DHANA ya ‘Elimu Bure’ kwa kila mtoto wa Tanzania imeshindwa kuendana na uboreshaji wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia ambapo wanafunzi wa shule za msingi Kasindaga na Mshanje wilayani Muleba katika Mkoa wa Kagera wako katika hali mbaya, FikraPevu inaripoti.
Uchunguzi unaonyesha kwamba, mazingira ya utoaji wa elimu bora katika shule hizo ni magumu kutokana na kukosekana kwa miundombinu, hususan ya madarasa, madawati pamoja na vyoo.
FikraPevu imebaini kwamba, katika Shule ya Msingi Kasindaga iliyoko Kata ya Kyebitembe, wanafunzi wanalazimika kujisaidia vichakani na kwenye vyoo vibovu, hali ambayo inahatarisha usalama wao wa afya na kudunisha taaluma.
FikraPevu ilishuhudia wanafunzi wakipanga foleni kwenye vyoo vya makuti, huku wengine wakikimbilia vichakani kujisaidia.
Hali hiyo ipo pia katika Shule ya Msingi Nshanje ambayo iko ndani ya Kata hiyo ya Kyebitembe, ambapo licha ya kwamba vyoo hivyo vimesilibwa kwa makuti, lakini pia mazingira ya ndani si salama kwa kuwa kuna magogo tu yaliyowekwa na sehemu kubwa ya mashimo ikiwa wazi, hali ambayo ni ya hatari zaidi.
Inaelezwa kuwa, usalama mdogo katika kutumia vyoo hivyo vinavyoweza kusababisha wanafunzi wakatumbukia, ndio unaowafanya wanafunzi wengine, hasa wa elimu ya awali ambao ni wadogo, wakimbilie vichakani kujisaidia.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kasindaga, Dawson Julius, alisema mbele ya mkutano wa kijiji hicho kwamba, wanafunzi wanateseka katika kupata maarifa ambapo kipindi cha mvua wanaweza kupata magonjwa ya mlipuko kwani baadhi yao hawana viatu na wanaingia peku chooni.
Julius alisema ufundishaji katika shule hiyo unawapa wakati mgumu kwani mara nyingi wanafunzi hulalamika kuugua magonjwa ya tumbo huku kukiwa hakuna huduma za afya baada ya zahanati ya kijiji kuishia kuezekwa miaka kadhaa iliyopita bila kutumika kwa kukosa waganga na vifaa tiba.
Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 730 – wavulana 433 na wasichana 297 – ambapo yanahitajika matundu 27 kwa ajili ya wavulana na matundu 15 kwa ajili ya wasichana.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Nshanje, Kata ya Kyebitembe, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera wakiwa kwenye foleni ya kupata huduma ya choo ambapo vyoo hivyo vya muda vimejaa, hivyo kuwafanya watoto wa darasa la awali hadi la tatu kujisaidia nje wakiogopa kuanguka ndani kwa kuwa matundu yamefunikwa na mabanzi yaliyoanza kuoza. Picha na Shaaban Ndyamukama.
Aidha, shule hiyo haina choo hata kimoja kwa ajili ya walimu, hali inayowalazimu kuomba hifadhi katika nyumba za jirani, jambo ambalo huwapa usumbufu mkubwa nyakati za masika.
“Changamoto ya vyoo ni ya muda mrefu na hali hii inatisha sanjali na kupata magonjwa ya minyoo. Sheria zingekuwa zinafuatwa, shule hii ingefungwa hadi kukamilika kwa matundu ya vyoo vya walimu na wanafunzi,” Mwalimu Julius aliieleza FikraPevu.
Mwalimu Julius alisema kwamba, shule hiyo haina mwalimu wa kike kwa muda mrefu, hivyo kuwafanya wanafunzi 297 wa kike kukosa mtu wa kusikiliza kero zao za kimaumbile
“Wanafunzi hawa wa kike wanakosa haki yao ya msingi ya elimu ya kimaumbile, maana mwanamume hawezi kuwaelekeza hata namna ya kujihifadhi wanapokuwa kwenye hedhi, Halmamshauri ya Wilaya ya Mulemba haijawasambaza walimu wa kike katika shule za kijiji hicho kwa madai ya kukosa nyumba za kuishi, changamoto nyingine ambayo inakwamisha maendeleo ya elimu,” alisema.
