Gari la zimamoto lakwamisha Bombardier kutua Mpanda

Jamii Africa

UKOSEFU wa gari la zimamoto umekwamisha kuanzishwa kwa safari za ndege za Bombardier za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) mjini Mpanda katika Mkoa wa Katavi kama ilivyopangwa hapo awali.

FikraPevu inafahamu kwamba, Serikali kupitia kwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa ATC, Kapteni Richard Shaidi, iliahidi kwamba safari ya ndege hizo kutoka Dar es Salaam hadi Mpanda ingeanza mapema tangu ndege hizo zilipozinduliwa na Rais Dkt. John Magufuli.

Ndege aina ya Bombardier iliyonunuliwa na ATCL

Hata hivyo, mpaka sasa safari hizo za Dar es Salaam – Mpanda, hata ile ya Tabora – Mpanda kwa ndege hizo kubwa bado haijaanza na sababu kubwa inayotajwa ni ukosefu wa gari la zimamoto.

Akiwa katika ziara ya kikazi hivi karibuni, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchunguzi na Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani, alimuagiza Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Mpanda kuwasiliana na Kampuni ya Uendelezaji Uwanja wa Ndege wa  Kilimanjaro (KADCO) kupata gari la zimamoto ili ndege za Bombardier ziweze kuanzisha safari zake mkoani humo.

Mhandisi Ngonyani alisema kwa muda sasa uwanja huo umekuwa ukitumiwa na ndege chache za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), hivyo ni wakati sasa kutumika na ndege za ATCL ili kuboresha huduma za usafiri wa anga mkoani humo.

“Kamilisheni mazungumzo na KADCO ili kupata gari la zimamoto lenye ujazo wa lita 4,000 za mafuta litakalokuwa na uwezo wa kukabiliana na majanga ya moto endapo yatatokea, kutakapokuwa na gari hilo uwanjani hapa tutaanzisha safari za ndege za Shirika letu,” alisema naibu waziri huyo.

Aidha, alimtaka meneja wa uwanja huo kuhakikisha anauingiza katika mpango maalum kwa ajili ya ujenzi wa taa ili uweze kutumika kwa mchana na usiku.

Eng. Ngonyani aliongeza kuwa azma ya Serikali ni kuhakikisha usafiri wa anga nchini unaimarika kwa kutumia ATCL na mashirika mengine yalipo nchini na kwamba wamejipanga kuendelea kuboresha miundombinu ya viwanja ili viwe katika viwango vinavyokubalika.

FikraPevu imeelezwa kwamba, Meneja wa Uwanja huo, Seneth Lyatuu, alimhakikishia naibu waziri kuwa changamoto ya kuwa na gari la zimamoto itatatuliwa mapema ili wakazi wa Mpanda waweze kunufaika na huduma za ATCL na hivyo kuwapa unafuu watumiaji wa  usafiri wa anga.

“Kuanza kwa safari za ATCL hapa Mpanda kutawapunguzia gharama wananchi ambao kwa sasa hulazimika kwenda Mwanza au Mbeya ili kupata ndege ya kwenda Dar es Salaam na gharama huwa kubwa,” alisisitiza Lyatuu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Saleh Mhando, alisema kuanza kutua kwa ndege kubwa za Bombardier kutaleta tija na kutafungua fursa ya utalii wa ndani na nje ya nchi hasa katika Hifadhi ya Katavi ambayo ina vivutio vingi.

Ndege za ATCL

FikraPevu inafahamu kwamba, Serikali ya wamu ya tano ilinunua ndege tatu zinazotumia injini ya pangaboi kutoka kampuni ya Bombardier Aerospace ya Canada, ambapo mbili kati ya hizo ni Dash 8 Q400 zenye uwezo wa kubeba 76 na moja Dash 8 Q200 aina ya  CRJ-200 ER yenye uwezo wa kubeba abiria 50.

Ndege hizo, ambazo zilizinduliwa na Rais Magufuli, zilianza kufanya safari zake nchini tangu Oktoba 15, 2016, ambapo mpango wa awali ulionyesha kwamba hata safari za Dar es Salaam kwenda Mpanda na Tabora-Mpanda zilikuwa zimehusishwa.

Taarifa ambazo FikraPevu inazo zinaeleza kwamba, sifa za ndege hizo zinaztumia mafuta kidogo ni kuwa na Urefu: (Length) mita 32.6, Kimo: (Height) futi 6.40, Upana: (Width) futi 8, Nguvu/Injini: (HorsePower) 10,142 HP, Kasi: (AirSpeed) 666.7 Km/h na Umbali inayoenda: (Max.Range) km 2,522.4.

Pia kwa Umbali Kuruka Juu: (Cruising Altitude) futi 27,000, Uzito Wa Kubeba: (Max Payload) tani 8.7, Full Tank: (Fuel Capacity) lita 6,617, muda inayotumia kufika umbali wa juu: (Time to Cruising Altitude) dakika 18.

Na kwa upande mwingine, zina urefu njia ya kurukia: mita 1067, urefu njia ya kutua: mita 1286, ulaji mafuta: (Fuel Economy/Km) 16,940/-Tzs kila 1.8 km lakini pia bei kwa ndege moja: (Price range) ni bilioni 66.

FikraPevu inafahamu kwamba, serikali ina mpango wa kununua ndege kubwa ya Boeing 787-8 Dreamliner kutoka kampuni ya Boeing ya Marekani, ndege ambayo ina uwezo wa kuchukua abiria 262 ambayo inatarajiwa kuwasili nchini humo Juni 2018.

Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli akitazama kitabu cha picha ya ndege aina ya Boeing 787-8 Dreamliner wakati alipokuwa akisikiliza maelezo yake kutoka kwa Mkurugenzi wa mauzo wa kampuni ya Ndege ya Boeing Jim Deboo Ikulu jijini Dar es salaam. Picha/IKULU, TANZANIA.

Ndege nyingine ambazo Tanzania itazinunua ni ndege moja aina Bombardier Q400 Dash 8 NextGen iliyotarajiwa kuwasili mwezi Juni 2017, ndege mbili aina ya Bombardier CS300 zenye uwezo wa kuchukua kati ya abiria 137 na 150 na zinazotarajiwa kuwasili nchini kati ya Mei na Juni, 2018.

Tayari malipo ya awali kwa ununuzi wa ndege hizo yameshafanyika.

Safari za ATCL

Tangu kupatikana kwa ndege hizo, ATCL ambayo ilikuwa haina ndege za abiria kwa muda mrefu, imeanzisha safari katika miji mbalimbali nchini Tanzania pamoja na nchi jirani na kufufua matumaini ya uhai wa shirika hilo ambalo kwa muda mrefu limekuwa likielemewa na madeni huku likiwa na mzigo mkubwa wa matumizi.

Taarifa ambazo FikraPevu inazo zinaeleza kwamba, ndege hizo za Air Tanzania hivi sasa zinafanya safari nne kwa wiki kwenda Mbeya katika siku za Jumatatu, Jumatano, Ijumaa na Jumapili kwa mwendo wa saa moja tu kutoka Dar es Salaam kwa gharama ya Shs. 150,000 kwa safari ya kwenda na Shs. 260,000 kwa tiketi ya kwenda na kurudi.

Aidha, ndege hizo zinafanya safari nne pia kwa wiki kati ya Dar es Salaam na Mwanza na zinafanya safari nne kati ya Dar es Salaam na Moroni katika Visiwa vya Comoro kila Jumatatu, Jumatano, Ijumaa na Jumamosi.

Miji mingine ya ndani ambayo ndege hizo zinafanya safari ni Mtwara, Tabora, Kigoma, Bukoka, Dodoma, Arusha, Moshi na Zanzibar, lakini pia zinakwenda Bujumbura nchini Burundi, Entebe nchini Uganda na Nairobi nchini Kenya.

Hivi sasa kuna safari mbili kila wiki za ndege kutoka Dar es Salaam kupitia Dodoma hadi Kigoma.

Nauli ya njia moja kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza ni Shs. 160,000 na kwa tiketi ya kwenda na kurudi ni 320,000, wakati ambapo nauli ya kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma ni Shs. 395,000 kwa njia moja na ka tiketi ya kwenda na kurudi ni Shs. 610,000.

Aidha, viwango vya nauli kutoka Dar es Salaam hadi Arusha ni Shs. 180,000 na kwenda na kurudi Shs. 360,000; kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ni Shs. 165,000 na kwenda na kurudi ni Shs. 299,000; kutoka Arusha hadi Zanzibar ni Shs. 249,000 na kutoka Zanzibar hadi Dar es Salaam ni Shs. 123,000.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *