Je, kuwatoa watoto wa kike vijijini kwenda mjini kufanya kazi, kunachangia kuwepo usafirishaji haramu wa binadamu nchini? Watoto wangapi Tanzania ni wahanga wa usafirishaji haramu wa binadamu?
Mwandishi Rebecca Grant anasema kwenye taarifa iliyochapishwa na gazeti la The Guardian la Uingereza kuwa usafirishaji haramu wa binadamu umeshamiri nchini Tanzania, huku watoto wengi wakijikuta kwenye mazingira ya utumwa baada ya kurubuniwa na madalali wanaofanya biashara hiyo kwa ahadi kuwa wao na familia zao watapata maisha bora.
Grant anaeleza kuwa utekwaji wa namna hii unaofanywa ili kuwatumikisha wasichana ni tatizo kubwa nchini Tanzania linalohusiana na usafirishaji wa binadamu kama inavyoelezwa kwenye Ripoti iliyotolewa na serikali ya Marekani kuhusu biashara ya usafirishaji haramu wa binadamu.
Mara nyingi, familia za hao watoto huhusika katika kuwezesha aina hii ya usafirishaji haramu wa binadamu ndani ya mipaka ya nchi kwa kushirikiana na madalali wanaotoa ahadi kuwa watoto wao watapata kazi nzuri kirahisi, pesa nyingi na elimu.
Inasemekana wapo baadhi ya madalali wanaowafuata wazazi na kuwapa fedha taslimu mkononi, kuanzia kiasi cha shilingi 10,000 mpaka 30,000 (tarkriban US$4.50–13.30) ili wawaruhusu watoto wao waende nao, kwa ahadi ya kuwapatia ajira na kipato kizuri ambacho kinahitajika katika mazingira wanayoishi, pamoja na kuwapatia elimu wakiwa mjini. Mara nyingi ahadi hizo hazitimii na badala yake watoto wanaishia kuingizwa katika utumwa mamboleo.
Je, tatizo hili la kuwasafirisha wasichana kutoka vijijini kwenda mijini kutafuta kazi ni kubwa kiasi gani?
PesaCheck imefanya uchunguzi kuona kama kuwatoa watoto wa kike vijijini na kuwaleta mjini kwaajili za kutafuta kazi kunachangia usafirishaji haramu wa binadamu na tumeona kwamba madai haya ni ya KWELI kwasababu zifuatazo:
Kwa mujibu wa Utafiti wa Utumikishwaji wa Watoto Tanzania (2014), watoto 131,741 wameajiriwa kama wafanyakazi wa ndani huku watoto 110,911 kati yao wakiwa ni wasichana.
Hata hivyo, ni vigumu kujua idadi kamili ya watoto wanaosafirishwa kwenda mjini kwaajili ya kutafuta kazi kwasababu hufanywa kwa siri na wahanga huogopa kujitokeza na kusema lolote juu ya hili.
Tafiti zinaonyesha kuwa asilimia 97 ya usafirishaji haramu wa binadamu hufanyika ndani ya mipaka ya nchi, ikihusisha vijana wenye umri wa miaka 12 hadi 17, ambao asilimia 74 kati yao ni wasichana.
Hawa wasichana wanatoka mikoa ya Iringa, Morogoro, Singida, Dodoma na Kilimanjaro kwenda jijini Dar es Salaam na visiwani Zanzibar kufanya kazi za ndani na wakichangia ukuaji wa biashara hii haramu.
Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2017 iliyotolewa na serikali ya Marekani kuhusu biashara ya usafirishaji haramu wa binadamu, viko viashiria vinavyoonyesha kwamba Tanzania “inatoa, inapitisha na ni sehemu wanayofikia” watu wazima pamoja na watoto wanaotumikishwa pamoja na kuhusishwa na biashara ya ngono.
Serikali ya Tanzania imechukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na tatizo hili. Angalau wahanga 100 wamepewa msaada kwa kuwekwa kwenye vituo maalumu na kupewa makazi, kujiunga na shule za serikali na wengine kupewa elimu ya ufundi.
Serikali pia imeonyesha jitihada zake katika kudhibiti biashara hii kwa kuweka Sheria ya Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu (2008). Mwaka 2015, serikali ilitenga kiasi cha Sh. Milioni 80 kwaajili ya kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu na kuwezesha sheria ya mwaka 2008 kuanza kutumika.
Hata hivyo, sheria iliyopo haijaanza kutumika na huduma za ulinzi kwa wahanga wa biashara hii haziridhishi. Japokuwa kwa wastani, kulikuwa na majalada 100 ya kuchunguza tuhuma za usafirishaji haramu wa binadamu mwaka 2016, idadi ya wasafirishaji wanaoshtakiwa ni ndogo. Watuhumiwa wa makosa ya usafirishaji wa binadamu hulipa faini tu badala ya kutumikia kifungo kwa makosa waliyofanya. Kulingana na takwimu zilizopo kulikuwa na kesi 12 za usafirishaji binadamu kwa mwaka 2015 pekee.
Ripoti iliyotolewa na serikali ya Marekani inaonyesha kuwa serikali ya Tanzania imefanya kampeni mashuleni ya kuelimisha juu ya usafirishaji haramu wa binadamu. Pia, idadi ya kesi ambazo ziko kwenye uchunguzi, zinazotolewa hukumu na kukamatwa kwa watuhumiwa wa biashara ya usafirishaji haramu wa binadamu zimeongezeka.
Hivyo, tunaweza kuhitimisha kwa kusema kwamba usafirishaji haramu wa binadamu ndani ya nchi unachangiwa kwa kiwango kikubwa na kuwasafirisha watoto wa kike kutoka vijijini kwenda mijini kwaajili ya kufanya kazi za ndani.
Hii ina maana kwamba madai ya ripoti iliyoandaliwa na serikali ya Marekani kuwa utekwaji wa namna hii unaofanywa ili kuwatumikisha wasichana ni tatizo kubwa nchini Tanzania linalohusiana na usafirishaji haramu wa binadamu ni KWELI.
Makala hii imeandikwa na PesaCheck Fellow Belinda Japhet, Mwandishi na Mshauri Mtaalamu wa maswala ya mawasiliano.