Zijue kampuni zilizowekeza katika mafuta na gesi Tanzania – AFREN

Jamii Africa

HATUWEZI kuzungumzia maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi nchini Tanzania bila kwanza kuzifahamu kampuni zilizowekeza humo. Hawa ndio wadau muhimu Zaidi kwa sababu, kama tulivyoona, hata ugunduzi wa awali usingeweza kufanyika na kufanikiwa bila wao kwa sababu kama inavyoeleweka, Tanzania haikuwa na bado haijapata wataalamu na mitaji ya kutosha kuwekeza katika tafiti, uchimbaji na uchakataji wa gesi.

Tangu mwaka 1952 utafiti ulipoanza kufanyika, kumekuwepo na kampuni nyingi za kigeni ambazo zilipewa mikataba ya kufanya tafiti na sasa nyingine tayari zimekwishapewa mikataba ya uchimbaji pamoja na kutengeneza miundombinu inayotakiwa katika sekta hiyo, hasa gesi ambayo tayari inaendelea kuzalishwa.

Tumeona katika makala iliyotangulia kwamba harakati za utafiti wa mafuta na gesi nchini Tanzania zimehusisha kampuni mbalimbali na takwimu zilizopo zinaonyesha kwamba kuna kampuni nyingi zilizowekeza nchini.

Baadhi ya kampuni hizo zinazojihusisha na utafiti wa mafuta na gesi ni Afren, Aminex, Beach Energy, BG Group, Bounty Oil and Gas, Dodsal Resources, Heritage Oil, Jacka Resources, Maurel et Prom, Motherland Homes, Total, Statoil, Signet Petroleum, Shell, Petrodel Resources, Orca, Petrobas, Nor Energy, Ophir Energy, na Swala Energy.

FikraPevu inachambua taarifa mbalimbali za kampuni hizo kupitia kwenye mitandao, tovuti za kampuni husika pamoja na zile zilizotolewa na serikali kupitia idara mbalimbali likiwemo Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Leo tunaanza kuitazama kampuni ya Afren Ernergy:

Afren Energy Resources Limited (Uingereza)

• Aina: Kampuni ya Umma

• Imeandikishwa: Soko la Kuu la Hisa la London (LSE), Uingereza kama kampuni ya Afrika

• Mtendaji Mkuu: Alan Linn

• Kuanzishwa: 2004

• Makao Makuu: London (Uingereza)

• Waasisi: Osman Shahenshah, Egbert Imomoh, Constantine Ogunbiyi, Ethelbert Cooper

• Watendaji wengine: Simon Appell, Daniel Imison na Catherine Williamson ambayo waliteuliwa Julai 31, 2015

• Bidhaa: Utafiti wa Mafuta na Gesi

• Mapato: Dola za Marekani 1.644 bilioni (2013)

• Mapato baada ya kodi: Dola 474.8 milioni (2013)

• Mapato ya Uendeshaji: Dola 491 milioni (2013)

• Waajiriwa: 485

• Tovuti: www.afren.com

• Simu: +44(0) 161 838 4536

• Barua-pepe: [email protected].

Kampuni hii inatoka Uingereza na inajishughulisha na uchimbaji wa mafuta na gesi barani Afrika na imewekeza katika nchi 11, ambazo ni Nigeria, Ghana, Cote d’Ivoire, Sao Tome & Principe na Ukanda wa Pamoja wa Uendelezaji (Joint Development Zone – JDZ), Congo Brazaville, Afrika Kusini, Ethiopia, Kenya, Madagascar, Shelisheli na Tanzania ikijikita katika uzalishaji, tathmini ya miradi ya maendeleo, na utafutaji wa rasilimali asilia.

Kwa bahati mbaya Afren haiungi mkono jitihada za Mkakati wa Uwazi katika Shughuli za Uchimbaji Rasilimali (EITI), ambao unahimiza kuwepo kwa uwazi katika shughuli zote za uchimbaji ikiwa ni pamoja na kuweka wazi mikataba pamoja na mapato.

Uwekezaji nchini Tanzania

Taarifa zilizopo zinaonyesha kwamba, Afren iliingia katika uwekezaji kwenye sekta ya gesi na mafuta Tanzania mwaka 2011 baada ya kununua asilimia 74 ya hisa katika Kitalu cha Tanga ambacho kilikuwa kinamilikiwa kwa asilimia 100 na kampuni ya Petrodel, ambayo kwa sasa inamiliki asilimia 26. Petrodel ilipata kitalu hicho katika zabuni ya mwaka 2005/2006.

Taarifa za tovuti ya kampuni hiyo zinaonyesha kwamba, Kitalu cha Tanga kinaungana na kitalu namba L 17 na L 18 vilivyoko nchini Kenya ambavyo vinamilikiwa kwa asilimia 100 na kuendeshwa na Afren.

afren-oil

Taarifa za Kitengo cha Afren cha Uthamini wa Athari za Kimazingira (EIA), zinaeleza kwamba, upimaji na tathmini ya uchimbaji umekamilika kwa maeneo yote mawili ya kisima cha Chungwa-1 na kisima cha Mkonge-1 (kisima kingine kilichoko kwenye kitalu hicho) ambavyo viko tayari kwa uchimbaji.

Kwingineko

Nchini Congo Brazzaville, kampuni hiyo inajihusisha na eneo la La Noumbi inakomiliki asilimia 14 ikishirikiana na kampuni ya Maurel et Prom ya Ufaransa ambayo ndiyo mwendeshaji mkuu.

Nchini Côte d'Ivoire wamewekeza katika maeneo mawili. Kwenye kitalu cha CI-523 wanamiliki hisa asilimia 20 na kampuni ya Taleveras ina asilimia 70 na Petroci asilimia 10, wakati kwenye kitalu cha CI-525 chenye visima vya Eland na Kudu inamiliki asilimia 61.875, Taleveras asilimia 28.125 na Petroci asilimia 10.

Nchini Ethiopia imewekeza katika kitalu namba 8 ambako ina asilimia 30 wakati zilizobakia zinamilikiwa na kampuni ya New Age ambayo ndiyo mwendeshaji mkuu.

Huko Ghana imewekeza katika Kitalu cha Keta ambako ina asilimia 35 na zilizobakia zinamilikiwa na kampuni ya Eni na eneo hilo liko katika hatua ya tathmini ya kiuchumi.

Kwenye vitalu vya L17 na L18 nchini Kenya kampuni tanzu ya Afren ya EAX inamiliki asilimia 100 wakati kampuni hiyo inamiliki asilimia 80 katika kitalu namba 1.

Huko Iraq katika eneo la Kurdistan ina hisa asilimia 60 katika eneo la barda Rash na asilimia 20 kwenye eneo la Aini Sifni.

Nchini Madagascar, Afren inamiliki hisa asilimia 90 katika Kitalu namba 1101 ambacho kinaendeshwa na kampuni yake tanzu ya EAX. Kitalu hicho kiko mashariki mwa Bonde la Ambilobe, kaskazini mwa kisiwa hicho. Eneo hilo lina ukubwa wa kiometa za mraba 14,900 katikati ya bahari.

Huko Nigeria, mnamo Desemba 2014 Afren plc ilikuwa miongoni mwa kampuni 100 ambazo zilipongezwa na Rais (mstaafu) Goodluck Ebele Jonathan ikishika nafasi ya 86 wakati washirika wao AMNI na Oriental Energy zilishika nafasi ya 58 na 20 mtawalia.

Kisiwani Shelisheli, Afren inamiliki asilimia 75 ya hisa katika vitalu A na B ambavyo vinaendeshwa na kampuni yake tanzu ya EAX. Eneo hilo liko kwenye kina kirefu cha maji kaskazini mwa kisiwa hicho vikiwa na kilometa za mraba 14,319.

Nchini Afrika Kusini Afren ina asilimia 25 katika kitalu namba 2B ambacho kinaendeshwa na washirika wao kampuni ya Thombo na hisa zinaweza kuongezeka hadi asilimia 50 ikiwa zitahamishiwa kwa Afren ikiwa zoezi lake la kuchimba kisima kimoja litakamilika.

Changamoto zilizoipata

Mwaka 2015, Afren ilikuwa kampuni ya kwanza kukumbwa na tatizo la kuporomoka kwa bei ya mafuta duniani baada ya kampuni hiyo iliyoorodheshwa kwenye AIM kubadilisha utawala.

Uamuzi wa bodi ya wakurugenzi wa kampuni hiyo ulifuatia miezi kadhaa ya kutetereka kwa kampuni katika kulipa madeni ambapo bodi hiyo ilikuwa inahitaji nyongeza ya Dola za Marekani 200 milioni ili iweze kusimama.

Mapema mwaka 2015 kampuni hiyo ilibainisha upotevu wa mapato kabla ya kukatwa kodi wa kiasi cha Dola za Marekani 1.95 bilioni kutokana na gharama za kufidia Dola 900 milioni zilizopotea kufuatia kushuka kwa bei ya mafuta na kusitishwa kwa akiba yake ya mafuta huko Barda Rash katika eneo la Kurdistan nchini Iraq ambapo mapato yalishuka hadi Dola 946 milioni kulinganisha na Dola 1.64 bilioni za mwaka 2014.

Kwa hiyo bodi ikawateua Alix Partners kufanya kazi za utawala ili kuhakikisha wanaendelea na shughuli zao kama kawaida na katika taarifa yake, Afren ilisema: “Bodi inaamini kwamba taratibu zote zimefuatwa na kuzingatiwa katika suala hili.”

Mnamo Ijumaa, Januari 2, 2015 Mtendaji Mkuu wa zamani wa kampuni hiyo Osman Shahenshah na ofisa uendeshaji mkuu Shahid Ullah walikubali kulipa Dola 20 milioni kwenye kampuni hiyo baada ya kutishiwa kufikishwa mahakamani kutokana na kashfa ya ufisadi.

Afren ilikiri kupokea Dola 17 milioni pamoja na Dola 3 milioni nyingine za gharama za uchunguzi.

Shahenshah, ambaye ni mmoja wa waasisi wa kampuni hiyo, alidaiwa kufanya malipo makubwa bila ridhaa na gazeti la The Guardian la Uingereza liliripoti kwamba kashfa hiyo ilisababisha mapato ya kampuni hiyo kushuka kwa asilimia 30 hadi kufikia Paundi 565 baada ya kuporomoka kwa bei ya hisa za uzalishaji katika maeneo muhimu ya nchini Nigeria.

Shahenshah na Ullah wanadaiwa katika kashfa hiyo kwamba waliidhinisha malipo ya Paundi 640,000 kwa ajili ya gharama za usafiri wa ndege na kwamba kulikuwa na ufisadi mwingine walioufanya wa kupokea malipo kutoka kwa washirika wao wa mafuta nchini Nigeria, malipo ambayo kama yangetolewa kihalali kwa wakurugenzi wote yangeweza kuiingizia kampuni hadi Dola 200 milioni. Inaelezwa kwamba wawili hao walipokea isivyo halali Dola 17.1 milioni kutoka kwa washirika wao wa mafuta Nigeria, kampuni ya Oriental Energy Resources na wakakiri kupokea fedha hizo.

Katika ripoti ya kampuni hiyo, Shahenshah alikuwa ametumia kiasi cha Paundi 288,000 kwa matumizi binafsi ya ndege ya shirika kati yam waka 2013 na 2014 na katika kipindi hicho hicho Ullah naye alikuwa ametumia gharama za usafiri zinazofikia Paundi 349,000.

Hata hivyo, tangu walipomtimua Shahenshah kwenye nafasi ya mtendaji mkuu mwaka 2014 pamoja na Ullah, hisa za Afren zilipanda kwa asilimia 3.5.

Baada ya kuwafukuza watendaji hao, mwenyekiti mtendaji wa Afren, Egbert Imomoh, alisema: “Uamuzi na hatua za makusudi tulizozichukua leo hii hazitamwacha huru yeyote anayetuhumiwa na inadhihirisha ni kwa namna gani Afren inashughulikia kwa umakini mkubwa kashfa hii. Mtazamo wetu kwa sasa ni kutekeleza fursa tulizonazo katika mazingira ya uwazi zaidi kwenye biashara kwa misingi ya uadilifu.”

Kwa sasa nafasi ya Mtendaji Mkuu inashikiliwa na Alan Linn wakati David Thomas ndiye Ofisa Uendelezaji Mkuu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *