Gesi yamfanya aokoe Sh. 1.5 milioni za mkaa kwa mwaka

Jamii Africa

“KWA mwezi mmoja nilikuwa natumia Sh. 140,000 kwa ajili ya kununulia magunia mawili ya mkaa ambayo yanatosha kwa matumizi ya nyumbani, lakini sasa ninaokoa Sh. 365,000 kwa miezi mitatu, ambayo ni takriban Sh. 1.5 milioni kwa mwaka, kwa kutumia gesi” ndivyo anavyoanza kueleza Amina Fidelis (37).

Amina ni mfanyabiashara ndogo ndogo wa Mbagala jijini Dar es Salaam na mama wa watoto wanne.

Mwanamke huyo alianza kutumia gesi kwa matumizi ya nyumbani tangu mwaka 2013, ameieleza FikraPevu kwamba, mtungi wa gesi wa kilo 15 unaouzwa Sh. 55,000 na hutumia kwa miezi mitatu.

“Kama ningetumia mkaa ina maana kwa miezi mitatu ningetumia Shs. 420,000, lakini sasa gesi imekuwa nafuu zaidi kwangu na inarahisisha mapishi, sina kazi tena ya kuhangaika ama kumhangaisha mtoto kuwasha jiko la mkaa kama zamani na ninaweza kupika wakati wowote ninapojisikia na kwa haraka,” anasema.

Mama huyo ameiambia FikraPevu kwamba anaamini hata madhara aliyokuwa akiyapata kutokana na moto na vumbi la mkaa yamepungua tangu alipoanza kutumia gesi, kwani kila wakati alikuwa akikohoa na kubanwa na kifua.

“Daktari aliniambia moto wa mkaa ulikuwa unaniathiri, sikuwa na njia nyingine, lakini nikaamua kucheza mchezo wa kupeana, nilipopokea zamu yangu nikaenda kununua mtungi wa gesi pamoja na jiko lake kwa gharama ya Shs. 210,000,” anabainisha.

Gharama nafuu

Amina ni miongoni mwa wananchi wengi jijini Dar es Salaam na sehemu mbalimbali nchini ambao wameanza kutumia nishati ya gesi badala ya mkaa, ambao upatikanaji wake unalalamikiwa kusababisha uharibifu wa mazingira kutokana na ukataji wa miti.

Khalid Ramadhan (32), mfanyabiashara ya mgahawa katika eneo la Mbagala Rangi Tatu jijini Dar es Salaam, ameiambia FikraPevu kwamba, sasa anaona faida ya biashara yake tangu alipoanza kutumia gesi mwaka 2015 kwani mapato yake yalikuwa yakiishia katika ununuzi wa mkaa.

“Ingawa nilikuwa napata faida, lakini si kama ninayoipata sasa. Kwa mwezi mzima nilikuwa natumia Shs. 700,000 kununua magunia 10 ya mkaa kwa ajili ya kukaanga viazi (chips), leo hii nanunua gesi kwa Sh. 200,000 tu kunitosha mwezi mzima kwa shughuli zangu zote,” anasema.

Hata hivyo, anasema kwamba bado anatumia mkaa katika mapishi mengine, hasa wali, lakini si makubwa na anayamudu.

FikraPevu inatambua kwamba, kubadili matumizi ya nishati kutoka kwenye kuni na mkaa kwenda kwenye gesi, ambayo inaagizwa kutoka nje, kunaweza kusaidia kupambana na mabadiliko ya tabia nchi na kudhibiti ukataji ovyo wa miti kwa ajili ya kuchoma mkaa.

Taarifa kutoka Mfumo wa Kitaifa wa Mkakati wa Kupunguza Uzalishaji wa Hewa ya Ukaa Kutokana na Ukataji Miti na Uharibifu wa Misitu (Mkuhumi) zinasema, Tanzania inapoteza takriban ekari 412,000 za misitu kila mwaka kati ya hekta milioni 35 za misitu zilizopo nchini kutokana na ukataji miti ovyo, uharibifu wa mazingira unaoendana na uchomaji moto wa misitu.

Hali hiyo inasababisha upotevu wa Shs. 6.8 bilioni kila mwaka kwa matumizi yasiyo sahihi ya misitu, ambapo inaelezwa kwamba kwa sasa ni asilimia 55 tu ya ardhi nchini iliyofunikwa na misitu huku maeneo mengi kama Dodoma, Singida, Shinyanga na Mwanza yakiwa nusu jangwa.

Tunachokijua

FikraPevu inafahamu kwamba, karibu asilimia 70 ya wakazi wa Dar es Salaam wanatumia nishati ya mkaa na kuni, ambazo kwa kiasi kikubwa zinavunwa katika Mkoa wa Pwani, hususan wilaya za Kisarawe, Mkuranga na Bagamoyo.

Jiji la Dar es Salaam linakadiriwa kutumia magunia kati ya 50,000 na 60,000 ya mkaa kwa siku ambazo ni sawa na gunia kati ya milioni 15.3 na milioni 2.1 kwa mwaka, kiwango kinachochangia kasi kubwa iliyopo sasa ya kutoweka kwa misitu nchini.

Malori yakiwa yamebeba magunia ya mkaa kusafirisha kwenda mijini.

Lakini idadi ya watumiaji wa gesi majumbani katika Jiji la Dar es Salaam inaongezeka kwa kasi, ingawa bei yake imekuwa ikibadilika kila wakati.

Uchunguzi wa FikraPevu unaonyesha kwamba, kwa sasa mtungi mdogo kabisa gesi wa aina mbalimbali, unauzwa kwa wastani wa kati ya Shs. 22,000, mtungi wa kilo 15 kwa kati ya Shs. 50,000 hadi Shs. 55,000 na mtungi wa kilo 38 Shs. 95,000 hadi Shs. 110,000.

“Gesi ni nafuu sana kuliko mkaa. Mtungi wa kilo 15 ninaoutumia kwa familia yangu unakaa kwa wiki 10 hadi 13 – wastani wa miezi mitatu – wakati katika kipindi hicho ningeweza kununua magunia sita ya mkaa,” anafafanua Amina.

Amina anawatoa hofu wanawake wenziwe, hasa wa kipato cha chini kama yeye, kwamba wanaweza kununua mitungi ya gesi na kubadilisha matumizi ya nishati, ikiwa tu watadhamiria.

“Ndiyo, huwezi kupata fedha kwa wakati mmoja, lakini sisi wanawake tunashiriki kwenye ‘michezo ya kupeana’ na vicoba, ni kama tunaweka kwenye ‘kibubu’, kama ukipangilia vizuri, unapopokea fedha hizo unaweza kuzifanyia jambo la maana… ndivyo nilivyofanya mimi wakati nanunua mtungi kwa mara ya kwanza,” anasema.

Hata hivyo, katika kipindi hiki ambacho serikali iko katika harakati za kuhakikisha gesi asilia inawanufaisha Watanzania, mojawapo ya maeneo yanayolengwa ni matumizi ya majumbani.

Ukiachilia mbali mradi wa kuwasambazia majumbani baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam, lakini gesi hiyo itasindikwa kwenye mitungi kwa ajili ya matumizi hayo kama ilivyo sasa.

Mbali ya kupunguza athari za mazingira, lakini ujio wa gesi asilia unaweza kupunguza hata bei ya nishati hiyo tofauti na ilivyo juu kwa sasa kutokana na kuiagiza nje.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *