GREENLAND: Ulevi, ukosefu wa usingizi unavyochochea watu kujiua

Jamii Africa

Matukio ya watu kujiua yameendelea kushamiri katika maeneo mbalimbali nchini. Watu ambao wanaondoa uhai wao kwa kunywa sumu, kujinyonga au kujirusha kwenye majengo marefu, sio mambo mageni tena. Zipo sababu mbalimbali ambazo zinawasukuma watu kujiua ikiwemo mabadiliko ya mfumo wa maisha.

Lakini umewahi kujiuliza ni nchi gani inayoongoza kwa watu kujiua? Greenland inatajwa kuwa nchi ya kwanza yenye viwango vikubwa vya watu wanaojiua duniani.

Kimsingi Greenland sio nchi. Bado inachukuliwa kama sehemu ya Ufalme wa Denmark. Hata hivyo, katika siku za karibuni, Greenland imetambuliwa kama ‘nchi huru’, ikiwa na maana kuwa inafanya kazi kama Taifa huru katika maeneo mengi lakini sio katika mambo yote.

Greenland haitambuliki kama nchi rasmi, na huwezi kuiona kwenye orodha ya nchi zenye viwango vikubwa vya kujiua, lakini kiuhalisia inaongoza duniani kwa matukio hayo. Kwenye orodha hiyo, Guyana inatajwa kuwa katika nafasi ya kwanza, kwa wastani watu 44.2 kati ya 100,000. Ikiwa ina maana kuwa kati ya watu 100,000 wa nchi hiyo 44 hujiua kila mwaka.

Hata hivyo, nchini Greenland hali ni mbaya zaidi. Kulingana na ripoti za kuanzia mwaka 1985 hadi 2012, wastani wa  viwango vya kujiua katika nchi hiyo ulikuwa watu 83 kati ya 100,000, ambapo ni karibu mara mbili zaidi ya Guyana.

                                      Polisi wakibeba mwili wa mtu aliyejiua

Greenland imeziacha kwa mbali nchi zote duniani katika matukio makubwa ya watu wake kujiua, na matukio haya hayapungui badala yake yanaongezeka kila mwaka. Kwa kawaida, lazima kuna tatizo ambalo linasababisha hali hiyo kutokea.

Kwa haraka haraka utakuwa na maswali mengi ya kutaka kufahamu kwanini wakazi wa Greenland wanashawishika kuondoa uhai wa maisha yao kwa kiasi hicho. Watu wengi katika nchi hiyo wana kipato kizuri na uhakika wa kupata pensheni nzuri kabla na baada ya kustaafu.

Lakini bado asilimia 20 ya wakazi wa Greenland wamewahi kuthubutu kujiua angalau mara moja katika maisha yao. Hiyo ina maana kuwa watu 2 kati ya 10 wana uwezekano mkubwa wa kujiua.

Swali la kujiuliza ni kwamba nani alaumiwe kwa matukio ya kujiua nchini Greenland? Jibu ni wananchi wenyewe wa Greenland kutokana na sababu zifuatazo:

 Ulevi

Kwa tafsiri nyepesi neno ‘Greenland’ ni ardhi yenye uoto wa kijani. Lakini Greenland tunayoizungumzia hapa haina sifa hizo. Hali ya hewa ya nchi hiyo ni ya baridi nyingi. Sehemu kubwa imefunikwa na barafu na kuzuia mimea kuota.

Kulingana na historia ya nchi hiyo, alikuwepo mtu mmoja maarufu ajulikanaye kama Viking Erik ambaye alilipa jina eneo hilo ‘Greenland’ (ardhi ya kijani). Alifanya hivyo ili kumshawishi mwenzake kuungana naye ili waanzishe makazi katika nchi hiyo.

Ili kufanikisha hazima yake, alichagua jina la ‘Green’land, japokuwa kulikuwa hakuna kitu kama hicho katika nchi hiyo.

Wakati wa majira ya joto, wastani wa jotoridi katika nchi hiyo huwa kati ya juzi joto 0 hadi 10 (10C). Wakati wa majira ya baridi (winter), jotoridi hushuka hadi juzi joto sifuri (0C). Nachelea kusema, Greenland ni kama kisiwa kilichofunikwa kwa barafu.

                       Barafu imefunika sehemu kubwa ya nchi ya Greenland

Ukweli ni kwamba, watu wanaoishi kwenye miji yenye baridi wanaowezekano mkubwa wa kuathirika na ulevi.  Watafiti wanaeleza kuwa kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya idadi ya watu wanaojiua na matumizi ya pombe.

Matumizi ya pombe ni tatizo kubwa la kijamii nchini Greenland. Pombe inasimama kama chanzo kikubwa cha ugomvi wa kifamilia, udhalilishaji wa kingono, ukosefu wa ajira, jambo linalochangia janga kubwa la kujiua katika nchi hiyo.

Ukosefu wa usingizi

Sehemu kubwa ya Greenland iko kwenye eneo la juu kabisa la nchi za Kaskazini, ambazo zinapata kipindi kimoja cha baridi. Pia inapata kipindi kimoja cha joto ambapo jua halipotei (sunset).

Katika eneo hilo la juu kabisa la Kaskazini mwa dunia, nchi zake nyingine zinatawaliwa na vipindi vingi vya baridi na giza hata wakati wa mchana na wakati wa majira ya joto, jua haliondoki angani.

Katika eneo hilo, kuna siku 120 katika mwaka ambapo jua halitui (sun never set), siku 108 katika mwaka jua halichomozi, na siku 137 tu ndiyo hupata mwanga na giza.

Unaweza kufikiri kwamba watu wanaweza kujiua kwasababu hakuna ishara ya jua wakati wa mchana hasa majira ya baridi, lakini la kushangaza ni kwamba tafiti zinaeleza kuwa matukio mengi ya kujiua yanatokea wakati wa majira ya joto.

Wataalamu wanasema wakati wa joto, watu hawapati usingizi wa uhakika jambo linalowaletea msongo wa mawazo na mkazo. Zaidi ya hapo, ukosefu kabisa wa giza unaweza kuathiri mwili wa binadamu na kutengeneza homoni ya ‘serotonin’ ambayo ni mahususi kusawazisha hali na hisia.

Swali la kujiuliza ni rahisi kwa kiasi gani akili zetu zinaweza zikabadilisha mfumo wa kupata usingizi kulingana na hali ya hewa? Hata hivyo sababu zote mbili – ulevi na ukosefu wa usingizi hazichukuliwi kama sababu zenye nguvu.

Kujiua halikuwa tatizo la siku zote nchini Greenland. Matukio ya kujiua yalikuwa machache katika miaka ya 1950. Baada ya kuingia miaka ya 1960, idadi ya matukio ya kujiua iliongezeka maradufu. Sababu za asili kama hali ya hewa zisingeweza kusababisha ongezeko hilo. Lakini zipo sababu zingine…

Uhamiaji na utengano

Greenland haina wakazi wengi ukilinganisha na nchi nyingine duniani. Japokuwa ni miongoni mwa visiwa vikubwa duniani ina wakazi wapatao 56,400 na 16,000 kati ya hao wanaishi katika mji mkuu wa Nuuk. Wakazi wengine wanaishi pembezoni mwa jiji hilo na wengine kwenye vijiji vya mbali ambapo vijiji vingine vina wakazi wasiozidi 50.

                            Makazi ya watu wa mji wa Nuuk, Greenland

Mnamo 1960, Greenland iliamua kutoendelea kuvisaidia vijiji vya mbali. Vijiji hivyo vilikuwa mbali na makao makuu ya Serikali na ikawa vigumu kwa wakazi wake kupata huduma muhimu za kijamii. Watu waliokuwa tayari kuondoka kwenye vijiji hivyo walipelekwa mjini ili kupata makazi na huduma za kijamii.

Lakini watu wengine walikataa kuondoka na kuamua kubaki katika vijiji hivyo. Walitaka kuendelea kulinda utambulisho na nyumba za waasisi wa kabila la Inuit. Kwa bahati mbaya, hawakuwa na chaguo tena zaidi ya kuondoka na kuungana na wenzao waliopo mjini.

Wakazi wa mjini hasa mji mkuu wa Nuuk wanawaona watu hao wanaohamia katika miji yao kama wakimbizi na wakati mwingine wanawatenga katika shughuli muhimu za kiuchumi na  kijamii. Kutokana na kadhia hiyo, wale wanatajwa kuwa ni wakimbizi hujiua kwasababu ya kutengwa na kunyimwa haki za msingi za kuishi.

Hata hivyo, Serikali ya Greenland imechukua hatua mbalimbali kupambana na janga hilo kwa kutengeneza miundombinu ya simu za mkononi kuongeza mawasiliano na kutoa ushauri kwa watu wenye hatari ya kujiua kuendelea na maisha.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *