Daladala zagoma Tarime, abiria wakesha stendi

Sitta Tumma

MADEREVA wa magari madogo ya kusafirisha abiria, maalufu kwa jina la ‘daladala’ Wilayani Tarime mkoani Mara, wamegoma kusafirisha abiria wakishinikisha Mamlaka ya Usafiri wa nchi Kavu na Majini (SUMATRA), iruhusu magari yao yatoze bei kubwa ya nauli kulingana na kupanda kwa bei ya mafuta nchini.

Kutokana na mgomo huo ulioanza tangu janai, baadhi ya abiria waliokuwa wakisafiri kutoka Tarime kwenda sehemu nyingine, walilazimika kulala kwenye stendi ya magari mjini hapa wakisubiri usafiri, jambo ambalo hadi kufikia jana magari hayo yalikuwa yamegoma kufanya kazi zake.

Mwandishi wa habari hizi alijionea leo kwenye stendi kuu ya mabasi mjini Tarime mamia ya wananchi wakiwa wamekosa usafiri, huku baadhi ya daladala na zile ‘mchomoko’ zikiwa zimepaki kwenye stendi hiyo bila kufanyakazi zake za kusafirisha abiria.

 

tarime-leo

tarime-leo

Baadhi ya abiria wakiwa kwenye stendi ya Tarime mjini wakiwa wamekosa usafiri baada ya daladala kugoma tangu jana na leo. (Picha zote na Sitta Tumma).

Wakizungumza na FikraPevu leo kwenye stendi hiyo, baadhi ya abiria, madereva na maajenti wa magari hayo, walisema wamelazimika kufanya mgomo huo baada ya Sumatra kuwazui kutoza nauli mpya waliokuwa wamejipangia wenyewe kulingana na kupanda kwa mafuta pamoja na uendeshaji wa magari hayo.

Silvester Emmanuel ambaye ni ajenti wa magari ya abiria wilayani hapa, alisema kwamba, Sumatra imewaamuru kutoza nauli ya sh. 700 badala ya 1,500 kutoka Tarime kwenda Sirari, sh. 2,900 badala ya 4,000 kutoka mjini hapa kwenda Musoma.

Alisema, nauli ya sh. 5,000 waliyokuwa wameanza kutoza abiria kutoka Tarime mjini kwenda Shirati wilayani hapa wameamuliwa na Serikali kutoza sh. 2,900, huku nauli mpya ya sh. 9,000 kwenda jijini Mwanza kwa sasa imepunguzwa na Sumatra hadi kufikia sh. 6,200 jambo ambalo wanalipinga.

“Tunasema hatutoi magari yetu, vinginevyo Serikali ilete magari yake isafirishe abiria kwa bei hii ndogo. Lita moja ya mafuta hapa Tarime ni sh. 2,500 maana yake ukisema upeleke watu Musoma ukubali kula rosi ya kukopa hela pembeni.

“Mfano, kutoka Tarime kwenda Sirari ni kilometa 25, lakini tunaambiwa na Sumatra tutoze nauli ya sh. 700. Tarime Mwanza kilometa zaidi ya 290 tunaambiwa nauli sh. 6,200 huku lita moja ya mafuta tunanunua 2,500 hivi hii ni sawa?”, alihoji Emmanuel huku madereva na baadhi ya makondakta wakimuunga mkono.

Kulingana na hali hiyo, madereva na makondakta pamoja na maajenti hao wa magari waliapa kutoingiza magari yao barabarani kusafirisha abiria kwa bei hiyo ya Serikali, badala yake waliitaka serikali ipeleke magari yake ya kifahari yakaanze kazi ya kusafirisha abiria kwa gharama hiyo ya mafuta, iwapo kama wataweza.

“Abiria wanakubali kulipa nauli hii mpya. Serikali nayo inatuambia vijana tufanyekazi, lakini mbona inazuia tena?. Tukale wapi, au twende kuwa ombaomba kwa watumishi wa serikali wanaotembelea VX?. Tunasema hatutoi magari hadi kieleweke”, alisema dereva mmoja.

