MIAKA kadhaa iliyopita kulikuwa na matangazo mengi kuhusu ugonjwa wa Ukimwi kwenye vyombo mbalimbali vya habari; redio na magazeti.
Watu wengi walielimika kupitia vyombo hivyo na hakika uelewa wa namna Ukimwi unavyoambukiza, namna ya kujikinga na hata kuhudumiwa pindi “unapoukwaa.”
Hata hivyo, pamoja na ongezeko la njia za kupashana habari kupitia mitandao ya kijamii, simu za mikononi na uwepo mkubwa teknolojia ya habari, matangazo ya ugonjwa huo yamepungua mno, je hii maana yake nini?
Je, ugonjwa umepungua au kwamba watu wameuzoea na kuuona kama ugonjwa mwingine mdogo tu?
Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa Kushughulia Ukimwi– Tawi la Tanzania (UNAIDS – Tanzania) mwaka 2015, idadi ya watu wote nchini ilikadiliwa kuwa milioni 49 ambapo watu milioni 1.4 walikadiliwa kuishi na Virusi vya Ukimwi (VVU) sawa na asilimia 4.7.
Mwaka 2015 pekee watu 54,000 waligundulika kuwa na VVU huku watu 36,000 walikufa kwa maradhi yatokanayo na Ukimwi. Watu wazima wenye umri wa miaka 15 na zaidi wanaoishi na VVU ni milioni 1.3, kati yao wanawake ni 780,000 na wanaume ni 520,000.
Vilevile watoto wenye miaka 0 hadi 14 wanaoishi na VVU ni 91,000 wakati yatima waliotokana na athari za Ukimwi wenye umri wa miaka 0 hadi 17 ni 790,000.
Seli za CD4 ni seli nyeupe za damu zenye shughuli muhimu katika mfumo wa kinga ya mwili. Seli za CD4 wakati mwingine hujulikana kama seli za T (T-cells), limfositi za T (T-lymphocytes) au seli saidizi (Helper cells).
Idadi ya seli za CD4 inatoa ishara ya afya ya mfumo wako wa kinga, ambayo ni njia ya asili ya mwili kupambana na maradhi mbalimbali.
Idadi ya seli zako za CD4 ni kipimo cha namba ya seli za damu katika milimita za ujazo wa damu (kiwango kidogo cha sampuli ya damu). Sio kiwango cha idadi ya seli zote za CD4 katika mwili wako.
Idadi kubwa ya seli za CD4 huashiria uimara wa kinga ya mwili. Idadi ya seli za CD4 kwa mtu asiye na VVU inatarajiwa kuwa kati ya 500 na 1,600.
Watu wanaoishi na VVU wenye seli za CD4 zaidi ya 500 mara nyingi huwa katika afya njema. Watu wanaoishi na VVU wenye idadi ya seli za CD4 chini ya 200 wapo katika hatari ya kupatwa na maradhi hatari kama kifua kikuu.
Matibabu ya kufubaza VVU yanapendekezwa kuanzwa kwa wote waliogundulika kuwa na VVU.
Ikiwa una VVU na haupati matibabu ya VVU, idadi ya seli zako za CD4 zitaendelea kushuka kadili muda unavyokwenda. Vile idadi ndogo ya seli za CD4 inavyokuwa ndivyo mfumo wa kinga wa mwili unavyozidi kuharibika na inavyokuwa rahisi kupata maradhi mbalimbali kama kifua kikuu na kuhara sugu. Inategemewa kupanda kwa idadi ya seli za CD4 pale unapoanza matibabu ya VVU.
Hapo mwanzo, idadi ya seli za CD4 ilitumika kutoa muongozo wa maamuzi ya kuanza matibabu ya VVU. Ingawa sasa tunatambua kwamba watu wote wanapatikana kuwa na VVU wanapaswa kuanza matibabu haraka iwezekanavyo pindi tu wanapogundulika kuwa na VVU.
Unapoonza matibabu ya VVU, kipimo cha mzigo wa virusi (viral load) ndio kiaahiria muhimu sana kwa afya yako na ubora wa tiba unayopata kuliko idadi ya seli za CD4.