Hali kama hiyo imetajwa na Kaimu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nshanje, Joseph Sanga, aliyesema kwamba wanafunzi wa shule hiyo wanatumia vyoo vilivyozungushiwa matete na nyasi ambavyo wakati wa mvua huvuja.
“Wanafunzi wa darasa la awali hadi la tatu wanajisaidia popote hata kwenye mashamba ya shule na kusababisha uchafuzi wa mazingira, lakini wako hatarini kiafya,” Sanga aliiambia FikraPevu.
Alisema shule hiyo, ambayo iko nje ya kijiji jirani na Hifadhi ya Biharamulo, tangu ianzishwe walimu wanatembea umbali wa kilometa 18 kila siku kwenda kufundisha na kurejea makao makuu ya kijiji cha Kasindaga kuliko na nyumba za kupanga kwani huko hakuna nyumba za walimu.
Sanga alisema kwamba, wananchi, kupitia mpango wa nguvukazi, walijenga nyumba moja ya walimu ambayo imekwamia kwenye renta kwa miaka 10 sasa.
“Walimu wanateseka kwa kutumia gharama kubwa za kukodi usafiri huku wakiwa ombaomba kwenye magari yanatoka na kwenda Muleba mjini katika barabara kuu ya Biharamulo-Bukoba, jambo linalohatarisha usalama wao,” aliiambia FikraPevu.
Aidha, alisema kwamba wanafunzi wa darasa la tatu hadi la tano shuleni hapo wanasomea chini ya miembe kwa kukosa vyumba vya madarasa, hali inayowakosesha usikivu kwani miembe hiyo iko kandokando ya barabara za vijiji na barabara kuu ya Biharamulo-Muleba
“Wanafunzi na walimu husumbuliwa na kelele za pikipiki na magari huku wakipata adha ya mvua na jua,” alisema wakati akiongea na FikraPevu.
Uhaba wa vyumba vya madarasa katika shule hizo mbili ni mkubwa, ambapo Shule ya Kasindaga inahitaji vyumba 16, kwani vyumba vitano vilivyopo vinatumiwa na wanafunzi wa darasa la awali hadi la tatu na darasa la saba, wakati madarasa mengine wanasomea chini ya miembe na wakati mwingine huchanganyika katika chumba kimoja.
Shule ya Msingi Nshanje yenye wanafunzi 430 inatumia vyumba vitatu kati ya 10 kutokana na vingine kutokamilika, huku walimu tisa wa shule hiyo ambao wote ni wa kiume, wakiwa wanakuja na kuondoka kila siku.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kasindaga, Mathias Bishobo, amethibitisha kuwepo wa changamoto hizo na kwamba wananchi wanajitahidi kuchangia vifaa vinavyopatikana kwenye mazingira yao ili kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia na kuiomba serikali kuchangia vifaa vya ujenzi kutoka viwandani.
Alisema Serikali ya Kijiji ilijenga nyumba ya miti kwa ajili ya walimu wa Shule ya Msingi Nshanje ili kuwapunguzia adha ya kutembea kilometa 18 kila siku.
“Nyumba hii imeezekwa tu mabati na haijakandikwa udongo baada ya kutokea ukame na kushindwa kupata maji karibu,” Bishobo aliieleza FikraPevu.
Alisema katika Shule ya Kasindaga, ujenzi wa darasa moja umefikia hatua ya kuezeka na kwamba mpaka kukamilika litagharimu Shs. 12 milioni.
Aidha, katika Shule ya Nshanje wananchi wamekusanya vifaa vinavyopatikana katika mazingira yao na ujenzi wa darasa utaanza ndani ya wiki tatu zijazo.
Ofisa Elimu Idara ya Msingi wilayani Muleba, Charles Katarama na Mbunge wa Jimbo la Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka, wamekiri shule hizo kukumbwa na changamoto ya uhaba wa matundu ya vyoo na vyumba vya madarasa na kwamba wananchi waendelee kuchangia rasilimali zinazowazunguka.
Mwalimu wa darasa la tatu katika shule ya msingi Kasindaga, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, Joseph Zacharia Msuya, akifundisha wanafunzi chini ya miembe kutokana na shule hiyo kukabiliwa na uhaba wa vyumba vya madarasa.