“Wananchi wanataka maendeleo. Wanataka huduma bora za jamii. Wanataka maji safi na salama, wanataka elimu bora, huduma za afya, na miundo mbinu bora. Katiba mpya si kipaumbele cha Watanzania. Wananchi wanataka ‘Ukatiba’ na sio katiba. Wananchi wanataka maendeleo”.
“Serikali ya awamu ya Tano haitashughulika na katiba, itaendelea kutumia katiba iliyopo. Itajikita katika kutatua matatizo na kero za wananchi, kupambana na rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya fedha za umma, matumizi mabaya ya madaraka.” Hizi ni kauli au msimamo ambao tumekuwa tukiisikia mara nyingi kutoka kwa viongozi wetu hasa wale wa chama tawala.
Inawezekana vipi Watanzania, tuliamua kutumia rasilimali fedha, rasilimali watu na muda kujaribu kuandika katiba mpya baada ya muda mfupi tu tuseme kuwa suala hili si kipaumbele tena. Zoezi la kuandika katiba mpya ambalo halikuweza kukamilika lilitumia rasilimali nyingi sana.
Tulifanya hivyo, kwani tulijua kuwa tunahitaji katiba mpya na tulikuwa na sababu za msingi kabisa za kuandika katiba mpya. Baada ya takribani miaka miwili kupita tunasema kuwa suala hili si kipaumbele tena! Nadhani kwa kuchukua msimamo huu tutakuwa na kila sababu ya kujitathmini.
Swali la msingi hapa ni kwanini ilikuwa muhimu kuandika katiba mpya miaka miwili iliyopita na kwanini sasa isiwe muhimu? Swali hili linahitaji majibu ya kina. Tulitumia muda, tulitumia fedha, tulitumia watu, utaalamu wao na nguvu zao katika zoezi la kuandika katiba mpya. Haliwezi likafa hivihivi. Mzee Warioba, Humphrey Polepole, Prof. Kabudi, Mzee Salim, Jaji mstaafu Augustino Ramadhani, Mzee Butiku, Marehemu Mvungi na wengine wengi, walifanya kazi kubwa ya kuzunguka nchi nzima, wakakusanya maoni ya wananchi.
Nina uhakika walikesha usiku wakisoma na kuandika, wakatuletea rasimu ya katiba ambayo ilikuwa na mambo mazuri sana, leo hii hatuwezi kuitupa kazi yao hii nzuri. Kazi hii ni lazima tuienzi na kuithamini. Ombi langu kwa Wazee wetu hawa na vijana wafufue mjadala huu na tupate katiba ambayo itakubalika na kuheshimika na wengi.
Inapojengwa hoja kuwa ‘wananchi wanataka maendeleo na sio katiba’! hivi maendeleo ni nini? Je maendeleo ni barabara za lami, shule, afya nyumba za kifahari, magari n.k. Je, maendeleo ni ya watu au ya vitu? Je, iwapo hata kama utaishi katika ukwasi mkubwa na kuwa vitu hivyo nilivyovitaja hapo juu lakini huna uhuru, unaishi katika woga, huwezi kutoa maoni yao kwa uhuru.
Je, hayo ni maendeleo? Ni vyema tukabeba dhana pana ya maendeleo. Maendeleo si ya vitu, maendeleo ni ya watu.
Maendeleo ni pamoja na kuheshimu haki za uraia, kuheshimu haki za binadamu, kuimarisha demokrasia, utawala wa sheria na uhuru wa kisiasa. Maendeleo pia yanahusisha suala zima la kujitegemea, ushirikishwaji katika maamuzi muhimu na chaguzi huru za haki. Wananchi kuwa na uwezo wa kuamua serikali wanayoitaka na serikali kutekeleza kulingana na matakwa ya wananchi.
Dhana ya maendeleo hubeba masuala haya yote na si tu ubora wa huduma za jamii au ukuaji wa uchumi. Ili ukuaji wa uchumi na ubora wa huduma za jamii uwe na maana au manufaa kwa wananchi, ni lazima wananchi waishi kwa uhuru, bila woga na kwa kuheshimu utawala wa sheria.
Tutaweza vipi kufikia maendeleo katika dhana hii pana bila kuwa na katiba bora? Masuala haya yanatawaliwa na mfumo wa kisheria na taasisi imara. Mfumo wa kisheria unachimbuka kutoka katika sheria mama ambayo ni katiba.
Sheria nyingine zote zinatokana na katiba. Na kunapokuwa na mgongano wa sheria na katiba, basi katiba huwa na nguvu. Sasa tutaweza vipi kuwa na maendeleo wakati hatuna katiba bora? Sote tunaafikiana katika hili kuwa hatuna katiba bora ndio maana tulifanya juhudi za kuandika katiba mpya ambazo zilikwama kwa makosa tuliyoyafanya.
Hivyo Watanzania, ili tupate maendeleo tunahitaji katiba bora. Katiba bora itatupa uchaguzi usio na mashaka na unaokubalika, kuaminika na ulio uhuru na wa haki. Kwasababu hiyo, ndio maana Tume ya Warioba ilipendekeza kuwe na Tume Huru ya Uchaguzi. Ilipendekeza katiba iruhusu wagombea binafsi. Hii ni haki ya uraia ambayo hakuna mtu mwenye mamlaka ya kumyang’anya raia wa nchi.
Uchaguzi bora ni jambo la msingi sana tukiweza kuwa na chaguzi bora, pia tutaweza kulinda na kudumisha Amani na utulivu wetu. Amani na Utulivu ni changamoto kubwa sana katika nchi nyingi za Afrika na hasa baada ya uchaguzi. Amani na utulivu ni na tunda la haki na ni nyenzo muhimu sana katika kujiletea maendeleo ambayo tunayakusudia.
Katiba bora itatuwezesha kujenga taasisi imara ambazo zitakuwa na mgawanyo mzuri wa madaraka. Muhimu zaidi katiba bora itatupa taasisi ambazo zinaweza kuchungana na kuwajibishana. Tutakapoweza kujenga taasisi imara vita dhidi ya rushwa, ufisadi, na matumizi mabaya ya raslimali zetu, itakuwa ni vita endelevu na si ya mtu mmoja.
Nimalizie Makala yangu kwa kunukuu ahadi ya CCM iliyopo katika ilani ya uchaguzi 2015. Inasema hivi: “Ili kuendeleza Utawala Bora, Demokrasia na Uwajibikaji,katika kipindi cha miaka mitano ijayo (2015-2020), CCM itahakikisha kuwa, Serikali inatekeleza yafuatayo:– Kukamilisha mchakato wa kutunga Katiba mpya na kuanza kuitekeleza kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba”.
Ni vizuri ahadi hii kwa Watanzania ikaheshimiwa na kutekelezwa. Haja ya mja hunena muungwana ni vitendo.
Mwandishi wa makala hii ni Selemani Rehani.