Vuguvugu la kufufua mchakato wa Katiba Mpya limeendelea kujitokeza kwa sura mpya ambapo uchunguzi uliofanywa na Shirika la Twaweza unaoonyesha kuwa wananchi wengi wanataka katiba mpya inayoakisi matakwa yao.
Akiwasilisha matokeo hayo ya uchunguzi wa Sauti za Wananchi kuhusu Kukwama kwa Mchakato wa Marekebisho ya katiba leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Twaweza, Aidan Eyakuze amesema wananchi wengi wanataka mchakato wa Katiba Mpya ufufuliwe lakini wanatofautiana katika njia za kuuendea mchakato wa kupatikana kwa katiba.
“Matokeo haya yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,745 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara mwezi Juni hadi Julai 2017. Asilimia 67 ya watanzania wanasema ni muhimu kwa Tanzania kupata katiba mpya” amesema Eyakuze.
Wananchi 2 kati ya 3 waliowahoji katika uchunguzi huo wamesema njia nzuri ya kufufua mchakato wa katiba ni kuanza upya na tume mpya. Hili kundi ni kubwa na linashauri mchakato wote wa awali uwekwe pembeni na Tume mpya ya kukusanya maoni iundwe na wananchi watoe maoni yao.
“Karibu nusu ya wananchi (48%) wanasema kuwa njia nzuri ya kufufua mchakato wa mabadiliko ya katiba ni kuanza mchakato huo mpya” amesema Eyakuze.
Wananchi wengine wamependekeza kuwa Rasimu ya Warioba (New Constitution) ambayo iliwasilishwa katika bunge la Katiba ndio ipigiwe kura na wananchi kwasababu wakati wa kukusanya maoni ilizingatia maoni mengi ya wananchi. Pia wameikataa Katiba ya Chenge iliyopendekezwa na wabunge wa Bunge la Katiba ambayo ilibeba maslahi mengi ya wanasiasa kuliko wananchi.
Aidan Eyakuze anaeleza kuwa “ Wananchi wawili kati ya kumi (18%) wanasema njia nzuri ni kwenda moja kwa moja na kuipigia kura rasimu ya Warioba. Wananchi waliokuwa na uelewa wa maana ya katiba walionesha kupendelea zaidi kufufua mchakato wa mabadiliko ya katiba kwa kupigia kura rasimu ya katiba ya Warioba; asilimia 25 ikilinganishwa na asilimia 18”
Lakini idadi ya wananchi wanaopendekeza rasimu ya Warioba ni ndogo ikilinganishwa na wale wanaosema mchakato uanze upya kwasababu uligubikwa na tofauti kubwa za kisiasa na hata kuharibu kazi yote aliyoanzisha Rais mstaafu Jakaya Kikwete. Hii inaweza kutafsiriwa kama kiu waliyonayo wananchi kuipata katiba mpya ambayo kwa sehemu inakwamishwa na wanasiasa ambao wanatetea maslahi yao ya kuendelea kushika dola.
Hisia hizo za wananchi zimeendelea kujitokeza katika uchunguzi huo ambapo mwananchi 1 kati ya 10 anasema ili tupate katiba mpya tumalizie mchakato wa kuipigia kura rasimu ya Chenge/ Katiba Pendekezwa. Katiba hiyo ilikataliwa na baadhi ya wabunge wa Bunge la Katiba ambapo walisusia mchakato huo baada ya maoni yao kukataliwa.
“Idadi ndogo ya asilimia 13 ya wananchi wanasema njia sahihi ni kuipigia kura rasimu ya Chenge/Katiba inayopendekezwa, wakati wananchi wachache sana (6%) wanasema mchakato uanze upya na Bunge jipya au rasimu ipelekwe bungeni ili wabunge wafanyie kazi toleo jipya”.
Hata hivyo, uchunguzi huo wa sauti za wananchi uliwauliza ni toleo gani litumike kama sehemu ya kuanzia majadiliano iwapo mchakato wa katiba utaanzishwa tena?
Ambapo Wananchi wanne kati ya kumi (38%) wanasema tuanze “ukurasa mpya” na wananchi watatu katika ya kumi (31%) wanasema rasimu ya Tume ya mabadiliko ya Katiba (rasimu ya Warioba) itumike.
Ili kukwepa gharama za kifedha na kupoteza muda kuanza mchakato wa kuunda tume mpya na kukusanya maoni, baadhi ya wananchi (43%)walionesha kupendelea zaidi kufufua mchakato wa mabadiliko kwa kurejea kwenye rasimu ya katiba ya Warioba na kuanza hapo.
Maoni ya Wadau kuhusu uchunguzi
Msemaji wa Chama Cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu amesema matokeo ya uchunguzi wa Twaweza ni muendelezo wa utamaduni wa kufanya tafiti za kisayansi ambazo zinaakisi hali halisi ya jamii yetu. Amesema kuwa kusitishwa kwa mchakato wa katiba mpya baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2015 kulizima sauti za wananchi ambao walitaka kusikika kwenye katiba.
“Katiba ni jambo la kimuafaka hata kama hatulipendi, msingi wa mambo yote katika nchi ni katiba. Utafiti huu umeonyesha wananchi wengi wanahitaji katiba mpya lakini mchakato mzima wa katiba mpya umezima sauti za wananchi”.
Ameongeza na kusema kuwa mchakato wa katiba ulikwama kwasababu ya kuibuka vikundi vyenye maslahi kutoka katika vyama vya siasa ambavyo vilikuwa vinapigania kushika madaraka.
Naye Katibu wa Itikadi, Siasa na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema uchunguzi huo wa Twaweza amegundua kuwa watanzania wengi wanataka ukatiba na sio katiba iliyoandikwa. Amesema mahitaji makubwa ya wananchi ni viongozi waadilifu wenye uwezo wa kusimamia rasilimali za nchi.
“Watanzania kwa takwimu hizi za Twaweza wanataka kuona Ukatiba (Constituonalism) kuliko katiba (Constitution) nchini. Watu wa kawaida wanataka viongozi waadilifu, wasiokula rushwa, wanaojua cheo ni dhamana huo ndio ukatiba” amesema Polepole,
“Ukatiba ni kuwekeana mifumo hata kama haikuandikwa mahali, kila mtu akielewa hii mifumo hakutakuwa na tatizo. Tunaweza kuaandaa katiba na kuiweka kwenye kitabu lakini bila Ukatiba hakuna atakayeifuata”.
Wakati huo huo amesema katiba ni muhimu kwa taifa lakini wao kama Chama Cha Mapinduzi wanaona sio wakati mwafaka wa kufufua mchakato wa katiba mpya na wataruhusu jambo hilo hapo baadaye.
Kwa upande wake Mjumbe wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Deogratius Bwire amesema suala katiba lisichukuliwe kisiasa kwasababu wananchi wanyonge wanahitaji katiba bora itakayowahakikishia upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii ikiwemo maji, elimu, huduma za afya na nishati.
“Wananchi wanaahidiwa vitu lakini hakuna sehemu inayompa nguvu ya kudai vitu vile wakinyimwa. Tunaposema tuwe na ukatiba wa kukubaliana bila maandishi, nini kitatokea pale makubaliano haya yatakaposahaulika?”
Kukwama kwa Mchakato Wa Katiba Mpya
Ikumbukwe kuwa mchakato wa kuipata katiba mpya ulianza miaka mingi iliyopita lakini ulipata nguvu mwaka 2011 baada ya wadau na wananchi kuishinikiza serikali kuanza mchakato huo.
Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete alikubali na kuteua Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilikusanya maoni kutoka kwa wananchi.
Katiba hiyo ilipitia michakato mbalimbali na ilipofika katika Bunge la Katiba ulikwama kutokana na wabunge wa bunge hilo kushindwa kufikia muafaka na kuipitisha Katiba ya Warioba. Mabadiliko kadhaa yalifanyika katika Katiba ya Warioba na baadaye ikaitwa Katiba Pendekezwa ambayo inatajwa kuacha maoni mengi ya wananchi.
Hata alipoingia madarakani Rais John Magufuli hakuonyesha nia ya kuendeleza mchakato huo wa kuwapatia wananchi katiba mpya kwa madai kuwa katiba siyo kipaumbele chake.
Hata hivyo makundi mbalimbali zikiwemo Asasi za Kiraia na wanaharakati wameendelea kupaza sauti kuishinikiza serikali kukamilisha mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya.
Katika kuendeleza majadiliano ya katiba, Shirika la Twaweza limekuja na matokeo ya uchunguzi ambao ulihusisha sauti za wananchi ambao wamesema wananchi wengi wanapenda kuona mchakato wa katiba mpya ukifufuliwa na kukamilishwa kwa wakati.
Inaeelezwa kuwa Afrika Kusini na Kenya ndio nchi pekee ambazo zina katiba bora miongoni mwa ncho zote barani Afrika ambapo zimezingatia zaidi uhuru wa wananchi katika kujieleza, kupata taarifa na kujenga mifumo imara ya kitaasisi ambayo inaendeshwa kwa uwazi na ukweli.