Butiama: Majengo mabovu ya Zahanati ni hatari katika nyakati za mvua

Mariam Mkumbaru

"Nina miaka 20 sasa nafanyakazi katika mazingira haya, ni magumu sana lakini kwa sababu natoa huduma kwa watanzania wenzangu inabidi niwe mvumilivu,"alisema Veridiana Majura(49)  ni muuguzi katika zahanati ya Rwamkoma wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara.

Veridiana ni mzaliwa wa kijiji cha Majita wilaya ya Musoma Vijijini, alimaliza shule darasa la saba na kujunga katika  chuo cha mafunzo ya uuguzi kilichopo Shirati katika wilaya ya Rolia mkoa wa Mara kwa mwaka mmoja, mwaka 1993 alianza kutoa huduma katika zahanati hiyo.

Veridiana alisema kuwa zahanati ya Rwamkoma ndio kituo cha kwanza kuaza kazi, hakutegemea  kama angepangwa katika kijiji hicho maana ni mbali kutoka kijijini kwao Majita.

Veridiana-akiwa-zahanati

Veridiana akiwa nje ya jengo la zahanati (dirisha linaloonekana ndicho chumba cha wajawazito, maarufu kama 'leba')

Alipofika katika zahanati hiyo alimkuta muuguzi mmoja na mganga mmoja, walimpokea na kumuonesha ukubwa wa zanati hiyo na jinsi ya kutoa huduma kwa wakazi wa kijiji hicho.

"Nilikuwa sina furaha kwa kuona mazingira ya zahanati yalivyo lakini furahi ilikwisha kabisa baada muuguzi mwenzangu kuhamishiwa katika hopsitali ya wilaya ya Butiama,  huku akiwa ameniacha na mganga mpaka sasa tupo wawili bado hatujapata mtu mwengine wa kutusaidia toka mwaka 1995,"alisema Veridiana.

Aidha Veridiana alisema kuwa  zahanati hiyo imeanza kutoa huduma mwaka 1964, ikiwa na vyumba vitatu tu vya kutolea huduma, chumba cha kwanza cha kumuona mgonjwa na kumpima, chumba cha pili ni leba na chumba cha tatu kwa ajili ya kupima watoto na wajawazito.

"Vyumba vilivyokuwepo havitoshi kulingana mahitaji ya wagonjwa wanaofika kwa siku katika zahanati hii kuanzia wagonjwa 15 hadi 20 wote wanataka huduma na chumba cha kutolea huduma ndio hiki unachokiona hapa,"alisema Veridiana.

Kwa upande wa Chumba cha kujifungulia hakina usiri wowote, mjamzito anapojifungua kama kuna mtu nje anamuona kutokana na dirisha lake kuwekewa mabati tuu, wakati chumba kama hiki kinatakiwa kiwe cha usiri wa hali ya juu, pia hakuna chumba maalumu cha kupumzikia wagonjwa anapofika hapa hali ikiwa mbaya.

Kwa uhalisia jengo la zahanati linatakiwa kuwa na vyumba visivyopungua sita, chumba cha maabara, chumba cha mganga, chumba sindano, chumba cha kutoa dawa, chumba cha kupumzika wagonjwa na  chumba cha leba.

Changamoto nyingine ni uchakavu wa jengo lenye la zahanati ya Rwamkoma lina ufa mkubwa sana ukutani, hii ni hatari kwa wahudumu wanaoishi katika jengo hilo pamoja na wagonjwa wanaopatiwa huduma katika zahanati hiyo. Kuna uwezekano mkubwa wa kuanguka na kusababisha madhara makubwa hasa kipindi hiki cha mvua.

Ukuta-zahanati-Rwamkoma-Butiama

Aidha zahanati hiyo pia inakabiliwa na ukosefu wa vifaa tiba na dawa za kutibu magonjwa mbalimbali ikiwemo dawa ya malaria haipo katika  katika zahanati hiyo kwa muda wa miezi sita sasa.

Pia hakuna dawa za kumchoma mjazito baada ya kujifungua ili mfuko wa uzazi usinye na asiweze kupoteza damu nyingi, dawa za kifua, kuharisha, vipimo vya VVU kwa wajawazito hakuna, kipo cha kujua wingi wa damu kwa mjamzito hakuna, hakuna mzani wa kumpimia mtoto wa kuanzia miezi mitatu.

Vilevile hakuna mashine ya kumtoa uchafu mtoto mdomoni anapozaliwa, Quinine hakuna pamoja na madawa ya kutuliza maumivu pia hakuna, kwa sasa mgonjwa anapokuja anapimwa malaria na kuambiwa aende kununua dawa kwenye maduka ya madawa.

"Mgonjwa anapofika kama anaumwa malaria na anapimwa akigundulika anayo anaambiwa akanunue dawa za malaria na bomba la sindano katika maduka ya madawa yaliyopo karibu na zahanati kisha anarudi kuja kuchomwa kama ameandikiwa sindano,"alisema Veridiana.

Tatizo la ubovu wa majengo ya zahanati na uosefu wa madawa sio tu katika zahanti ya Rwamkoma bali lipo katika zahanati nyingi ambazo nimezitembelea na kuona uhalisia wa tatizo hili.

Sanduku-dawa

Kama zahanati ya Bunda, zahanati ya Ifinga Songea, zahanati ya Kiegei Nachingwea, zahanati ya Guta Bunda, hata sehemu ya kuhifadhia madawa katika zahanaati hizi ni tatizo na husababisha madawa mengi kuharibika kwa kuwekwa sehemu ambayo haina hewa ya kutosha.

Tatizo la uchakafu wa miundombinu ya kutolea huduma na uhaba wa madawa mbalumbali katika zahanati, vituo vya afya na hospitali hapa nchini litaisha lini? nani anastahili lawama juu ya tatizo hili? nani anatakiwa kuwajibika juu ya tatizo hili?

Watanzania wasio kuwa na hatia wanaendelea kupoteza maisha katika sehemu mbalimbali za vijijini na wengine kukimbia kujifungua katika vituo vya afya na zahanati na kwenda kwa wakunga wajadi kwa sabau ya ukosefu wa madawa na uchakavu wa miundombinu ya kujifungulia.

Umefika wakati sasa serikali kukaa chini na kufanya wajibu wake katika kutatua matatizo ya upatikanji wa huduma za afya hapa nchini, ili watumishi wa sekta hiyo na wagonjwa wawe na imani na uhakika wa kupata huduma za afya vijijini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *