Elimu duni, vitisho vyachangia asilimia 60 ya wananchi kukosa uhuru wa kumkosoa rais

Jamii Africa

Moja ya nguzo kuu za demokrasia ni uwepo wa uhuru na haki ya wananchi kuwa na maoni na kujieleza. Uhuru huo kimsingi huenda sambamba na uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kutafuta na kupokea taarifa.

Hapa nchini Tanzania uhuru wa kujieleza unalindwa na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 katika Ibara ya 18.

Sambamba na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, ipo mikataba ya kimataifa na kikanda ambayo inalinda uhuru wa kujieleza. Tamko La Ulimwengu La Haki Za Binadamu (Universal Declaration of Human Rights 1948) pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Haki za Watu; Ibara ya 19 inatoa haki na uhuru wa kila mtu kuwa na maoni yake na kujieleza bila mawasiliano yake kuingiliwa.

Nayo Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, kifungu cha 52 (2) (a) na (b), inaruhusu vyombo vya habari au mwananchi kutoa maoni yake kwa ajili au dhidi ya Serikali kwa lengo la kuweka sawa jambo lolote katika jamii.

Licha ya kuwepo mikataba ya kimataifa, katiba na sheria bado dhana ya uhuru wa kujieleza na kuwakosoa viongozi waliopo madarakani nchini inakabiliwa na changamoto mbalimbali ambapo uhuru huo umepungua na baadhi wa raia walinaojaribu kutoa maoni yanayotofautiana na serikali wamekuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kuitwa ‘wachochezi’.   

Kulingana na utafiti wa taasisi ya Twaweza (Machi, 2018) juu ya Sauti za Wananchi: ‘Siyo kwa kiasi hicho’, unaeleza kuwa tangu kuingia madarakani kwa serikali ya awamu ya tano, wananchi wengi hawana uhuru wa kuikosoa serikali pale inapokesea hasa viongozi waandamizi akiwemo rais.

“Idadi kubwa ya wananchi (60%) wanasema hawako huru kukosoa kauli zinazotolewa na Rais wakati asilimia 54 wanasema hivyo kuhusu kauli zinazotolewa na Makamu wa Rais na asilimia 51 Waziri Mkuu”, inaeleza sehemu ya ripoti ya utafiti wa Twaweza.

Kwa tafsiri rahisi ni kuwa wananchi 6 kati ya 10 hawana ujasiri kukosoa au kutofautiana na kauli anayoitoa rais hata kama haikisi matakwa ya katiba na sheria za nchi.

 

Serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani mwaka 2015, imekuwa ikikosolewa kutokana na mtazamo wake kuhusu uminyaji wa uhuru wa kuzungumza na uhuru wa vyombo vya habari.

Wanasiasa na watu wamekuwa wakikamatwa kwa ‘kosa’ la kuikosoa serikali (uchochezi), mara nyingi wakituhumiwa kwa ‘uchochezi’ au kwa makosa yaliyomo chini ya Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015.

Hata hivyo, wananchi wengi wako huru zaidi kuwakosoa viongozi wa ngazi ya chini hasa wale kuchaguliwa wakiwemo wabunge, madiwani, wenyeviti wa vijiji kwasababu wanafikiri wana dhamana ya kuwatumikia kulingana na matakwa yao. Lakini uhuru wa kuwakosoa unapungua zaidi kwa wateule wa rais; wakuu wa mikoa na wilaya.

“Wananchi wanajisikia huru zaidi kuwakosoa viongozi katika ngazi za chini za serikali au viongozi wenye mamlaka ndogo. Wananchi nane kati ya kumi wanasema wanajisikia huru kuwakosoa mwenyeviti wa vijiji/mitaa (83%), viongozi wa vyama vya upinzani (77%), madiwani (76%)”, inaeleza ripoti hiyo na kuongeza kuwa,

“Hii inaweza kuwa ni kwa sababu wananchi wanawachagua wabunge kama wawakilishi wao na hivyo wanaona kuwa mbunge ana jukumu la kusikiliza mahitaji na vipaumbele vyao na kuvifanyia kazi ipasavyo. Vinginevyo, inawezekana wananchi wanaona kuwa wakuu wa mikoa na wilaya wanaonekana wapo karibu na Rais”.

Kinachowafanya wananchi wengi wakose ujasiri wa kumkosoa rais, makamu wa rais au waziri mkuu kwa uhuru kama wanavyofanya kwa viongozi wa kuchaguliwa ni kutokana na imani iliyojengeka kuwa taarifa au kauli zinazotolewa na viongozi hao zinaaminika na ni vigumu kuzipinga au kutofautiana nazo.

“Idadi kubwa ya wananchi wanasema ‘wanaamini kabisa’ taarifa zinazotolewa na Rais (70%) au Waziri Mkuu (64%). Wananchi wengi wanaamini ‘kwa kiasi fulani tu’ taarifa zinazotolewa na viongozi wengine huku taarifa zinazotolewa na wabunge wa vyama vya upinzani, wanachama na wafuasi wake zikichukuliwa kwa tahadhari”, inafafanua zaidi ripoti hiyo.

 

Akizungumza na FikraPevu juu ya matokeo ya utafiti huo, aliyewahi kuwa Mchambuzi Mkuu wa Sera wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Prof.  Morjorie Mbilinyi amesema kila kinachotajwa  kuwa wananchi hawana uhuru wa kumkosoa rais kwasababu ya wadhifa alionao sio dhana yenye nguvu lakini imetokana na uoga wa viongozi kutopenda kuelezwa ukweli au kuhojiwa mambo ya msingi yanayogusa maisha wananchi.

Amesema kuwa kukosoa ni wajibu wa wananchi kwasababu umejengwa katika misingi ya katiba na sheria na pale wanapoona mambo yanaenda wasivyotarajia lazima waseme na viongozi wawasikilize ili kukidhi mahitaji ya jamii.

Lakini bado watu ambao wanatumia haki yao kikatiba kutoa maoni na kuwakosoa viongozi waliopo madarakani ikiwemo rais wamekuwa wakikabiliwa na vitisho na kufunguliwa kesi za ‘uchochezi’ wakidaiwa kuhatarisha amani na kuichonganisha serikali na wananchi.

Hivi karibuni, Mbunge wa Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi  alihukumiwa kifungo cha miezi sita gerezani kwa kosa la kutoa kauli zinazodhniwa kuwa za kashfa dhidi ya rais John Magufuli.  Naye Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu mara kadhaa amejikuta katika tafrani na vyombo vya dola kwa kile kinachotajwa kuwa ni ‘mchochezi’ anayetofautiana na serikali.

Lissu alishambuliwa kwa risasi na watu ‘wasiojulikana’ akiwa mjini Dodoma muda mfupi baada ya kumalizika kwa vikao vya Bunge mwezi Septemba mwaka jana. Tukio hilo lilitokea siku wiki mbili baada ya Lissu kutoa taarifa kuwa ndege zilizoagizwa na serikali nchini Canada zilizuiliwa kwasababu Tanzania haikuliipa fidia kampuni moja ya ujenzi iliyopo nchini humo.

Watumiaji wa mitandao ya kijamii, wanaharakati na wanasiasa mbalimbali nao wamekuwa wakipata usumbufu, vitisho pale wanapokosoa mwenendo wa serikali, jambo linajenga  hofu na woga kwa wananchi kutimiza wajibu na haki zao za kutoa maoni na kujieleza.

 

Wadau watoa ya moyoni

Akitoa maoni yake juu ya matokeo ya utafiti wa Twaweza, Mkurugenzi wa Utetezi kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia amesema wananchi wengi hawako huru kumkosoa rais kwasababu ya kutokuwa na elimu ya kujitambua na uwezo wa kujenga hoja zinazoweza kuwawajibisha viongozi waliopo madarakani.

“Watu hawakosoi wala kuhoji hapa nchini kwa sababu ya aina ya elimu yetu, tunafundishwa tu kukubaliana na mamlaka ndio maana hata 'wanaoamini kabisa' taarifa zitolewazo na Rais ni wengi sana. Na hili si tatizo letu pekee ni dilemma ya Afrika nzima”, amesema Sungusia.

Ameongeza kuwa serikali inapaswa kufungua milango ya kuambiwa ukweli ili kupata mawazo mbadala kuelekea kwenye uchumi wa viwanda.Tukitaka kuelekea Tanzania ya Viwanda tunahitaji watu skilled (wenye ujuzi) na skills hizo (ujuzi huo) hatuwezi kuzi-nurture (kuukuza) kama hawazungumzi. Inabidi watu wazungumze ili tuweze kujua wana nini ndani yao”.

Kwa upande wake, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt. Vicensia Shule amesema woga au hofu ya wananchi kumkosoa rais ni mamlaka aliyonayo na si vinginevyo.

“Kwa nini watu wanaogopa kumkosoa rais, ni suala la mamlaka unajua ukiwa na kipato kikubwa, mamlaka watu watakuogopa. Kwahiyo ni suala tu kwamba angekuwa kama yeye sio rais huenda angekuwa anakosolewa kwa asilimia 99.9”, ameweka wazi Dkt. Vicensia na kuongeza kuwa,

“Unayeogopwa kukosolewa sio rais ni mamlaka inayoogopwa, tunapotafsiri kwamba watu wanaamini taarifa inazotoa mamlaka, ni kama polisi anapokuambia kaa chini hakuna option (chaguo) nyingine zaidi ya kukaa la sivyo utapigwa virungu”.

Ameshauri kuwa viongozi wakubali kukosolewa na kuambia maneno wasiyoyapenda kwasababu kuna nyakati na wao wanawatolea wananchi lugha za kibaguzi, dharau zenye lengo la kudhoofisha umoja wa kitaifa.

“Utafiti huu unaonesha kuwa wananchi hawapendi kutukanwa wala kukejeliwa hivyo Viongozi nao wajue kama ambavyo hawapendi kutukanwa nasi ni hivyo hivyo. Pia Uongozi ni jalala; Viongozi wavae ngozi ngumu”, ameshauri Dkt. Vicensia.

Mchambuzi Mkuu wa Sera wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Prof.  Morjorie Mbilinyi akitoa maoni yake juu ya matokeo ya utafiti wa Twaweza

 

Serikali yaweka wazi msimamo wake…

Akizungumza kwa niaba ya serikali, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas amesema kukosoa sio kosa lakini watu wanapaswa kujifunza jinsi ya kutoa maoni yao kwa njia sahihi inayozingatiwa wajibu na  kuheshimu mamlaka zilizopo madarakani.

Rais ni mtu mkubwa sana hata kumkosoa kunahitaji taratibu fulani. Kwenye familia unaweza kumkosoa kaka lakini baba huwezi kumwambia 'umebugi'”. Amesema Dkt. Abbas.

Amesema rais anashaurika na amekuwa akipokea maoni ya watu mbalimbali kinyume na dhana iliyojengeka katika mioyo ya baadhi ya watu kuwa rais hakoselewi au hapokei maoni tofauti na yale anayoamini katika kuongoza nchi.

“Mimi huwa namshauri Rais na ananisikia; wanaosema hashauriki wanamshauri wapi?”, amebainisha Dkt. Abbas na kuwataka wananchi kuendelea kushirikiana na serikali katika kutatua changamoto zinazozijitokeza kwenye utekelezaji wa uhuru wa kujieleza na vyombo vya habari nchini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *