Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa kila mwaka watu 60,000 hufariki kutokana na ugonjwa wa kichaa cha mbwa, ambapo milioni 15 hupata matibabu ya ugonjwa huo na kuuweka miongoni mwa magonjwa hatari yanayoua watu wengi Afrika.
Asilimia 99 ya ugonjwa huo ambao kitaalamu unajulikana kama ‘rabies’ huenezwa kupitia mate ya wanyama akiwemo mbwa. Nusu ya wakazi wote dunia wanaishi katika mazingira yenye viashiria vya ugonjwa huo na kujiweka katika hatari ya kuambukizwa maradhi hayo.
Ingawa makundi yote ya watu wako katika hatari ya kupata ugonjwa huo, watoto walio chini ya umri wa miaka 15 ndio wanaothirika zaidi. WHO inasema watu 4 kati ya 10 wanaofariki kutokana na ugonjwa wa kichaa cha mbwa ni watoto walio chini ya miaka 15 huku wanaume wakiongoza kupata matibabu ya ugonjwa huo kuliko wanawake.
Njia za kuambukizwa
Kichaa cha mbwa ni ugonjwa hatari unaoathiri sana na virusi vya ugonjwa huo husababisha uvimbe kwenye ubongo (encephalytis). Virusi hizi zinaweza kutokea kwa binadamu na wanyama lakini ni mara chache hutokea kwa wanyama.
Kichaa cha mbwa kinaweza kusambazwa kwa mate ya wanyama, wengi tumezoea kwamba mbwa ndiye anasambaza kichaa, lakini wanyama wengine kama paka, popo, ng'ombe, mbweha, fisi na wengine wanaweza kukisambaza pia.
Njia za maambukizi ni mate na damu baada ya kung'atwa na mnyama mgonjwa. Watu wanaotibiwa mara moja baada ya kuambukizwa wanaweza kupona. Lakini tiba inahitaji kutekelezwa kabla ya virusi havijafika kwenye ubongo katika muda wa saa za kwanza baada ya kung'atwa.
Dalili za kwanza za kuambukizwa ni pamoja na homa na kuhisi mchonyoto katika eneo la mwili ambako mtu aling'atwa. Dalili nyingine ni kukasirika au kuogopa sana kwa ghafla, hofu ya maji, kukosa uwezo wa kutawala mwendo wa viungo vya mwili na kupoteza fahamu.
Inaelezwa kuwa dalili hizi zikionekana kwa mgonjwa ni ishara kuwa ubongo umeshambuliwa na hatua za haraka zisipochukuliwa mgonjwa anaweza kupoteza maisha.
Muda kati ya kuambukizwa ugonjwa na mwanzo wa dalili ni mwezi mmoja hadi miezi mitatu. Hata hivyo, kipindi hiki cha muda kinaweza kutofautiana kutoka chini ya wiki moja kwa zaidi ya mwaka mmoja. Kipindi cha muda kinategemea umbali virusi viliko hadi kufika kwenye mfumo mkuu wa neva.
Njia ya kudhibiti ugonjwa huo ni kuwachanja dawa pamoja na kinga mbwa wanaofugwa majumbani na endapo mtu anang’atwa na mbwa mwenye kichaa apate matibabu haraka ili kumuepusha na kifo. Kabla mgonjwa hajapelekwa hospitali ni muhimu kuosha kidonda au mchubuko kwa maji ya sabuni ili kupunguza virusi kusambaa maeneo mengine ya mwili.
Mradi wa kuzuia ugonjwa wa kichaa cha mbwa Tanzania
Mwaka 2010, serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani walipata msaada wa kifedha kutoka kwa Wakfu wa Bill na Melinda Gates kwa ajili ya program ya kuwajengea uwezo wananchi wa mikoa ya Kusini juu ya ugonjwa huo na jinsi ya kuzuia usienee kwa watu wengi.
Programu hiyo imelenga kupunguza vifo vinavyotokana na kichaa cha mbwa kwa kuanzisha kampeni ya kuwachanja mbwa wanaofugwa majumbani. Pia kuongeza wigo wa matibabu kwa watu walioathirika na ugonjwa huo. Wilaya 28 zimefaidika na mradi huo ambapo watu milioni 10 wamepata elimu ya kujikinga na ugonjwa huo na kampeni hiyo inaendelea mikoa mingine ya Tanzania.
Ugonjwa wa kichaa cha mbwa ni miongoni mwa magonjwa yanayoongozwa kwa kuuwa watu duniani yakiwemo malaria, UKIMWI, kifua kikuu na kuhara. Hivyo basi jitihada za pamoja zinahitajika kutokomeza ugonjwa na kuokoa maisha ya watu.