Baada ya ukarabati, Uwanja wa Ndege Tabora kujiendesha kiuchumi

Jamii Africa

WAKATI Rais Dkt. John Magufuli anatarajiwa kuuzindua Jumatatu, Julai 24, 2017, Uwanja wa Ndege Tabora sasa unatakiwa kujiendesha wenyewe baada ya ukarabati mkubwa uliogharimu Shs. 27 bilioni.

FikraPevu inafahamu kwamba, miongoni mwa maeneo yaliyokarabatiwa ni pamoja na kuboresha njia ya kurukia, eneo la abiria na masuala mengine ya mawasiliano uwanjani hapo.

Meneja wa Mradi wa ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Tabora Eng. Neema Joseph, akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, kuhusu maendeleo ya ujenzi yaliyofikiwa kiwanjani hapo, wakati akikagua ujenzi wake.

Ukarabati huo unawezesha ndege kubwa kutua uwanjani hapo na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika ukanda wa magharibi.

Tayari Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amekweisha uagiza uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kuweka mikakati endelevu ili kuwezesha uwanja huo kujisimamia na kujiendesha kutokana na miundombinu bora na ya kisasa ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 96.

"Hivi sasa huduma ya usafiri wa ndege katika uwanja huu inaridhisha, hivyo ongezeni ubunifu ili kuvutia abiria wengi na kuwezesha uwanja kujiendesha," alisema Prof. Mbarawa wakati alipofanya ziara ya ukaguzi hivi karibuni.

Alisisitiza kuwa gharama za usafiri wa anga zitaendelea kupungua kadiri huduma na ubora zitavyokuwa zinaendelea kuongezeka ili kuwezesha abiria wengi zaidi kutumia usafiri huo na hivyo kuwezesha pato la Taifa kuongezeka.

Rais Magufuli anatarajiwa kufungua Uwanja wa Ndege wa Tabora baada ya kufungua barabara ya Tabora – Puge – Nzega na barabara ya Tabora – Nyahua.

Barabara ya Tabora – Nyahua yenye urefu wa kilometa 85 imejengwa na kampuni ya China Chongqing International Construction Corporation (CICO) kwa gharama ya Shs. 93.402 bilioni.

Aidha, barabara ya Tabora – Puge – Nzega yenye urefu wa kilometa 114.9 imejengwa kwa awamu ambapo awamu ya kwanza ni kutoka Nzega-Puge (58.8km) ambayo ilijengwa na kampuni ya China Communications Construction Company (CCCC) kwa gharama ya Shs. 66.358 bilioni, wakati awamu ya pili (56.1km) kutoka Puge hadi Tabora ilijengwa na kampuni ya umma ya China, Sinohydro, kwa gharama ya Shs. 62.737 bilioni.

FikraPevu inafahamu kwamba, Sinohydro ndiyo “sura ya upanuzi wa China ulimwenguni” kwani ina mikataba katika nchi 55 duniani kuanzia Bara Asia, Afrika, Ulaya (kutoka makao makuu ya Umoja wa Ulaya huko Belgrade, Serbia), Amerika Kaskazini na Amerika Kusini, ambapo nchini Tanzania ilishinda mikataba 12 ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa 779.95km.

Kampuni hiyo pia ndiyo iliyojenga barabara ya Manyoni – Itigi – Chaya yenye urefu wa kilometa 89.3 kwa gharama ya Shs. 109.643 bilioni , na uzinduzi wa barabara hiyo utafanywa na Rais Magufuli Julai 25, 2017 huko Itigi.

Kwa upande wake, Meneja wa TAA Mkoa wa Tabora, Eng. Danstan Komba, alisema kuwa idadi ya abiria wanaotumia uwanja huo imeongezeka kutoka asilimia 10 kwa mwaka 2011 hadi kufikia asilimia 62.3 mwaka 2016 kutokana na ndege mpya za ATCL za Bombardier Dash-8 kuanza safari zake mkoani humo.

“Baada ya mradi wa ujenzi wa uwanja huu kukamilika, mashirika ya ndege yataongeza safari zake mkoani hapa kwa kuzingatia uwepo wa miundombinu bora yenye kukidhi mahitaji na hivyo itatoa chachu ya maendeleo kwa wakazi wake na kuboresha shughuli za kiuchumi na kijamii,” alisema Komba.

Katika hatua nyingine, Prof. Mbarawa alitoa wito kwa uongozi wa Chuo cha Reli cha Tabora kuwajengea uwezo wanachuo ili kupata wataalam wenye ujuzi, weledi, maarifa na uadilifu katika kusimamia mradi mkubwa wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge).

Prof. Mbarawa alitoa wito huo alipotembelea chuo hicho ambacho kinatoa mafunzo mbalimbali yahusuyo reli.

“Serikali inawategemea ninyi kuendesha Reli ya Kisasa kwa kuwa ujenzi wa reli ni kitu kimoja na usimamizi na uendeshaji ni kitu kingine," alisema. 

Aidha, alisema Mkoa wa Tabora utakuwa kiungo muhimu cha Reli ya Kisasa kwani utaunganisha Mikoa ya Shinyanga, Kigoma, Mwanza na nchi za jirani. 

Ujenzi wa reli hiyo utagharimu takriban Shs. 16 trilioni, hivyo Waziri Mbarawa aliwataka Watanzania kutumia fursa hiyo kujipatia ajira na kufanya kazi kwa uzalendo.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *