili ulifanyika mkoa wa Mtwara, unaopakana na Lindi, kwenye eneo la Mnazi Bay.

Kugunduliwa kwa wingi wa gesi katika maeneo haya kulichochea utafiti wa gesi eneo la ufukweni (onshore) na mbali ya ufukwe (offshore). Utafiti ulikuwa ukifanywa na kampuni za mafuta ghafi za kimataifa baada ya hapo kumekuwepo na ugunduzi mwingine mkubwa eneo la Mkuranga, Kiliwani Kaskazini na Ntorya.

Kwa mujibu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), historia ya mafuta na gesi nchini imegawanyika katika awamu tano ambazo zinafafanuliwa kama TPDC wenyewe walivyoieleza FikraPevu.

Awamu ya Kwanza: 1952-1964

Awamu hiyo ilihusisha kampuni za Shirika la Petroli la Uingereza (British Petroleum – BP) na Shell ya Uholanzi ambao walipewa sehemu ya kufanya tafiti na uchimbaji katika ukanda wa pwani. Hii ni pamoja na visiwa vya Mafia, Pemba na Zanzibar (Unguja). Kwa wakati huo, uchimbaji wa visima haukugundua haidrokaboni ya kutosha kwa ajili ya biashara.

Awamu ya Pili 1969-1979

Awamu hiyo ilikuwa na matukio muhimu mawili katika historia ya mafuta na gesi nchini Tanzania. Kwanza, ilikuwa ni kuanzishwa kwa kampuni inayomilikiwa na serikali, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) mwaka 1969, na pili, ugunduzi mkubwa wa gesi katika eneo la Songo Songo.

Baada ya kuanzishwa kwa TPDC, Mkataba wa kwanza wa Kuchangia Uzalishaji (Production Sharing Agreement – PSA) ulisainiwa kati ya TPDC na AGIP (Aziende Generale Italian Petroli – kampuni ya mafuta ya Italia) kwenye eneo ambalo lilikuwa chini ya usimamizi wa kampuni za BP na Shell wakati wa Awamu ya Kwanza. Mwaka 1973, AGIP waliingia ubia na kampuni ya AMOCO na kuchimba visima vitano, vitatu ufukweni na viwili mbali na ufukwe. Maandiko mengine yanaonyesha kwamba jumla ya visiwa sita vilichimbwa na AGIP na AMOCO huku vitatu vikiwa ufukweni na vitatu mbali na ufukwe.

Uchimbaji huu ulisababisha ugunduzi mkubwa kule Songo Songo mwaka 1974, ugunduzi ambao ulithibitishwa na TPDC katika programu yake ya visima vitatu iliyotekelezwa kuanzia mwaka 1975 hadi 1979.

Kuanzia mwaka 1978, TPDC iliingia moja kwa moja katika utafiti kwenye maeneo ya ufukweni na mbali na ufukwe. Utafiti wa ufukweni ulijumuisha maeneo ya Ruvu, Kimbiji/Bigwa, Pemba, Mafia na Ruvuma, wakati ule wa mbali na ufukwe ulijumuisha Songo Songo, Pemba na Zanzibar.

Awamu ya Tatu: 1980-1991

Ni katika kipindi hiki ambapo Serikali ilitunga Sheria ya Petroli (inayohusu Utafiti na Uzalishaji) Tanzania mwaka 1980, na kugundulika kwa gesi katika eneo la Mnazi Bay. Kati ya awamu hizo tano, uchimbaji mwingi ulitokea katika awamu hiyo ya tatu na hii ilisababishwa na kutungwa kwa Sheria ya Petroli na kupanda kwa bei ya petroli mwanzoni mwa miaka ya 1980.

Kwa hiyo TPDC, kampuni ya serikali, ikaingia katika uendelezaji wa Songo Songo kwa kuchimba visima viwili vya Kimbiji Mashariki-1 na Kimbiji Kuu-1. Kampuni za Shell, IEDC (Shirika la Kimatatifa la Maendeleo ya Uchumi), na Camarco Group, ELF, na AMOCO walipewa leseni za utafiti wa mafuta na gesi. Kampuni ya Shell na baadaye Esso walipewa leseni tano zinazochukua maeneo ya Ruvu na Bonde la Selous mwaka 1981.

Awamu ya Nne: 1992-1999

Awamu hiyo ilikuwa na shughuli chache za utafiti katika miaka yake ya mwanzo baada ya kukosekana waombaji wapya wa kufanya tafiti, na maamuzi ya serikali kuendeleza zaidi maeneno ya uchimbaji eneo la Songo Songo ambayo yaligubika shughuli nyingine.

TPDC na Shirila la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO), wakishirikiana na kampuni za Canada, Ocelot na Trans-Canada Pipelines, walijishughulisha sana na uendelezaji, usambazaji na utumiaji wa nishati katika eneo la Songo Songo.

Kutolewa kwa leseni za utafiti mwaka 1995 katika mabonde ya pwani kwa kampuni za kimataifa, ikiwa ni pamoja na Tanganyika Oil Company, Exxon Mobil, Shell, KUFPEK (Kampuni ya Kigeni ya Utafiti wa Petroli ya Kuwait) na AMOCO kuliongeza kasi ya shughuli za utafiti.

Tanganyika Oil Company ilichimba visima viwili katika Bonde la Mandawa mwaka 1996/97. Pia, makubaliano ya utafiti yalitiwa saini kati ya TPDC na kampuni ya Canada ya Antrim Resources (sasa hivi inaitwa Atrim Energy Limited) na Canop World-Wide na Ndovu Resources ya Australia.

Awamu ya Tano: 2000-hadi Sasa

Kampuni tano zilipewa leseni kufanya kazi katika kipindi hiki. Kampuni hizo ni pamoja na Petrobras ya Brazil (Kitalu namba 5, mwaka 2004), Ophir Energy (Kitalu – 1, mwaka 2005), Ophir Energy (Kitalu –3, na 4, mwaka 2006), na Statoil (Kitalu – 8, mwaka 2012).

Ikumbukwe kwamba, Songo Songo na Mnazi Bay ziliingia katika shughuli timilifu ya kibiashara mwaka 2004 na 2006 mutawalia.

Kutolewa kwa leseni hizo kulifuatiwa na utafiti na uchimbaji wa visima na kampuni ya BG Group (Kitalu – 1,2,3), Statoil (Kitalu – 2) na Petrobras (Kitalu – 5), ambao ulipelekea kwenye ugunduzi mkubwa wa gesi katika kitalu namba 1,2,3 na 4.

Mnamo mwezi Machi 2012, kampuni ya Statoil na ExxonMobil walifanya ugunduzi mkubwa kuliko yote wa akiba ya gesi mbali na ufukweni katika eneo la Zafarani. Hadi Juni 2012, kulikuwa na mikataba 26 ya Makubaliano ya Kuchangia Uzalishaji (PSA) iliyosainiwa na kampuni 18 za utafiti wa mafuta.

Katika juhudi za kusimamia sekta ya gesi, Serikali imepitisha Sera ya Gesi Asilia Tanzania, ambayo inagusa changamoto zinazohusishwa na usimamizi wa gesi asilia na jinsi ya kuendesha usimamizi mzuri wa sekta hii.