MWAKA 2016 wakati wa mojawapo ya vikao vya Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Rukwa, wajumbe walizizima kwa muda baada ya kupokea taarifa kuwa daktari mmoja mkoani humo alikuwa akihudumia wagonjwa 200,000.
Uwiano huo ni mara nane ya uwiano unaotakiwa kitaifa wa daktari mmoja kwa wagonjwa 25,000.
Aliyekuwa akikaimu nafasi ya Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk. Gasper Nduasinde, aliambia kamati hiyo kwamba, upungufu wa madaktari uliokuwepo ni sawa na asilimia 60 ya mahitaji.
Mkoa huo wenye jumla ya wakazi 1,048,892, kwa mujibu wa Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, una madaktari 10 sawa na asilimia 32 ya mahitaji, madaktari wasaidizi 59 sawa na asilimia 70 ya mahitaji na wauguzi 142 sawa na asilimia 25 ya mahitaji.
Aidha, mkoa huo unaelezwa kwamba una madaktari bingwa wawili, upungufu ambao umekuwa na athari kubwa kwa akina mama wajawazito na watoto waishio kwenye dimbwi la umaskini.
Katika kada ya wauguzi, uwiano wa kitaifa ni muuguzi mmoja kwa wagonjwa 5,000 lakini katika mkoa huo, muuguzi mmoja anahudumia wagonjwa 30,000.
Na Mkoa wa Rukwa usitegemee kama changamoto hiyo ya uhaba wa madktari itapatiwa ufumbuzi kesho ama keshokutwa hasa kutokana na uamuzi wa serikali wa kutoajiri watumishi wapya.
Licha ya kuwepo kwa upungufu mkubwa wa watendaji katika sekta ya afya, lakini mikoa ya pembezoni, ukiwemo Rukwa, imeleemewa zaidi na uhaba huo kiasi cha uwiano wa watumishi kwa wagonjwa kuwa changamoto kubwa kiasi cha kuwalazimu baadhi ya wananchi wa mikoa hiyo kwenda kutibiwa nchi za jirani kama Malawi na Zambia ambako wanasema huduma zinapatika kwa uhakika.
FikraPevu inatambua kwamba, uwiano kati ya daktari na wagonjwa nchini Tanzania ni daktari mmoja kwa wagonjwa 30,000, kiwango ambacho ni kikubwa kuliko uwiano wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wa daktari mmoja kwa wagonjwa 1,000.
Aidha, takwimu za WHO zinaonyesha kwamba Tanzania bado ina uwiano mbovu wa madaktari kwa wagonjwa, ambapo kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita ilikuwa inashika mkia kwa kuwa na uwiano wa daktari mmoja kwa wagonjwa 50,000.
Takwimu hizo zilionyesha kwamba, Tanzania ambayo kwa sasa ina idadi ya watu 49.25 milioni, ilikuwa na uwiano sawa na Malawi (yenye watu 16.36 milioni) na ndizo zilikuwa zinaburuza mkia kwa Afrika.
Afrika Kusini, Misri, Congo DRC na Nigeria zina idadi kubwa ya watu, lakini uwiano wa madaktari kwa wagonjwa unaridhisha kama siyo kukidhi kwa kiasi chacke.
Nigeria, nchi yenye watu 173.6 milioni na kuongoza Afrika, uwiano wake wa ni daktari mmoja kwa kila wagonjwa 3,571 wakati Afrika Kusini yenye wakazi 52.98 uwiano wake ni daktari mmoja kwa kila wagonjwa 1,299, na Misri yenye watu 82.06 ina uwiano wa daktari mmoja kwa wagonjwa 1,923.
Algeria yenye wakazi 39.21 milioni inashika nafasi ya pili keleleni nyuma ya Shelisheli, ambapo uwiano wake ni daktari mmoja kwa wagonjwa 884, ikiwa imevuka hata uwiano wa kimataifa.
FikraPevu inatambua kwamba, nchi jirani za Kenya, Congo DRC, Uganda na Rwanda ziko juu kwa uwiano kulinganisha na Tanzania.
Uwiano kwa nchi ya Kenya (idadi ya watu 44.35 milioni) ni daktari mmoja kwa wagonjwa 7,143, Congo DRC (watu 67.51 milioni) pamoja na vita visivyokwisha uwiano wake ni daktari mmoja kwa wagonjwa 9,090, Uganda (watu 37.58) uwiano ni 1:12,500, na Rwanda ni 1:20,000.
Ingawa serikali inasema imepunguza pengo la upungufu wa watumishi kutoka asilimia 58 mwaka 2011/12 hadi kufikia 51 mwaka 2015/16, lakini madaktari wasaidizi waliopo nni asilimia 9 tu ya mahitaji ya kitaifa katika sekta ya afya.
Kumbukumbu za FikraPevu zinaonyesha kwamba, wakati akiwasilisha wa kuboresha rasilimali watu katika sekta ya afya nchini, kwa wabunge wa Kamati ya Huduma za Jamii na Maendeleo ya Jamii, Meneja wa Mipango na Utetezi wa Sera kutoka Taasisi ya Benjamin Mkapa, Manka Kway, alisema mwaka 2014-15 kulikuwa na mahitaji ya madaktari wasaidizi 1,744, lakini waliopatikana ni 149 tu.
Tathmini hiyo ilifanyika katika wilaya 30 za mikoa saba ya Tanzania ambayo ni Geita (Bukombe na Chato), Iringa (Kilolo, Mafinga, Iringa, Mufindi), Kilimanjaro (Mwanga, Siha, Rombo, Hai, Moshi na Moshi Manispaa).
Mikoa mingine ni Mtwara (Tandahimba, Masasi, Mtwara, Manispaa ya Mtwara), Pwani (Kisarawe, Rufiji, Bagamoyo, Kibaha na Mji wa Kibaha), Ruvuma (Mbinga, Namtumbo, Songea na Mji wa Songea), Shinyanga (Shinyanga Manispaa na Halmashauri ya Shinyanga).
“Mahitaji ya madaktari wasaidizi kwa mwaka 2014-15 yalikuwa 1,744, waliokuwapo ni 149 na waliopungua 1,595 sawa na asilimia 91,” alisema Kway.
Aidha, mbali na madaktari wasaidizi, FikraPevu inatambua kuna upungufu wa maofisa wauguzi kwa asilimia 33, maofisa tabibu wasaidizi kwa asilimia 78, maofisa tabibu kwa asilimia 26, wauguzi kwa asilimia 72, maofisa wauguzi kwa asilimia 53 na wataalamu wa maabara kwa asilimia 37.
Inaonyesha pia kwamba, wakati sekta ya afya inakabiliwa na uhaba wa rasilimali watu kwa asilimia 52 kwa mujibu wa ikama ya mwaka 2014, zaidi ya asilimia 74 ya madaktari waliopo wanafanya kazi maeneo ya mijini.
Kulingana na taarifa zilizopo, wakati daktari mmoja anahudumia wagonjwa 78,880 maeneo ya vijijini, daktari mmoja mijini anahudumia wagonjwa 9,095.
Kufuatia changamoto hiyo, kuna uwezekano wa kutofikiwa kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDG) nchini Tanzania na ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambalo lina wakazi zaidi ya 700 milioni na lenye kubeba 24% ya msigo wa magonjwa duniani.
Lengo namba tatu la SDG linahimiza kuhusu afya bora na ustawi.
Serikali inasema kwamba inaendelea kutekeleza Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) kwa kuongeza idadi ya wanafunzi watarajali wa ngazi ya kati katika vyuo vya afya na kufikia 11,192 kwa mwaka.
Lakini kwa mwaka 2014 hadi 2015 serikali haikuajiri madaktari licha ya kuwepo kwa zaidi ya wahitimu 2,000.
Hali hii imesababisha madaktari wengi kuamua kwenda kufanya kazi kwenye mashirika au taasisi binafsi, na waliobahatika wameajiriwa nchi za nje.
Mchangiaji mmoja kupitia mtandao wa JamiiForums anasema, tatizo la upungufu wa madaktari linafugwa na serikali ambayo inafanya makosa kwa kuchelewa kuwaajiri kwa wakati madaktari waliomaliza masomo yao na mafunzo kwa vitendo.
“Lakini pia kuwepo kwa idadi ndogo ya wanafunzi wanaodahiliwa kwenye vyuo katika fani ya udaktari… kipindi cha nyuma hali hii ilichangiwa na vikwazo vilivyowekwa katika kiwango cha ufaulu ambapo ilikuwa ni lazima anayejiunga na masomo ya udaktari chuo kikuu awe na ufaulu wa daraja la kwanza,” anasema mchangiaji kupitia JamiiForums.
Suala jingine analolizungumzia ni mishahara isiyoendana na ugumu wa kazi.
Changamoto hizi zote zinaweza kutatuliwa kwa serikali kukubali kujifunza na kubadilika, ikiwa ni pamoja na kutenga bajeti maalum kwa ajili ya kuajiri madaktari wanaomaliza mafunzo kwa vitendo mapema iwezekanavyo.