Dondoo muhimu ili kupata usingizi wa uhakika

Jamii Africa
Woman sleeping on bed in hotel room, close-up

Kufanya kazi  ni sehemu ya maisha ya binadamu yeyote. Mtu asipofanya kazi huugua kwasababu mwili unashindwa kujiendesha na kuzalisha seli mpya ambazo zinatakiwa zitumike. Kwa kila anayefanya kazi huchoka na huitaji mapumziko.

Mapumziko huwa  wakati wa usiku ambapo mtu huacha kila kitu na kupanda kitandani kulala ili kuurudisha mwili katika hali ya kawaida. Wapo watu wakifika kitandani wanakosa usingizi kabisa au wengine wanachelewa kupata usingizi. Wataalamu wa afya wanashauri mtu kulala masaa 6 hadi 8 kwa usiku mmoja ili kuufanya mwili kuwa na afya bora.

Tafiti  zinaonyesha kuwa asilimia 25 ya watu wazima wanasumbuliwa na matatizo ya usingizi na asilimia 6 hadi 10 wanasumbuliwa na tatizo la kukosa usingizi.

Imewalazimu baadhi ya watu kutumia vidonge vya usingizi lakini bado tatizo haliishi. Baadhi ya tabia ambazo zinasababisha mtu akose usingizi, husababishwa na mabadiliko ya mazingira ya sehemu ya kulala kama vile kuwa kwenye mazingira ya baridi kali, moshi au harufu mbaya.

Sababu nyingine ni mabadiliko ya muda wa kulala tofauti na mtu alivyozoea. Lingine ni makelele katika maeneo ya makazi, muziki wenye midundo mizito na sauti ya juu au vurugu. Mambo mengine ni msongo wa mawazo, wasiwasi, woga na hofu zitokanazo na matatizo ya kimaisha kama vile kukosa fedha, matatizo ya kifamilia na ugomvi wa wanandoa .

Zingatia mambo yafuatayo ili upate usingizi wa kutosha na wenye uhakika:

  1. Lala kwa muda muafaka

Panga muda sahihi wa kulala kila siku, mfano unaweza kukusudia kulala kila ifikapo saa 3 usiku na kumka saa 12 asubuhi. Ukiupangia mwili ratiba utatii na muda wa kulala ukifika utajikuta unapata usingizi wa uhakika.

 

  1. Epuka mazoezi muda mfupi kabla ya kulala

Mazoezi ni muhimu lakini yanapaswa kupangiwa muda wake ambao hauingiliani na muda wa kulala. Ukifanya mazoezi  joto la mwili linapanda na linachukua muda kupungua na kurudi katika hali kawaida. Inashauriwa kufanya mazoezi masaa 5 kabla ya kwenda kulala.

 

  1. Usitumie eneo la kulala kwa shughuli nyingine

Chumba ambacho kimetengwa maalumu kwa ajili ya mapumziko hakipaswi kutumika kwa shughuli nyingine. Mfano kutumia chumba kama sehemu ya kusomea au kula chakula. Chumba cha kulala ni kwa matumizi mawili tu yaani kulala na kufanya tendo la ndoa.

Epuka kuangalia runinga (TV) au kusikiliza radio ukiwa kitandani utakuchukua muda mrefu kupata usingizi. Jaribu kadri uwezavyo kukifanya chumba cha kulala kuwa na mazingira yanayovutia kupata usingizi.

  1. Jiandae kisaikolojia

Kila jambo tunalofanya linaanzia kwenye ubongo ambako shughuli zote za mwili huratibiwa. Jitahidi kuielekeza akili katika kulala. Wakati kulala sio wa kufikiri mambo yaliyotokea mchana au mambo mabaya yaliyotokea.

Ukiruhusu akili yako kufikiri hayo utakosa usingizi na utaingiwa na wasiwasi na kuhofia matukio hayo kujirudia tena usiku. Fahamu mambo yaliyotokea hayawezi kutokea tena, pia jitathmini mwenyewe uko wapi na unafanya nini kwa wakati huo.

 

  1. Epuka kunywa pombe, kahawa na tumbaku kabla ya kulala

Vinywaji na vilevi hivyo vina ‘caffeine’ ambayo huondoa usingizi. Vinywaji kama pombe na kahawa huamsha mwili na kuufanya mwili uchangamke na ukivitumia muda mfupi kabla ya kulala itakuchukua muda mrefu mpaka upate usingizi.

Kumbuka dondoo hizi ni njia rahisi zitakazokusaidia kupata usingizi wa uhakika. Ikiwa baada ya kutumia njia hizo hapo juu bado unakosa usingizi,  muone daktari akusaidie kwa matibabu zaidi.

 

 

 

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *