HECHE: ‘Dowans wakilipwa utawala wa JK matatani’

Jamii Africa

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimemtahadharisha Rais Jakaya Kikwete na Serikali yake, kutodhubutu kutumia sh. bilioni 111
za walipa kodi kuilipa kampuni ya Dowans, na iwapo Serikali haitakuwa sikivu katika hilo, utakuwa ndiyo mwisho wa utawala wake. Kimesema, endapo Rais Kikwete ataamrisha Serikali ilipe fedha hizo kwa kampuni hiyo ya Dowans, iliyoridhi mkataba wenye utata kutoka Richmond, Chadema kitaungana na Watanzania nchini kote kuingia mitaani kushinikiza mkuu huyo wa nchi kuondoka mara moja madarakani.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema taifa (BAVICHA), John Heche, wakati alipokuwa akihutubia mkutano wa
hadhara, uliofanyika Nyamongo mjini Wilayani Tarime mkoani Mara, mkutano ambao ulihudhuriwa na watu wengi. Heche ambaye alikuwa akishangiliwa muda wote mkutanoni hapo, alisema Chadema haipo tayari kuona Watanzania wanaishi maisha magumu, huku Serikali yao ikiidhinisha mabilioni ya fedha kuilipa Dowans, wakati imeshindwa kulipa hata madeni ya walimu, kusomesha bure wanafunzi nakadhalika.

John Heche

“Hakiamungu Dowans ikilipwa, Rais Kikwete hatamaliza miaka yake iliyosalia uongozini. Naamini hapa wapo maofisa Usalama wa taifa
pamoja na polisi, nasema wakiilipa Dowans nchi itachimbika…wajaribu waone, safari hii tutawasha moto wa ajabu!.

“Kama Serikali imeshindwa hata kuwalipia karo wanafunzi, imeshindwa kulipa madeni ya walimu wetu…leo hii waje kuilipa Dowans?. Nasema
patachimbika na JK hatamaliza muda wake”, alisema mwenyekiti huyo wa Bavicha taifa, huku akishangiliwa na umati mkubwa wa watu, huku sauti
za baadhi ya raia zikisikika zikisema Serikali lazima ishtakiwe Mahakama ya Kimataifa ya ICC.  Heche alisema, Serikali ya CCM imeshindwa kabisa kuwaletea wananchi wake maendeleo makubwa, badala yake inaruhusu rasilimali za nchi kuporwa na wawekezaji kutoka Ulaya.

Aidha alisema: “Mapinduzi yoyote wakati mwingine yanakuja kwa namna tofauti. Tumeona huko Libya, Misri na Tunisia…Rais wa nchi hizi
walikuwa hawawasikilizi wananchi, lakini wananchi waliposema hapana kimeeleweka. Chadema tunasema ole wao wailipe Dowans”.

Kuhusu mikataba ya kifisadi, Heche ambaye alikuwa ameongozana na mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Mara, Machage Machage na viongozi wa
chama hicho wilaya ya Tarime, alisema, Serikali ya CCM imekuwa ikisaini mikataba aliyoiita ya kipumbavu, ambayo hailinufaishi taifa na wananchi wake, kinyume na sheria za nchi. Pamoja na hayo, alitumia pia fursa hiyo kumshutumu Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa kufanya ziara wilayani Tarime kisha kuacha kuzungumzia mauaji ya watu wanne waliopigwa risasi za moto na askari polisi katika vurugu za mgodi wa Nyamongo, badala yake alikwenda kuzungumza na uongozi wa mgodi huo.
“Tumemuona juzi hapa Waziri Mkuu Pinda alikuja akawasusa hakuongea nanyi juu ya mauaji ya Mei 16 mwaka huu!. Lakini badala yake aliingia
mgodini kuzungumza na Wazungu. Hivi huyo ni kiongozi mwenye uchungu kweli na ninyi?”, alisema Heche huku baadhi ya sauti za watu
zikisikika zikisema: “Tumechoshwa nao, tupo tayari kumwagana damu sasa potelea mbali hata tufe ili taifa tulikomboe”.

Hata hivyo, Heche alimrushia kombora la maneno Katibu wa Itikadi na uenezi wa CCM, Nape Nnauye kwa kusema, mwana CCM huyo ni mropokaji na hana machungu na Watanzania, na alimtaka ajichunge sana na kauli zake anazozitoa kwa viongozi wa Chadema kwani siyo saizi yake.

“Yupo mtu anaitwa Nape Nnauye, huyu mtu kwanza anaishi kwa nafasi za kuteuliwa zilizojaa upendeleo kutoka kwa watu wake wa CCM. Ninamtaka
Nape aache uropokaji, achunge mdomo wake…siku Chadema ikishika dola sijui atakimbilia wapi?. Mtu mwenyewe hajawahi kugombea na kushinda
hata ubalozi wa nyumba kumi, uenyekiti wa mtaa wala udiwani, huyu siyo saizi yetu anajitapa tu”, alisema Heche.

Awali mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Mara, Machage aliwataka wakazi wa mkoa wa Mara na Tarime kutambua ya kwamba, wasikubali kupakwa mafuta mgongoni kwa kigezo cha amani, badala yake waamke wadai haki zao za msingi. “Wana Nyamongo, tafuteni haki zenu na siyo kuendelea kuhubiriwa amani amani…Serikali hii ni sawa kwamba imeoza, haiwajali wala haifikilii kuwaondolea umasikini mlionao wakati mna utajiri mkubwa wamadini” alisema Machage.

 

Na Sitta Tumma

1 Comment
  • hakika kama watu wangejua nini maana ya uchungu wa NCHI au uzalendo hawa CCM mwisho wao ungekuwa mwa 2010 kwenye uchaguzi mkuu uliopita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *