MNAMO mwezi Agosti 2016, Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako, alitoa tamko kuwa kila mwanafunzi wa sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne lazima asome masomo ya sayansi.
Kauli hiyo ya waziri ilikuja miezi miwili baada ya Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, kuahirisha mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi na Sekondari nchini (Umitashumta na Umisseta), ambayo yalipangwa kufanyika kitaifa jijini Mwanza mwezi Juni 2016.
Michezo hiyo hukutanisha wachezaji waliochaguliwa kikanda kutoka shule mbalimbali nchini.
Sababu kubwa ya kuahirisha michezo hiyo, ilikuwa kupisha kampeni ya kuhakikisha kila shule inapata madawati ya kutosha.
FikraPevu inatambua kwamba, fedha zote zilizokuwa zimetengwa kutumika kwenye mashindano hayo zilielekezwa kwenye kampeni hiyo za kusaidia kununua madawati.
Uamuzi huo ulionesha jinsi gani michezo shuleni nchini haithaminiwi, imesahaulika kabisa huku ikiwa inaonekana haiwezi kumkomboa Mtanzania yeyote.
Michezo hii ambayo hukutanisha wachezaji waliochaguliwa kikanda kutoka shule mbalimbali nchini ilionekana kama haina matokeo chanya katika maendeleo ya michezo nchini. Hali hii ilifanya serikali kuisitisha.
Hali mbaya ya uendeshaji wa michezo hiyo ndiyo iliyofanya michezo hii kuonekana haina msaada katika Tanzania. Matatizo mengi yalikuwa yakiikabili michezo hiyo bila kupatiwa ufumbuzi hali tukitegemea matokeo chanya.
Uhaba wa walimu wa michezo ulisababisha shule nyingi za serikali zikose michezo. Kuna baadhi ya michezo kama vile mpira wa kikapu, mpira wa wavu, ambayo inahitaji walimu kwani ni ngumu kuchezwa majumbani, hali iliyosababisha kudorora kwa michezo hiyo na kuathiri hadi timu za taifa.
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kina shahada maalumu ya ualimu wa michezo lakini udahili wake ni mdogo na wahitimu wengi huishia kuajiriwa katika shule za binafsi, kwani serikali haijatilia mkazo michezo kama moja ya masomo muhimu kwenye mitaala.
Hali mbaya ya viwanja vingi vya michezo katika shule nyingi za msingi na sekondari nchini, pamoja na kuuzwa ama kuvamiwa kwa viwanja vya michezo vya shule hizo, ilisababisha wanafunzi kutokushiriki mchezo wowote.
Asilimia 90 ya shule za msingi na sekondari za serikali hazina viwanja vya michezo kama ya kikapu, wavu na mpira wa pete huku viwanja vichache vilivyopo vya mpira wa miguu vikiwa na hali mbaya.
Vyuo vikuu vina miundombinu ya michezo hiyo lakini hakuna wachezaji kutokana na kukosa misingi katika ngazi ya chini.
Mfano hakuna shule nchini zenye miundombinu ya kusaidia michezo kama kuogelea na Tennis, hali inayosababisha Tanzania kukosa uwakilishi katika mashindano ya kimataifa.
Baadhi pia ya shule zilizopo mijini na zile za kata hazina kabisa viwanja vya michezo kutokana na ufinyu wa maeneo yao.
Takwimu zinaonesha asilimia kubwa ya wanafunzi wanaofanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi ni wale wa shule za binafsi na za kimataifa zilizopo nchini.
Hii inatokana na ubora wa viwanja tofauti tofauti, walimu wa kutosha wa michezo, muda mwingi wa kucheza, pamoja na kuwa na afya bora.
FikraPevu inaona kwamba, serikali inatakiwa kutenga shule moja kila mkoa iwe kama shule kuu ya michezo.
Shule hiyo kuu ya michezo inatakiwa iwe na miundombinu yote kama vile mabwawa ya kuogelea, viwanja vya tennis, kikapu, wapu, ngumi, n a kadhalika pia shule hizi ziwe na makocha, ambao watakuwa wanafundisha wachezaji bora katika michezo mbalimbali waliotoka katika shule mbalimbali nchini.
Katika utawala wa awamu ya kwanza, michezo katika shule za serikali nchini ilikuwa ikipewa kipaumbele cha hali ya juu.
Itakumbukwa kwamba, Tanzania tuliweza kufanya vizuri katika michezo mbalimbali ikiwamo kunyakua medali za dhahabu katika riadha, huku timu ya taifa ya mpira wa miguu ikifanikiwa kushiriki katika michuao mikubwa ya Mataifa ya Afrika.
Hii yote ilichangiwa na jitihada serikali kuwaandaa wachezaji hawa tangu wakiwa shuleni.
Wanariadha kama Filbert Bayi, Juma Ikangaa, Gidamis Shahanga, Nzaeli Kyomo na wengine wengi wa enzi hizo walitokana na misingi ya michezo ya shuleni na wakaja kung’ara kimataifa.
Wengi walijitolea na walikuwa wamejezwa na uzalendo wa hali ya juu na haikushangaza wakati Nzaeli Kyomo alipopata ushindi huku akikimbia peku peku baada ya kuvua viatu akiona vinamchelewesha.
Mabondia kama Titus Simba, Habibu Kinyogoli, Willy Isangura na wengine, pamoja na kwamba wengi walitamba kwenye timu za majeshi, lakini mwanzo wao ulikuwa kwenye michezo hiyo ya shule za msingi na sekondari, ambapo shule kama Kibaha Sekondari na Tambaza zilikuwa na timu imara kiasi hicho.
Katika kipindi cha awamu ya tatu serikali ilifuta kabisa michezo mashuleni, uamuzi ambao ulitolewa na aliyekuwa Waziri wa Elimu wa wakati huo, Joseph Mungai.
Hali hii ikasababisha anguko kubwa la michezo nchini, na pamoja na kurudishwa tena baadaye, lakini hali ilikuwa mbaya huku ikionekana hakuna matunda wala msisimko.
Agizo lililotolewa hivi karibuni la kusoma masomo ya sayansi kwa lazima inaumiza sana wanafunzi wengine walio na vipaji au vipawa nje ya sayansi, mfano michezo.
Dunia ya sasa michezo ni moja ya sekta iliyoajiri watu wengi sana. Nchi zilizoendelea zinawekeza sana katika michezo kutokana na fursa zilizopo.
Leo hii Mwanasoka Bora wa Dunia, Cristiano Ronaldo, ambaye aliishia tu kupata elimu ya msingi, hafahamu chochote kuhusu sayansi, lakini ana maisha bora akiwa ameajiri watu wengi, yote hii ni kutokana tu na michezo.
Marekani wameweka utaratibu kwa mwanafunzi yeyote anapofanya vizuri katika michezo fulani na kufikisha kiwango kilichowekwa na serikali, hupata ufadhili wa masomo bure chuo kikuu huku akisajiliwa na baadhi ya timu kama mchezaji wa kulipwa.
Shule na vyuo vingi zina timu imara za michezo, hususan kikapu, mchezo unaoongoza nchini humo.
Hali hii hupelekea jitihada kubwa katika michezo miongoni mwa wanafunzi.
Moja ya wanufaika wa mpango huu ni Mtanzania Hashim Thabeet.
Tanzania tunaweza kuanzisha mfumo unaofanana na huu kuweza kuinua sekta ya michezo na tunatakiwa kuiona fursa hii na kuwekeza katika michezo kuanzia shule za msingi na sekondari.
Leo hii Tanzania tunatumia mabilioni kutangaza nchi yetu katika Ligi Kuu ya soka ya England. Wenzetu Kenya ambao wamewekeza sana katika michezo mashuleni hawatumii mabilioni kujitangaza kwani wana wachezaji waliotokea kwenye michezo ya shule za msingi na upili wanaocheza katika ligi hizo.
Wanariadha wa Kenya walioanzia mashuleni pia huitangaza nchi hiyo katika michuano mikubwa kama ya Olimpiki au mashinano ya dunia.
Tanzania inakosa sifa ya kushiriki baadhi ya michezo kwenye mashindano ya Olimpiki huku sababu ikiwa ni kukosa wachezaji wa michezo hiyo. Hakuna ya taifa ya michezo kama Rugby, Raga, Kriketi, Basketball,hali hii inaonesha jinsi gani sekta ya micheezo ilivyo na maelfu ya fursa za ajira hasa katika kipindi hiki ambacho kuna shida kubwa ya ukosefu wa ajira.
Shule ya Sekondari Mawenzi mkoani Kilimanjaro ina uwanja wa mchezo wa Raga pamoja na vifaa lakini hakuna mwanafunzi anayecheza mchezo huo kutokana na kukosa mwalimu wa kuwafundisha.
Kama serikali ingewekeza vya kutosha, leo hii shule hiyo ingekuwa kitovu cha mchezo huo na timu ya taifa ya mchezo huo nchini.
Shule nyingi za sekondari pia zina viwanja vya mchezo wa kikapu lakini kutokana na kutokuwa na walimu wa michezo husika tunajikuta tunakosa wachezaji mahiri na vipaji vingi kupotea.
Katika mfumo wa elimu ya juu, kuna tatizo kubwa katika sekta ya michezo. Vyuo vingi nchini vina miundombinu mizuri ya michezo mbalimbali, lakini tatizo kubwa ni kuwa hakuna chuo kinachotambua michezo kama sehemu ya mitaala.
Hii huwafanya wanafunzi wengi kuikimbia michezo na kujikuta wakikazania masomo tu ili kuweza kutafuta ufaulu.
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kina miundombinu mizuri ya michezo kama vile mabwawa ya kuogelea, viwanja vya michezo mbalimbali kama vile kikapu, mpira wa pete, tennis, na kadhalika, lakini hakuna wachezaji, hii ni kutokana na chuo hicho kutokutambua michezo kama sehemu ya kuongeza alama katika ufaulu.
Mfumo mzima wa elimu nchini kuanzia msingi hadi chuo kikuu unatakiwa kubadilika na kuingiza suala la michezo katika mitaala kwani ni moja ya sehemu yenye manufaa kwa wanafunzi na taifa kwa ujumla.
Kuna haja pia ya kutoa elimu kwa wazazi na kuwaeleza umuhimu wa michezo kwa mtoto, na pia kuwapa elimu jinsi gani michezo inaweza kutumika na kugeuka kuwa chanzo cha ajira kwa baadaye.
Wazazi wengi hukataza watoto wao kushiriki michezo kwa kutojua tu umuhimu wa michezo hiyo.
Jamii za wafugaji na wakulima zinatakiwa pia kupewa elimu ili waweze kuwapunguzia watoto kazi na kuwapa muda wa kutosha kushiriki katika michezo ili kuweza kuibua vipaji vya baadaye.