Muhogo: Zao linabebeshwa janga la njaa. Linakosa soko licha ya kuwa na utajiri

Jamii Africa

WATANZANIA wengi wameaminishwa kuwa zao la muhogo ni muhimu sana wakati wa njaa.

Wanaofanya kazi hiyo ni, kwa kiasi kikubwa ni wanasiasa na viongozi wa dini.

Hawa hujitokeza mara nyingi, hasa wakati wa njaa, wakitoa kauli nyingi, kubwa ikiwa ni – “limeni muhogo, mpate mavuno mapema mjiepushe na baa la njaa.”

Ni kutokana na kauli hizi, wananchi wengi, wakulima na wasiokuwa wakulima, wamejenga dhana kwamba muhogo ni zao linalipaswa kulimwa, kutunzwa na hata kutumiwa, wakati wa majanga, hasa njaa.

Mihogo ikiwa imepangwa sokoni.

Shamba la mihogo lililostawi.

Lakini ukweli ni kwamba muhogo, kamwe sio zao la kutibu majanga ya njaa, bali linabebeswa hali hiyo kutokana na mazoea tu yaliyokuwepo miaka mingi.

Muhogo unatengwa?

Kimsingi, hakuna tofauti kubwa ya vyakula vinavyotokana na mazao ya mahindi, mtama, muhogo na uwele, ni mazoea tu ya matumizi ya mazao hayo kutoka eneo moja hai jingine.

Yawezekana kabisa kuwa kwa msimamo huo, wakulima wengi wa kilimo cha muhogo ni watu wa kipato cha chini licha ya kutumiwa na watu wa madaraja yote kama chakula.

Muhogo unakolimwa

Zao la muhogo hulimwa maeneo mbalimbali hapa nchini, ambapo asilimia 75 hulimwa kwa ajili ya matumizi ya chakula na asilimia 25 kwa ajili ya  matumizi mengine.

Muhogo unaweza kuutafuna ukiwa mbichi, kupika majani yake kama mboga – almaarufu; kisamvu, kuichemsha, kukaanga na hata kuusindika na kusagwa kwa ajili ya kupata unga.

Mihogo iliyokaangwa, maarufu kama 'chips dume' ikiwa imejazwa kachumbari.

Kwa Mkoa wa Mtwara, zaidi ya asilimia 80 ya wakulima wanaojishughulisha na kilimo, kila mmoja lazima anakuwa na miti kadhaa ya mihogo kwaajili ya chakula cha nyumbani.

Kutokana na changamoto hizo, shirika lisilokuwa la kiserikali la Mennonite Economic Development Associate (Meda), linaloshughulikia kuondoa umaskini  kwa kutumia njia za kibiashara, limeamua kutekeleza mradi wa majaribio wa kurasimisha mfumo wa kupatikana mbegu bora za muhogo kwa kutumia njia za kibiashara ili kuwainua wakulima.

Futari ya mihogo.

Licha ya jitihada ya shirika hilo kuwawezesha wakulima hapa nchini kuzalisha mbegu za kisasa na kuzisambaza kwa wakulima wadogowadogo vijijini, bado kasi ya wakulima kuitikia  kulima zao hilo ni ndogo ikilinganishwa na kilimo cha mazao mengine ya chakula na biashara.

Hali hiyo inatokana na mamlaka mbalimbali za serikali zikiwemo halmashauri za miji na wilaya na wizara ya kilimo, uwangiliaji na ushirika,  kutokuwa na mikakati na jitihada za kuwatafutia soko wakulima hao.

Wakulima walonga

Mkulima mzalishaji wa mbegu za muhogo aina ya ‘Kiroba’ wa kijiji cha Ndomoni, Wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi, Raymond Erasto ambaye amewezeshwa na Meda, ameiambia FikraPevu kuwa kwa sasa wakulima wachache wanaojishughulisha na kilimo cha muhogo wanalima kwa ajili ya matumizi ya chakula pekee.

Anasema hali ambayo inawafanya wakulima kutojitokeza kwa wingi kujishughulisha na kilimo hicho, kwani hulima “vijishamba vidogo” ambavyo haviwezi kuwapatia tija.

FikraPevu imemtembelea mzalishaji  huyo wa mbegu mwenye hekari tano; ambapo hekari moja ina uwezo wa kupandwa miti 4,000, amekiri kuwa kwa muda wa miaka mitatu aliyojishughulisha na uzalishaji wa mbegu za muhogo, kasi ya wakulima kuchangamkia mbegu hizi ni ndogo mno.

“Changamoto kubwa ni kwa wale wateja ambao ni wanajamii, awali walitarajia kupata miti ya muhogo bila malipo, lakini angalau kwa sasa wamepata uelewa kuwa miti inauzwa Sh. 200, ingawa bado kasi ni ndogo kwani zamani walikuwa na tabia ya kuombana mbegu,” anasema Raymond

Mzalishaji wa mbegu za muhogo wa Kijiji  cha Lengo wilayani Newala, mkoani Mtwara, Hamisi Kasembe ameiambia FikraPevu kuwa kwa muda wa miaka mitatu aliyokuwa mzalishaji wa mbegu za muhogo amekabiliwa na  changamoto ya soko la zao hilo, licha ya kufanya jitihada mbalimbali kushawishi wakulima kutumia mbegu bora zenye zinazokabiliana na magonjwa.

Anasema mbegu ya muhogo kwa kipande kimoja cha mti anauza kati ya Sh. 200 hadi Sh. 300, lakini bado wakulima wengi wanaojishughulisha na zao hilo kwaajili ya chakula, wana utamaduni wa kuomba mbegu na sio kununua.

“Nilipatiwa mafunzo na Meda pia nikakutana na wataalamu wa mbegu na walinieleza mbegu bora na njia bora za kutumia, lakini licha ya kulima kilimo bora, bado hatuna wateja wa kuwauzia mbegu. Mwitikio ni mdogo kwasababu mtu anataka mbegu ya bure,” anasema Kasembe

Anasema kuwa licha ya kikundi chao hapo kijijini kuwa na mashine ya kusindika muhogo, bado soko la unga huo ni dogo, hali inayofanya kutojishughulisha na usindikaji, badala yake kutegemea wanunuzi wachache wanaojishughulisha na biashara ya kukaanga muhogo.

Geophrey Chilumba, mkulima kutoka Kata ya Chikukwe, Wilaya ya Masasi, anasema zao la muhogo linaweza kubadili maisha ya wakulima, endapo watafuata kanuni bora za kilimo kutoka kwa wataalamu.

“Naiomba serikali itujali wazalishaji wa mbegu, mfano pale halmashauri inapohitaji mbegu kuzitawanya, ituone sisi, hii itatupa moyo, kama hivi sasa nazalisha mbegu zenye ukinzani na magonjwa, lakini hakuna wateja,” Chilumba anaiambia FikraPevu.

Asha Namungulile, mkulima kutoka Kijiji cha Lengo, Kata ya Mchemo, Tarafa ya Kitangali, wilayani Newala, anasema miaka kadhaa iliyopita walikuwa wakijihusisha na kilimo cha kienyeji pasipo mafanikio, lakini kwa sasa wamepata mbegu bora, ingawa bado wanakabiliwa na changamoto ya soko.

Uzalishaji wa Muhogo

Mkuu wa Idara ya Utafiti wa Mazao ya Jamii ya Mizizi wa Kituo cha Utafiti cha Naliendele, Dkt. Geofrey Mkamilo anaiambia FikraPevu kuwa Tanzania inazalisha tani milioni tano kila mwaka, ambapo kati ya hizo, Kanda ya Ziwa yenye mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Mwanza, Kagera, Mara na Geita, ndio inayoongoza kwa kuzalisha asilimia 37 ya zao hilo.

Mihogo ya kuchoma.

Ukanda unaofuata kwa uzalishaji wa muhogo ni Kanda ya Kusini inayojumuisha mikoa ya Mtwara na Lindi, huzalisha asilimia 25 ya mihogo yote hapa nchini.

Mtafiti huyo alibainisha kuwa Kanda ya Mashariki yenye mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Tanga na Morogoro, inazalisha asilimia 12 ikifuatiwa na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yenye mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi na Ruvuma, ambayo uzalisha asilimia 10, Kanda ya Magharibi yenye mikoa ya Tabora na Kigoma, inazalisha asilimia 6.

Kanda za Kati zenye mikoa ya Dodoma na Singida na Kanda ya Zanzibar inayojumuisha mikoa iliyopo visiwa vya Unguja na Pemba, huzalisha asilimia 3 na ukanda wa mwisho ni Kanda ya Kaskazini yenye mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara, ambayo uzalisha asilimia moja ya muhogo wote unaozalishwa hapa nchini.

Dkt. Mkamilo anasema ukitaka kilimo bora ni lazima uanze kwa kuainisha mbegu bora zenye ukinzani wa magonjwa na zinazozaa sana kwa kuwatafuta wataalamu wa kilimo.

“Changamoto iliyopo kwa baadhi ya wakulima ukiwaambia wanunue mbegu hawataki, kwasababu walishazoea kupeana mbegu, jambo ambalo linasababisha hata mihogo kushambuliwa na magonjwa ya batobato na michirizi ya kahawia, kwasababu mbegu wanayotumia haijathibitishwa na mtaalamu,” Dkt Mkamilo anaiambia FikraPevu.

Anasema yapo mafanikio ya kusambaza mbegu kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali ikwemo Meda, ambapo anasema zaidi ya pingili milioni nne zimesambazwa kwa wakulima nchini.

“Zao la muhogo ni zao linalolimwa maeneo mengi, kwa kutumia maabara tumeweza kuanisha aina ya virusi tunavyoweza kupambana navyo ili kushauri wakulima na wadau wengineo kujua aina ya mbegu zinazoendana na mazingira na kubaini ni virusi aina gani,” anasema Dkt. Mkamilo

Nachingwea wajitosa

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Nachingwea, Mhandisi Jackson Masaka ameiambia FikraPevu kuwa halmashauri yake mwaka huu wa fedha wametumia kiasi cha Sh. 31 milioni kwa ajili ya kununulia mbegu za muhogo na ufuta na kuzisambaza kwenye vikundi vidogovidogo vya wakulima.

Bidhaa mbalimbali zilitokanazo na zao la muhogo.

Mkuu wa idara ya ya kilimo, ushirika na umwagiliaji wa halmashauri ya Nachingwea, Raphael Ajetu amekiri kuwemo kwa tatizo la soko la muhogo na katika kukabiliana na hilo idara yake imeendelea kuhamasisha wakulima kulima zao la muhogo.

Ili kukabili changamoto hizo, anasema kila kata katika halmashauri hiyo, inatakiwa na kuwa hekari kumi na kila mkulima lazima alime hekari moja ya muhogo, kwani kuna kiwanda kinatarajiwa kujengwa mkoani Lindi kwa ajili ya kutengeneza wanga, hivyo itasidia kutatua tatizo la soko.

Meda wazungumza

Meneja Miradi wa Meda, Stephen Magige anasema mradi huo wa muhogo ulianza utekelezaji wake mwaka 2012 katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Dodoma.

Magige ameiambia FikraPevu kwamba baada ya kuonesha mfumo wa kilimo cha muhogo kibiashara unafanya vizuri katika mikoa hiyo, mfadhili wa mradi Bill and Belinda Gates Foundation aliruhusu majaribio yafanyike katika kanda ya ziwa na pwani kuanzia mwaka 2012, ambapo mpaka sasa mradi unafanya kazi na wakulima wajasiliamali 156 katika ngazi mbalimbali za mfumo wa mbegu bora.

Anasema wakulima wamekuwa wakipata mbegu za muhogo kutoka kwa wakulima wenzao bure, hali ambayo ni rahisi mno kusambaa kwa magonjwa ya batobato na michirizi ya kahawia.

Magige anasema batobato na michirizi ya kahawia ni magonjwa yanayoweza kupunguza uzalishaji kwa asilimia 80-100, hivyo mradi wao unajaribu njia ya kibiashara itakayoonesha ni jinsi gani mkulima atapata mbegu bora za muhogo kwa njia endelevu.

FikraPevu inachokijua

Licha ya kuonekana muhogo ni zao lenye taswira ya umasikini, hivi sasa ni mwanga wa utajiri.

Wawekezaji kutoka China na India, wamekuwa wakipishana nchini kuomba kuanzisha viwanda vya kusindika muhogo kwa ajili ya unga; unaotumiwa kuwa chakula, kutengeneza gundi, chaki na matumizi mengine.

Wawekezaji hao, wanajipanga kuanza kusafirisha mazao ya muhogo, hivyo kujihakikishia utajiri mkubwa, ingawa hapa nchini muhogo, unaonekana kubezwa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *