Kinondoni ni wilaya mojawapo iliyopo katikati ya jiji Dar es salaam, ambapo katika fikra za watu waishio pembozoni mwa nchi hudhani kuwa upatikanaji wa huduma za jamii ni bora zaidi kuliko maeneo mengine.
Lakini ni tofauti na mawazo ya watu hao, wilaya hiyo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa huduma ya maji ambayo imekuwa tatizo la kihistoria.
Huduma ya maji safi hutolewa na Mamlaka ya Maji ya Mjini Dar es Salaam (DAWASA) ambayo husambaza maji ya bomba kutoka katika vyanzo vya mto Ruvu. Pia maji ya visima ambayo hutolewa na miradi inayoendeshwa na Taasisi, Sekta binafsi na Jumuiya za watumia maji.
Wilaya ya Kinondoni ina visima 97 vinavyomilikiwa na Halmashauri na 301 vinavyomilikiwa na taasisi na watu binafsi. Licha ya kuwepo kwa maji ya bomba na ya visima bado hayakidhi mahitaji yote ya wananchi wa wilaya hiyo.
Hali ya Upatikanaji wa huduma ya Maji
Kulingana na Takwimu za Ofisi ya Manispaa ya Kinondoni (2016) inakadiliwa kuwa wilaya hiyo ina wakazi wasiopungua 929,681 lakini wanaopata huduma ya maji ni 660,074 ambao ni sawa na asilimia 73 ya wakazi wote.
Mahitaji halisi ya maji kwa siku katika Wilaya Kinondoni ni lita 74,374, 480 lakini maji yanayopatikana ni lita 54,293,370 ambapo ni upungufu unaofikia asilimia 27.
Maji ya DAWASA hupatikana kwa mgawo kati ya masaa 16 hadi 24 kwa wiki kutoka eneo moja hadi lingine ambapo uzalishaji wa maji katika mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini katika mto Ruvu uhudumia wakazi wa Dar es salaam na Pwani.
Miundombinu ya maji iliyopo imechakaa ambapo katika maeneo mengine mabomba yamepasuka kwa sababu maji hayajatoka muda mrefu. Hata hivyo, nyumba/kaya nyingi za wakazi wa Kinondoni hazijaunganishwa na mfumo wa maji.
Tathmini ya Hali ya watu na Afya ya mwaka 2010 (Demographic and Health Survey 2010); ni asilimia 4.8 tu ya kaya zilizopo vijijini ndiyo zinazopata maji katika eneo lao la kaya (water on premises) wakati ni asilimia 19.4 tu ya kaya kwa mijini ndizo zenye maji katika kaya zao
Hali hiyo huwalazimu wananchi wa Kinondoni kutumia maji ya visima ambayo siyo salama kwa afya zao kutokana na eneo kubwa la wilaya hiyo kukabiliwa na uchafuzi wa mazingira unaotokana na mfumo mbovu wa ukusaji wa taka ngumu na nyepesi za viwandani na makazi ya watu.
Maji ya visima yanatajwa na wataalamu kuwa sio salama sana kwa afya ya binadamu kwa sababu yana chumvi nyingi na vimelea vya wadudu ambavyo husababisha magonjwa kama vile kipindupindu.
Hili linathibitishwa na kauli ya Waziri wa Maji na Umwagilia, Mhandisi Gerson Lwenge wakati wa bunge la bajeti 2016/2017 alipoelezea kuhusu uchunguzi wa visima 108 ambapo visima 66 vilikuwa sio salama na maji yake yalikuwa na vimelea vya ugonjwa wa kipindupindu. Visima virefu vilikuwa 40 na vifupi ni 26.
Wataalamu wa maji wanashauri kuweka dawa katika maji ya visima ili kupunguza uwezekano wa watu kushambuliwa na magonjwa ya mlipuko. Chlorine ni miongoni mwa kemikali zinazoaminika sana katika sayansi ya kutibu maji yaani kuua vijidudu hatarishi vya magonjwa katika maji, lakini dawa hii hutumiwa kwa maelekezo ya wataalamu.
Utafiti wa Chuo Kikuu cha Ardhi, unaonesha maji ya visima vingi sio salama na kushauri wachimba visima kupata ushauri wa kitaalamu ili kuepusha jamii na magonjwa kwa kutumia maji yasiyokuwa salama.
Mipango ya Halmashauri kuboresha huduma ya maji
Katika mwaka wa fedha 2016/2017 wilaya ya Kinondoni imejipanga kupunguza tatizo la maji ambapo imeunda vyombo vya watumia maji ili wananchi waweze kusimamia na kuendesha miradi yao ya maji katika ngazi ya jamii. Kutoa elimu kwa umma kwa njia mbalimbali juu ya hifadhi ya mazingira na uendeshaji wa miradi ya Maji hususan ngazi ya Jamii.
Pia inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuweza kupata fedha na kutekeleza Miradi mikubwa ya maji ya kuwahudumia jamii. Kushirikisha Sekta binafsi katika uendelezaji na uendeshaji wa huduma ya maji katika ngazi zote.
Kukabiliana na tatizo la maji, DAWASA wanatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo upanuzi wa mitambo ya Ruvu Chini na Ruvu Juu kuongeza uzalishaji wa maji. Upanuzi na ukarabati wa mifumo ya kusambaza maji safi katika makazi ya watu.
Upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu kutoka uwezo wa sasa wa mita za ujazo 82,000 kwa siku hadi mita za ujazo 196,000 kwa siku ili kukidhi mahitaji ya maji ya wakazi wa Dar es salaam na Pwani hadi mwaka 2032.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda anasema "Lengo la serikali ni kumtua mama ndoo kichwani na kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi wote".
Takwimu za serikali zinaeleza kuwa hadi kufikia Machi mwaka huu, watu milioni 22.9 walikuwa wanapata maji safi ikilinganishwa na watu milioni 21 waliokuwa wakipata huduma hiyo hadi Juni 2016 nchi nzima, ikiwa ni ongezeko la watu zaidi ya milioni moja.
Watu milioni 663 duniani wanaishi bila kupata maji safi na salama. Nchi wahisani zimekubaliana kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) ifikapo 2030 hasa lengo 6 ambalo ni kuhakikisha watu wote wanapata maji safi na salama.