Elimu Bure mkoani Rukwa: Shule saba zaandikisha watoto 5,300 darasa la kwanza na awali Nkasi

Jamii Africa

WATOTO wapatao 5,354 wameandikishwa darasa la kwanza na awali katika shule saba zilizopo Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa mwaka huu katika mwitikio wa mpango wa elimumsingi bure, hali iliyosababisha msongamano mkubwa, FikraPevu imebaini.

Uchunguzi unaonyesha kwamba, shule hizo saba zimeandikisha wastani wa 600 hadi 960 kwa madarasa ya awali na la kwanza na kusababisha shule moja kuwa na idadi ya wanafunzi kati ya 2,000 hadi 3,000 kutoka darasa la awali hadi saba.

Akizungumza na FikraPevu wakati wa ya kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Ofisa Elimu wa Halmashauri hiyo, Missana Kwangura, alisema uandikishwaji huo mkubwa wa watoto wa darasa la kwanza na awali na umesababisha mrundikano mkubwa madarasani.

Alizitaja shule hizo saba za msingi na idadi ya wanafunzi wa darasa la kwanza na awali kwenye mabano Kirando (963), Mtakuja (910), Swaila (841), Mkinga (703), Itete (691), Paramawe (650) na Korongwe (596).

“Uandikishaji mkubwa wa watoto wa awali na darasa la kwanza uliofanyika katika baadhi ya shule za msingi wilayani humu umesababisha shule kuwa na idadi ya wanafunzi kati ya 2,000 na 3,000 kuanzia awali hadi darasa la saba,” aliieleza FikraPevu.

Alisema kuwa halmashauri hiyo yenye shule za msingi za umma 103 zina jumla ya wanafunzi 78,144, wavulana wakiwa 38,006 na wasichana 40,138, lakini zinakabiliwa na upungufu wa madawati 5,152, vyumba 1,087 vya madarasa na matundu 2,407 ya vyoo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Julius Kaondo alisema ili kukabiliana na uhaba wa vyumba vya madarasa katika shule za msingi, Mkuu wa Wilaya (Said Mtanda) ameagiza kila shule ihakikishe inajenga vyumba vya madarasa vitatu na kwamba viwe vimekamilika ifikapo Aprili Mosi mwaka huu.

“Kufuatia uandikishaji mkubwa wa awali na darasa la kwanza zipo shule ambazo zimeandikisha zaidi ya watoto 900 na kusababisha siyo tu msongamano mkubwa madarasani, lakini pia uhaba wa madawati, vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo.

“Lakini tayari DC amekwishaagiza kila shule – kwa maana hiyo serikali za vijiji – kujenga vyumba vitatu vya madarasa ili kukabiliana na changamoto hiyo,” alisema Kaondo katika mahojiano na FikraPevu.

Baadhi ya madiwani waliohojiwa na FikraPevu walikiri kuwa shule zote za msingi za umma zinakabiliwa na changamoto hizo ambapo watoto wengi wanalazimika kusomea nje wakiwa wameketi chini huku wengine wakilazimika kwenda na vigoda kutoka nyumbani ili kukalia.

Uandikishwaji huo unatajwa kuongezeka kutokana na mpango wa serikali wa elimumsingi bure, ambapo wazazi wengi waliokuwa wakilemewa na mzigo wa michango na ada huku vipato vikiwa vidogo, wamehamasika kuwapeleka watoto wao shule mapema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *