IDARA ya Kilimo katika Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani imeanza kutafuta ‘mchawi’ mara baada ya FikraPevu kuchapisha habari za wakulima kugoma kuchukua mbegu za muhogo aina ya Kibaha o26/Mkuranga 1.
Ofisa Ugani wa Kijiji cha Mhaga wilayani humo liliko Shamba Darasa la Mbegu, David Shangali, aliieleza FikraPevu kwamba uongozi wa idara ya kilimo umemtaka atoe maelezo kuhusiana na taarifa hizo.
“Nilipokea simu kutoka ngazi za juu wilayani kutaka nijieleze ni kwa nini nilitoa taarifa zile, nimeshawaandikia barua waliyoitaka nasubiri nione hatua gani watakazochukua,” alisema Shangali na kubainisha kwamba aliwaeleza kwamba mwandishi hakuandika taarifa za kweli.
Wakati Shangali akieleza hayo, mnamo Januari 31, 2017 majira ya saa 4:11 usiku, mwandishi wa FikraPevu alipokea ujumbe wa maandishi wa simu kutoka kwa Karume Chausa, Mtaalam wa Kilimo wa Idara ya Kilimo wilayani Kisarawe akilalamika ni kwa nini habari hiyo ilichapishwa akidai siyo ya kweli.
Lakini FikraPevu, ambayo haiandiki habari zisizofanyiwa utafiti, ilifika katika shamba darasa la mbegu za Kibaha 026 zinazoelezwa kuwa ni bora, ambapo licha ya mbegu hizo kukataliwa na wakulima, shamba hilo lenye ukubwa wa ekari nne limetelekezwa na kugeuka pori kutokana na kukosa palizi.
Januari 29, 2017, FikraPevu ilichapisha habari kwamba, wakulima wa Kijiji cha Mhaga, Kata ya Kibuta wilayani Kisarawe walikuwa wamegoma kuchukua mbegu hizo mpya za muhogo wakidai zinawatia hasara
“Mbegu hii siyo mkombozi kwa wakulima, itatutia umaskini kwa kutumia gharama nyingi katika palizi, lakini pia mihogo inakuwa na mizizi mingi kutokana na kukaa muda mrefu ardhini,” walisema wakulima hao.
Mbegu hiyo ambayo ilibuniwa na Kituo cha Kilimo Kibaha baada ya utafiti wa miaka mitatu ulioigharimu serikali fedha nyingi inadaiwa kutumia gharama nyingi wakati wa palizi kwa kuwa inakaa shambani miezi 12 kabla ya kuvunwa, tofauti na aina nyingine ya mbegu.
Watafiti katika Kituo cha Kibaha walibuni mbegu hiyo katika jitihada za serikali za kupata mbegu bora na kinzani kwa magonjwa yanayoshambulia zao hilo.
Asilimia 80 ya wakazi 10,146 wa Kata ya Kibuta wanajihusisha na kilimo, hususan mihogo, lakini kuikataa mbegu hiyo kunaonekana kuwarejesha kwenye changamoto za siku zote za kutumia mbegu za kubahatisha ambazo zinadaiwa hazistahimili magonjwa.
Wakulima hao walisema, awali walikuwa wakitumia mbegu ijulikanayo kwa jina la Rasta ambayo iliwaletea mavuno mengi kabla ya kuathiriwa na ugonjwa wa batobato na michirizi ya kahawia.
Inaelezwa kwamba, baada ya mbegu ya rasta kuathiriwa na magonjwa wakulima walilazimika kutumia mbegu ya Kiroba au Enyimba ambayo bado imeonekana kuwa na changamoto katika upatikanaji wa soko kwani mihogo yake huwa michungu endapo itacheleweshwa kuvunwa.
Uzaaji wa mbegu ya rasta unadaiwa ulikuwa mzuri na kuwanufaisha wakulima, ambapo kwa ekari moja mkulima aliweza kuuza hadi shilingi milioni moja tofauti na Kibaha 026 ambayo wanapata shilingi 600,000 tu kwa ekari moja.
Katika mahojiano na FikraPevu kwenye eneo la shamba hilo, Ofisa Ugani David Shangali alisema kwamba, ingawa kuna changamoto, mbegu hizo zinapaswa kugawiwa kwa wakulima wote watakaozihitaji na kuorodhedha majina yao kwa uongozi wa kijiji na kwamba wangepatiwa mizigo mitatu yenye fito 30.
Lakini kwa mujibu wa wakulima hao, hata kama mbegu hiyo ingekuwa inafaa, kiasi cha mbegu walichopanga kuwapatia ni kidogo na hakiwezi kutosheleza hata katika eneo lenye ukubwa wa robo eka.