Ifahamu ndoto inayowatenganisha na kuwaunganisha watanzania

Jamii Africa

Ninayo ndoto. Inaweza ndoto hii isitimie katika uhai wetu, lakini inaweza kutimia kwa vizazi vijavyo. Ninayo ndoto kuwa ipo siku moja Watanzania tutaweka tofauti zetu pembeni, na kuweka mbele maslahi mapana ya nchi, maslahi mapana ya vizazi vijavyo.

Hatimaye tutaamua kumalizia mchakato wa kuandika katiba mpya. Katiba hii mpya itakuwa ni dira sio tu kwa kipindi hiki bali itakuwa ni dira katika miaka 100 ijayo na kwa vizazi vijavyo.

Watanzania tutaandika katiba kwa kuzingatia misingi muhimu sana ya kuhakikisha kuwa katiba yetu inaruhusu mgawanyiko wa madaraka kati ya mihimili mitatu yaani; Bunge, Dola na Mahakama. Mihimili hii itaweza kusimamiana na kuchungana na kila mhimili utakuwa na uhuru na utaweza kutekeleza majukumu yake bila kuingiliwa na mhimili mwingine.

Natamani tuwe na katiba ambayo inatoa mgawanyo wa madaraka kati ya mihimili hii mitatu. Mahakama ambayo itakuwa na uhuru, haingiliwi, ina fedha za kutosha, wafanyakazi wa kutosha wenye ari ya kufanya kazi, majengo ya kutosha na vitendea kazi vyote vya kutosha. Ni ndoto yangu haki itapatikana tena kwa wakati bila kucheleweshwa.

Mrundikano wa kesi utaondoka. Ni ndoto yangu kuona tuna Rais ambaye hana madaraka makubwa sana. Ni ndoto yangu kuona baadhi ya madaraka yanakasimishwa kwa taasisi na vyombo mbalimbali. Mfumo huu utaongeza uwajibikaji na vita vya rushwa vitakuwa endelevu.

Ni ndoto yangu kupitia zoezi hili la kuandika katiba mpya, tutaweza kujenga taasisi imara. Hapa tukumbuke maneno aliyosema aliyekuwa Rais wa taifa kubwa la Marekani, Barack Obama wakati akihutubia Bunge la Ghana ambapo alisema: “ Africa haihitaji watu wenye nguvu, inahitaji taasisi zenye nguvu.”

Katika karne ya 21, taasisi zenye uwezo, uhuru na uwazi ndio ufunguo wa maendeleo. Tunahitaji kuwa na Bunge lenye meno, tunahitaji kuwa na jeshi la Polisi lenye weledi na uadilifu mkubwa, tunahitaji Mahakimu na Majaji ambao wapo huru na wanatoa haki.

Tunahitaji waandishi wa habari na vyombo vya habari huru, vyenye weledi, uadilifu na vinavyofuata maadili ya uandishi. Tunahitaji asasi za kiraia na sekta binafsi yenye nguvu itakayoleta na kuamsha mijadala na tafakuri pana.

Haya ni baadhi tu ya mambo ambayo yanaweza kuifanya demokrasia iwe na maana kwa watu na iwe endelevu. Hii ni ndoto ambayo niliyonayo.

Ni ndoto yangu kuwa ipo siku moja moja tutakubaliana namna bora ya kuendesha mfumo wa vyama vingi vya siasa. Tutaunda taasisi zinazokubalika na kuaminika katika kusimamia siasa za kidemokrasia za vyama vingi. Tutakuwa na Tume Huru ya Uchaguzi.

Tutakuwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa ambayo haigemei upande wowote. Hiyo itatuwezesha kuendesha siasa za vyama vingi kwa ustaarabu, kuheshimiana na kupendana. Hili linawezekana.

Tutaacha siasa za chuki, ghilba, kuchafuana, kutukanana, ubabe, na visasi. Hiyo siku inakuja. Siku inakuja ambapo kiongozi mkuu wa chama kikuu cha upinzani ataheshimiwa na kupewa nafasi kama viongozi wengine waliopo serikalini.

Siku inakuja ambapo vyama vya upinzani vitaweza kufanya shughuli zake za kisiasa kama wanavyofanya wanasiasa wa chama kilichopo madarakani. Vyama vya upinzani vitaweza kufanya mikutano ili kunadi sera zake na kutafuta wanachama kama katiba na sheria ya vyama vingi inavyoelekeza.

Siku inakuja ambapo chaguzi zetu zitakuwa huru, za haki na zinazoaminika na kufikia viwango vya kimataifa. Tutafanya kampeni za kistaarabu. Tutawapa wananchi nafasi ya kuchagua na kuamua mustakabali wao. Tutashindanisha sera na mipango kwa hoja na si kwa vitisho, ulaghai na ghilba.

Tutawaheshimu wapiga kura kwa kufikisha kwao hoja zenye mashiko na kueleza mipango yetu kwenye namna vyama vitapata ridhaa na vitashughulikia vipi matatizo na changamoto zao.

Siku hiyo inakuja ambapo asasi za kirai zitaweza kuendesha shughuli zake kwa uhuru bila woga. Asasi za kiraia zitakuwa huru kukosoa na kupongeza pale inapostahili. Vyombo vya habari vitaandika habari za kweli, uchambuzi na uchunguzi bila woga wa kufungiwa au kutozwa faini. Wananchi watakuwa huru kutoa maoni yao na kueleza mawazo. Siku hiyo inakuja. Ni suala la muda tu.

 

Mwandishi wa makala hii ni Selemani Rehani

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *