CCM waendelea kuchapana makonde kugombea madaraka

Jamii Africa

BAADA ya kuripotiwa kupigana kwa wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), mkoani Dar es Salaam katika uchaguzi ndani ya chama hicho, ngumi zimeripotiwa sasa kutokea mkoani Mara.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, uchaguzi wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), mkoani Mara, umeingia dosari baada ya kuzuka vurugu kubwa zilizosababisha wajumbe kuchapana makonde mazito, kurushiana viti na mawe ndani na nje ya ukumbi.

Mapigano hayo makali ya wana CCM yaliyochukuwa takriban muda wa dakika 10 yalisababishwa na wafuasi wa mmoja wa wagombea wa nafasi ya mwenyekiti wa umoja huo, kumvamia Katibu Msaidizi wa CCM wilayani Tarime, Denis Zakaria na kuanza kumshushia kichapo cha ‘mbwa mwizi’, kwa madai kuwa alikuwa akiwahonga fedha wajumbe wa mkutano huo.

Vurugu hizo zimeibuka saa chache zilizopita, katika ukumbi wa CCM mkoa wa Mara, muda mfupi baada ya mgeni rasmi ambaye pia ni Mjumbe wa NEC kuitia wilaya ya Tarime na Kamanda wa Vijana wa CCM mkoa huo, Christopher Mwita Gachuma kufungua mkutano wa uchaguzihuo.

Baada ya hali hiyo mapigano hayo kuibuka, wajumbe wa mkutano huo kutoka wilayani Tarime walilazimika kutoka nje ya ukumbi, kisha kuanza kupambana na wafuasi hao kwa kurushiana ngumi kavu kavu, mawe na viti huku katibu msaidizi huyo wa CCM wilayani Tarime akitimua mbio na kuingia kwenye ofisi ya Katibu wa CCM wa mkoa kwa ajili ya kunusuru maisha yake.

Licha ya Katibu huyo wa CCM wilaya ya Tarime kutimua mbio, wajumbe hao walionekana kujawa hasira kali walimfukuza kwa mbio katibu huyo msaidizi, ambaye baadaye alifanikiwa kuingia na kujifungia ndani ya ofisi ya CCM mkoa huo.

Baada ya Katibu huyo kujificha ndani ya ofisi akikwepa kipigo wa wana CCM wenzake, wajumbe hao walionekana kutaka kumalizia hasira zao kwa mwandishi wa kituo cha Televisheni cha Channel Ten mkoani Mara, Mabere Makubi wakitaka kumnyang’anya kamera yake kwa lengo la kutaka kufuta mkanda wa ghasia hizo, lakini wakashindwa.

Mmoja wa watu walionusurika kipigo cha vijana hao, Arafat Idd kutoka wilaya ya Musoma mjini alimlalamikia mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mara aliyemaliza muda wake, Marwa Mathayo kwa madai ya kutaka kuhodhi nafasi zote zichukuliwe na wajumbe kutoka wilaya ya Tarime. Uchaguzi unaendelea sasa.

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Shy-Rose Bhanji amegaragazwa na Agnes Mathew katika nafasi ya ujumbe wa Baraza Kuu la UWT taifa kutoka mkoani Mara.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – FikraPevu, Musoma

2 Comments
  • hiyo ndio ccm watu hawa aminiani sasa sijui itakuwaje mwaka 2015 wakati wa uteuzi wa nafasi ya mgombea urais hali itakuwa mbaya sana binafsi naamini kwamba wenye ukwasi wa kutosha ndio watakao ibuka kidedea vinginevyo hali si shwari ndani ya chama cha mapinduzi. ngoja tusubiri.

  • huu ni mwanzo watazidi kupigana mpaka basi hii inamaanisha kuwa watu wamechoka sa siasa zisizoeleweka zenye lengo la kubebana,na watu kutotaka kuachia nafasi zao

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *