ZAIDI ya watu 30 wamenusurika kufa kwa kuzama majini, baada ya boti walizokuwa wakisafiria kugongana katika Ziwa Victoria, Wilaya ya Musoma Vijijini Mkoani Mara; imethibitishiwa.
Imeelezwa kwamba ajali hiyo imetokea hii leo majira ya saa 3:15 asubuhi katika eneo Rethi, ambapo boti moja iliyokuwa ikisafirisha abiria kutoka Mwigobero mjini Musoma kwenda Kisiwa cha Rukuba kugongana uso kwa uso na boti nyingine ya wavuvi, jambo lililosababisha taharuki kubwa.Taarifa kutoka mjini Musoma zinaeleza kwamba, boti ya abiria ilikuwa na watu 28 na mizigo nyingi, huku boti ya wavuvi ikiwa imebeba wavuvi wawili, na kwamba watu wote waliokolewa.
Kwa mujibu wa taarifa hizo zilizothibitishwa pia na Kamanda wa Polisi Mkoani Mara, Robert Boaz (RPC), zinasema kwamba, baada ya boti hizo kugongana iliharibika na kusababisha maji mengi kuanza kujaa ndani, ambapo abiria wote walipatwa na hofu kubwa.
“Ni kweli ajali ipo na watu kama 30 hivi nusura wafe kwa kuzama majini. Watu hawa walikuwa kwenye boti ndani ya Ziwa Victoria, lakini boti hizo hazikuwa na vifaa vya kujiokolea.
“Hii ajali imetokea asubuhi leo, na abiri walikanyagana baada ya ajali kutokea. Kila mmoja alitaka ajiokoe mwenyewe kabla ya kuokolewa”, alisema mashuhuda mmoja wa ajali hiyo, Fikiri Aloyce Malenge.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoani Mara, Robert Boaz alisema: “Kweli hii ajali imetokea leo, majira ya saa 3 hivi asubuhi. Na katika ajali hii boti moja ilikuwa na abiria 28, lakini ile ya wavuvi ilikuwa na watu wawili?
“Hizi boti ya wavuvi na ile ya abiria zimegongana uso kwa uso. Lakini watu wote walifanikiwa kuhamia kwenye boti ya wavuvi na hakuna aliyefariki dunia hata mmoja”, alisema Kamanda wa Polisi Mkoa huo wa Mara, Boaz.
Alisema, chanzo cha ajali bado hakijajulikana na kwamba jeshi lake linaendelea na uchunguzi kuhusiana na ajali hiyo mbaya, na kwamba hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo?
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Boaz, abiria wote walipatiwa huduma ya kwanza papo hapo na kuruhusiwa kuendelea na majukumu yao ya kawaida.
Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza