Elimu ya uhifadhi wa mazao kuihakikishia jamii usalama wa chakula

Jamii Africa

Imebainika kuwa sehemu kubwa ya mazao ya chakula yanayohifadhiwa katika maghala hupotea kutokana na kukosekana kwa njia bora za uhifadhi wa chakula.

Hali hiyo inatajwa kupunguza thamani ya mazao ambayo yanapelekwa sokoni na kuwakosesha wakulima mapato yaliyokusudiwa na hatari yake ni kuongeza gharama za uzalishaji.

Ripoti ya Mapitio ya Kiuchumi (June, 2017) ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) inaonyesha kuwa sehemu kubwa ya mazao  yanayohifadhiwa katika maghala ya watu binafsi na yale ya serikali hupungua thamani kwasababu ya kushambuliwa na wadudu. 

Ripoti hiyo inaeleza kuwa hadi kufikia mwishoni mwa Mei 2017, Wakala wa Taifa wa Hifadhi  ya Chakula (NFRA) ilikuwa na tani 74,826 ya hifadhi ya chakula ambapo kiasi hicho kilipungua kutoka tani 86,278 za mwezi April 2017. Na chakula kilichokuwepo ni mahindi pekee.

Kupungua kwa chakula hicho katika hifadhi ya taifa kulitokana na kuuzwa kwa tani 5,847 kwa Wilaya ambazo zilikuwa na tatizo la njaa katika baadhi ya maeneo yake. Pia tani 2,919 za mahindi ziliuzwa kwa wafanyabiashara binafsi  ili ziwafikie wananchi.

Lakini katika tani 74,826 zilizokuwepo katika hifadhi hiyo ya taifa, tani 106 zilipotea kutokana na vumbi la viwatirifu na kuharibika kwa mahindi hayo kutokana na kukaa kwa muda mrefu. Tani 106 ni sawasawa na kilo 106,000 ambazo zinaweza kukaa katika magunia 1060 ya kilo 100.

Huo ni mfano mmoja wa chakula kinachopotea katika maghala ya wakulima kwa sababu ya mbinu hafifu za utunzaji wa mazao kabla hayajauzwa na kutumika. Inaelezwa kuwa asilimia 20 mpaka 40 ya mazao hasa mahindi yanayovunwa na wakulima hupotea tangu yanapovunwa, kusafirishwa na kuhifadhiwa katika maghala  na matumizi ya kemikali ambazo huwa na madhara kwa mazao.

Kutokana na changamoto hizo za wakulima, Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo Cha Kitropiki (IITA) kupitia mradi wa Africa Rising imeendelea kutoa mafunzo kwa wakulima juu ya njia salama za kuzuia upotevu wa mazao hasa ya mahindi, jamii ya mikunde na karanga.

Pia taasisi hiyo inahamasisha matumizi ya mifuko maalumu ya kinga njaa maarufu kama “mifuko ya PICS” ambayo haihusishi matumizi ya kemikali za kuhifadhia mazao. Mkulima hutakiwa kuweka mahindi kwenye mifuko hiyo ambayo haipitishi hewa na kuruhusu wadudu waharibifu kupenya ndani ya mfuko. Njia hii ni rahisi kwa wakulima kuhifadhi mazao yao ili yasiharibiwe na wadudu au kupoteza ubora.

Maghala yanayotumika kuhifadhia chakula yanapaswa kusimamiwa vizuri ikiwemo kufanya usafi wa mara kwa mara, kuepusha maji kuingia kwenye mazao na  kupanga magunia katika mpangilio mzuri ili iwe rahisi kugundua mazao ambayo yameharibika. 

Magunia ya mazao yakiwa ghalani

 

UHIFADHI NA UPOTEVU WA MAZAO

Taasisi ya Kilimo Forum ambayo inajihusisha na ushauri kwa wakulima juu ya njia sahihi za kilimo na uhifadhi wa chakula kupitia ripoti yake ya mwaka 2014 inaeleza kwa kina dhana ya upotevu na uhifadhi wa chakula:

– Uhifadhi ni kitendo cha kuweka mazao yako sehemu maalum kwa muda maalumu kabla ya kuuzwa au kutumika.

-Upotevu wa mazao ni hali ya kupungua thamani kwa mazao kutokana na sababu mbalimbali kama vile kusinyaa, kunyauka, kuliwa na wadudu, kuibiwa au kupotea. Madhumuni ya kuhifadhi ni kwa ajili ya chakula, biashara na mbegu.

 

AINA YA UPOTEVU WA MAZAO.

Upotevu wa mazao unaweza kutokea kwa namna mbalimbali kama:

1. Kupungua Uzito

Kuna aina nyingi za visababishi na vingi ni vile vinavyokula mazao hasa wadudu na wanyama kama Panya. Aidha uvunaji usio na umakini huacha mazao mengi shambani na hivyo uhifadhi kuanza na kiasi pungufu kuliko ilivyokusudiwa.

2. Kupungua kwa Ubora

Visababishi vikuu ni wadudu wanaokula, wanaochafua, au shughuli inayovunja au kuharibu punje, kuchafua mazao kwa aina yoyote au kuoza, kusinyaa, kutoa harufu n.k

3. Upotevu wa Viini Lishe

Visababishi vikuu ni vile vinavyokula viini vya punje ambavyo ndivyo vyenye virutubisho na vitamini. Kadhalika hifadhi duni.

4. Upotevu wa mapato

Hutokana na yote yaliyotajwa hapo juu ambapo matokeo yake ni zao kupata ndogo kwenye soko na hivyo uchumi wa mkulima kuwa duni.

5. Upotevu wa nguvu ya uoto kwenye mbegu.

Visababishi ni hifadhi duni na vyote vilivyotajwa hapo juu. Katika mzunguko mzima wa uvunaji, kuna ngazi mbalimbali za upotevu ambazo ni;

– Kuvuna
– Kusafirisha
– Kukausha
– Kupukuchua/kupura
– Kupepeta/kuchambua
– Kupanga madaraja
– Kuweka dawa ya kuua wadudu
– Kuhifadhi kwenye vifaa au maghala
– Kutumia kwa chakula au kuuza
– Kusindika.

Wakulima wanashauriwa kufuata ushauri wa wataalamu wa kilimo ili kuhakikisha wanapata faida kupitia mazao wanayoyapata shambani. Pia kutumia njia sahihi za kuhifadhi chakula ambazo hazina madhara kwa mazao na binadamu.

 

 

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *