MIONGONI mwa mafanikio ya harakaharaka ya uongozi wa Rais John Magufuli tangu aingie madarakani, Novemba 5, mwaka jana, ni wingi wa madawati katika shule nchini.
Idadi kubwa ya shule, hasa za msingi, zimekuwa na “mafuriko” ya madawati, kiasi cha kukosekana mahali pa kuyahifadhi, kwani yanazidi mahitaji ya shule. Mwongozo wa Wizara ya Elimu unahimiza dawati moja kukaliwa na wanafunzi watatu hadi wanne.
Pamoja na mafanikio hayo, bado upo “ukame” wa madawati katika Shule ya Msingi Mkuyumani, Kata ya Majimoto, Wilaya ya Mlele, Mkoa wa Katavi.
Shule hiyo yenye wanafunzi 2500, ni wanafunzi wanaozidi kidogo, 1750, ndiyo wanaokalia madawati wakiwa darasani, huku wengine wakikaa juu ya sakafu au kukalia ‘madumu.’
Idadi hiyo ni sawa na asilimia 70 ya wanafunzi wanaosoma vyema, huku wenzao, asilimia 30 “wakiteseka” kuipata elimu. Pamoja na kuwepo changamoto huyo ya madawati, shule hiyo pia ina upungufu wa walimu; kwani ina walimu watatu tu kwa shule nzima.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mbamba Makoye ameieleza FikraPevu kuwa shule yake iliyoko katika Halmashauri ya Mpimbwe ina walimu watatu wa kuajiliwa.
“Tunashukuru pia kwamba pamoja na kuwa na idadi ndogo ya walimu wanaofundisha masomo yote na madarasa yote, pia tunao vijana wanne wa kujitolea, hawa wanatusadia sana,” anaeleza.
Mwalimu huyo anasema ongezeko la wanafunzi walioandikishwa darasa la kwana mwaka huu, linesababisha kukosekana kwa madawati ya kutosha.
Serikali ya awamu ya tano, chini ya Rais John Magufuli ilitangaza kuwepo kwa elimu bure kuanzia darasa la awamu hadi elimu ya sekondari, uamuzi ambao umeongeza wanafunzi katika shule za msingi na sekondari.
Pamoja na mwalimu Makoye kueleza hali hiyo kuwa ameizoea, walimu watatu anaowaongoza wameilalamikia, huku wakisisitiza kuwepo kwa mazingira bora ili wapate mwanya wa kufundisha vyema.
Mwalimu wa taaluma wa shule hiyo, Dickson Fabiani ameiambia FikraPevu kwamba mazingira yao ya kufundisha ni magumu na kamwe hayawezi kuwapa wanafunzi elimu bora. “Ninalazimika kufundisha madarasa matano na masomo yote, wakati sio utaratibu wa taaluma yetu katika kuwapa wanafunzi elimu nzuri,” anaongeza mwalimu huyo.
FikraPevu imebaini kuwepo kwa wanafunzi wanaofikia 250 kwa darasa moja na ambao hufundishwa kwa wakati mmoja, wengine wakiwa wamekaa chini.
Pia imebainika, mbali na uhaba wa madawati na walimu, shule hiyo inakabiliwa na upungufu wa matundu ya vyoo, hivyo kufanya mazingira ya kusoma na kusomesha kuwa magumu.
“Inasikitisha kuwa walimu wa shule hii wanatumia vyoo kwa pamoja, walimu hawana choo, hii siyo nzuri kwa utoaji wa elimu bora,” analalamika mwalimu Fabiani.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Nyasongwa Serengeti ameiambia FikraPevu kuwa Halmashauri ya Mpimbwe imeanza kufanya jitihada za kuondoa tatizo la wanafunzi kukaa chini kwani wameanza kutengeneza madawati 200 .
Mwandishi wa habari hizi aliyetembelea shule hiyo ya amebaini kuwa hata kama Halmashauri hiyo itatengeneza madawati hayo, bado hayatatosha.
Mmoja wa wazazi wa wanafunzi, Michael Kalubwa alisema kuwa ni jambo la kushangaza kwamba shule hiyo na nyingine za mkoa wake, bado zinakabiliwa na ukosefu wa madawati wakatizipo shule zilizozidisha madawati wakati wa zoezi la kuyatengeneza.