Diplomasia ni nguzo muhimu ya kuimarisha mahusiano na mataifa mengine ya kikanda na kimataifa. Kwa kutambua hilo viongozi wetu tangu taifa letu linapata uhuru waliweka misingi ya ushirikiano wa kimataifa ili kujenga diplomasia imara.
Tanzania imejengwa kwenye misingi ya amani na mshikamano ambayo inawaunganisha wananchi wote bila kujali tofauti za kidini, kabila au siasa. Misingi hii imeiweka Tanzania kwenye ramani ya dunia katika mambo mbalimbali ikiwemo kuitwa kisiwa cha amani.
Misingi hiyo imejengwa kwenye Sera ya Nje ya Tanzania (Tanzania Foreign Policy) ambapo toleo jipya limetoka 2015 baada ya kupitia mabadiliko mbalimbali ili iendane na mazingira ya wakati huu.
Uundwaji wa Sera hii imezingatia maadili na msimamo wa Tanzania ambao umeanishwa kwenye Waraka wa Rais namba 2 uliotolewa mwaka 1964 na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ambao uliweka misingi na malengo ya Sera ya Mambo ya Nje.
Tangu wakati huo mwenendo na maudhui ya Sera ya Nje yamekuwa yakiongozwa kwa misingi na maadili hayo ambayo ni pamoja na:
- Ujenzi wa uhuru, haki na usawa
- Kulinda utaifa, mipaka utawala na uhuru wa kisiasa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
- Kusaidia mapambano dhidi ya ukoloni, ubaguzi wa rangi na ukoloni mamboleo
- Kuwasaidia watu wanaonyanyaswa duniani kote
- Kukuza umoja wa Afrika
- Kusimamia sheria zinaheshimu kutokuingilia mambo ya ndani nchi nyingine
- Kusaidia utekelezaji wa sera ya kutofungamana na upande wowote
- Kuungana na Umoja wa Mataifa katika kutafuta amani na usalama wa kimataifa
- Kuhimiza ujirani mwema
Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Augustine Maiga akizungumza kwenye mkutano mmojawapo wa Umoja wa Mataifa
Sera hiyo mpya ya nje ya Tanzania imepitia mabadiliko mbalimbali ya kimfumo ili kuendana na mazingira ya sasa ya dunia ambayo yameyaweka mataifa karibu kuliko wakati mwingine wowote. Malengo ya sera hiyo ni pamoja na kuanzisha, kuhimiza na kulinda maslahi ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiuchumi ya Tanzania kupitia diplomasia endelevu ya kiuchumi.
Pia kuhakikisha mahusiano ya Tanzania na nchi nyingine, mashirika ya kimataifa yanachochewa kulingana na maslahi ya kiuchumi. Kujenga uchumi wa kujitegemea, kuimarisha amani na usalama wa taifa na kusaidia juhudi za kikanda na kimataifa za kuifanya dunia kuwa na amani.
Kuendeleza mafungamano ya kisiasa kikanda, kijamii na kiuchumi. Kutengeneza mazingira yatakayoiwezesha Tanzania kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kikanda na ulimwengu na usuluhishi wa kimataifa.
Ili kufanikisha malengo hayo ya Sera, Tanzania inatumia mikakati mbalimbali ili kuendana na mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi kwa kuzingatia misingi iliyowekwa na waasisi wa taifa letu. Mikakati hiyo imejikita kutengeneza mazingira mazuri ya ndani na nje ya utekelezaji wa sera hiyo ili kuimarisha diplomasia ya kimataifa.
Ikumbukwe kuwa Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini Mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya Madola, Umoja wa Mataifa (UN) na jumuiya zingine za kimataifa.
Sera hiyo pia inaitaka Tanzania kuimarisha utendaji wa mashirika ya kimataifa yasiyo ya kiserikali ambayo yanafanya kazi nchini ili kuhakikisha huduma mbalimbali zinazotolewa na mashirika hayo zinaendana na sheria za nchi.
Usimamizi na mapitio ya sera imekabidhiwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Wizara hiyo imepewa majukumu ya kuratibu shughuli zote kimataifa na kuimarisha shughuli zote kidiplomasia zinazoiunganisha Tanzania na mataifa mengine duniani.