Kwa upande wake, mwanamke mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mama Nyanjige, yeye alisema stendi hapo kwamba, jana amelazimika kulala njaa stendi akisubiri usafiri wa kutoka Tarime kwenda jijini Mwanza, na aliiomba Serikali iruhusu watu wasafirishwe na baadaye wakae pamoja kujadili suala hilo.

Ofisa Ukaguzi wa Sumatra Kanda ya Ziwa, Alfred Wariana alipoulizwa kuhusiana na mgogoro huo, alisema: “Kwanza nipo rikizo, lakini hao madereva wamejipangia nauli wenyewe bila kushirikisha mamlaka husika. Hivyo Serikali haiwezi kuruhusu upandishwaji wa nauli kienyeji”.

Mkuu wa wilaya ya Tarime, John Henjewele alipotakiwa kuzungumzia suala hilo alisema yupo kwenye mapokezi ya mbio za Mwenge, hivyo akaahidi kuwasiliana na mamlaka husika ili suala hilo lipatiwe ufumbuzi, ikiwezekana hatua zinazotakiwa zichukuliwe.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – FikraPevu, Tarime

2 Comments
  • Sumatra itakuwa inajiingiza matatani kila wakati kwa kujiingiza kupanga bei ya nauli na upandaji wa mafuta kiholela

  • Mara nyingi wananchi wanailaumu serikali kuwa haitekelezi majukumu yake ipasavyo, lakini pale inapofanya vizuri inabidi tuunge mkono 100%. Sasa hili la SUMATRA kupunguza nauli kwa mabasi Tarime ni swala moja la busara sana kwani wanachi wa wilaya mbalimbali katika mkoa huo (Mara) wamekuwa wakilanguliwa sana kwenye nauli huku madereva, makondakta na wamiliki wakitumia kigezo cha kupanda kwa mafuta.

    Sasa tuchukue ulinganisho mdogo tu: Tunaamini kuwa mafuta mikoani ni ghali kuliko Dar es Salaam, lakini tuchukulie tofauti kati ya Dar na tarime, Dar mafuta Diesel na Petrol iko kati ya 2,150/- na 2,300/- na Tarime haizidi 2,500/-, tofauti hapo unakuta ni 16% hadi 9% ya bei ya Dar.

    Sasa turudi Kwenye umbali: Umbali kutoka Ubungo (Dar) kwenda Kongowe (kibaha) na kutoka Tarime kwenda musoma haziachani kabisa. Lakini nauli kutoka Dar kwenda Kongowe ni Kati ya 1,500/- hadi 2,000/- kama sikosei. Lakini Kutoka Tarime kwenda musoma nauli ni 4,000/- hadi 5,000/- tofauti hapo ni 160% hadi 100% ya bei ya Dar-Kongowe. Na hapo hatujazungumzia maeneo mengine kama tarime kwenda shirati ambapo nauli inafikia hadi 5,000/- kwa umbali usiozidi km 50, hata kama ni barabara ya changarawe.

    Sasa linganisha tofauti ya asilimia za mafuta na asilimia za nauli. Je, watu wa Tarime na wilaya nyingine  hawalanguliwi kwenye nauli? Kigezo sasa ni nini kama zote (dar-kongowe na tarime-musoma) ni barabara za lami? Sumatra fanyeni kazi yenu, mkiwaacha mtaonyesha uzembe mkubwa sana na mtakuwa hamjawasaidia wananchi wa maeneo hayo.

    Jamani naombeni niwe mwkilishi wa Jamii Forum Rorya maana kule pia kuna matatizo mengi, ili niwe nakusanya habari za kule maana nimependezwa na jinsi website hii unavyopasha watu habari kwa njia ya internet, kwa 500/- tu nitasoma habari kibao badala ya kununua gazeti moja.

    Ahsanteni,

    David Charles Andata, (rorya native) 0752417401 / 0687417402

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *