Ludewa: Karaha ya kwenda Mchuchuma na utajiri wa makaa ya mawe

Jamii Africa

MIAKA 21 iliyopita wakati Mbunge wa Ludewa wakati huo, Horace Kolimba, alipokuwa akipigia debe kuhusu makaa ya mawe Mchuchuma, hakuna aliyekuwa analifahamu eneo hilo isipokuwa wale tu kutoka Mkoa wa Iringa (sasa Mkoa wa Njombe), hususan wilayani Ludewa.

Lakini FikraPevu inatambua kwamba, kwa sasa eneo la Mchuchuma, au Nchuchuma kama wenyeji wa huko wanavyoliita, limekuwa maarufu hata nje ya mipaka ya Tanzania.

Hii inatokana na uwepo wa hazina ya madini aina ya makaa ya mawe kwenye eneo hilo lililopo ukanda wa kusini mwa Tanzania.

Mwamba wenye makaa ya mawe.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma na Hesabu za Serikali (POAC) Mh. Zitto Kabwe akitazama madini ya chuma huko Liganga wilayani Ludewa wakati alipotembelea mwaka 2012.

Huku ndiko ambako kuna mgodi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma ambao una hazina ya zaidi ya tani 536 milioni za makaa, wakati upande mwingine katika eneo la Liganga kunakadiriwa kuwa na hazina ya chuma ghafi kati ya tani 200 hadi 1,200 milioni, huku tani 45 milioni zikiwa zimethibitishwa katika uchimbaji.

Inakadiriwa kwamba tani milioni tatu za makaa zitachimbwa kila mwaka zikidumu kwa zaidi ya miaka 100 na tani milioni mbili za chuma zitachimbwa kila mwaka kwa zaidi ya miaka 90 baada ya kampuni ya Sichuan Hongda Group kutoka China kushinda zabuni na kusaini mkataba mwaka 2011 huku ikiahidi kuwekeza kiasi cha Dola 3 milioni.

Safari ya kufika Mchuchuma ikiwa unatokea Dar es Salaam ni ya kubahatisha, hasa ukifika Ludewa mjini. Yapo mabasi mawili, lakini kila siku mabasi haya yanapishana kwa kufanya safari kati ya Ludewa na Manda kupitia Nkomang’ombe ambako wengi tunapafahamu kama Mchuchuma.

Kama unatokea Dar es Salaam unapaswa kufika Njombe, ulale hapo, halafu asubuhi ndipo uanze safari ya kwenda Ludewa. Walau kutoka Njombe kwenda Ludewa kuna magari mawili kwa siku na yanaweza kuongezeka kutokana na ujenzi wa barabara unaoendelea.

FikraPevu iliwahi kuzuru eneo hilo, lakini changamoto ya usafiri ilikuwa kubwa mno.

Kondakta, ambaye alitambua kwamba mwandishi wa FikraPevu ni mgeni wa eneo alilokuwa anakwenda hivyo ‘kumpiga’ nauli ya juu kuliko kawaida, alisema kwamba gari lingeondoka saa 8:00 mchana, hivyo mwandishi akaenda sehemu walau kuituliza minyoo ya tumboni ambayo ilikuwa inagombana mno.

Naam. Hatimaye gari likawa limeenea, siti zote zimejaa abiria wakiwa wameketi watano watano katika siti zinazostahili kukaliwa na abiria wanne. FikraPevu ikaamini safari karibu itaanza. Lakini kondakta akaendelea kukatisha tikiti.

“Hawa wengine atawaweka wapi?” mwandishi wa FikraPevu akamuuliza abiria wa jirani.

“Wewe mgeni huku? Mbona bado abiria wa kusimama? Subiri utaona, wenyewe wanasema gari haijai, inajaa ndoo ya maji!” akanijibu.

“Askari wa usalama barabarani wanaliona hili?” akauliza tena.

“Hii yote ni Tanzania, ndugu yangu. Askari wote wanafanana, mwajiri wao ni mmoja na tabia zao zile zile – rushwa. Hakuna anayejali madhara ya baadaye. Wewe unakwenda Manda au wapi?” abiria huyo akamuuliza mwandishi wetu.

“Nakwenda Mchuchuma,” akamjibu.

“Tutashuka wote Nkomang’ombe.”

“Mimi nakwenda Mchuchuma…”

“Unakwenda Kijiji cha Mchuchuma au kule kwenye makaa?”

“Kwani tofauti ni nini?” mwandishi akamuuliza.

“Hata kama unakwenda kwenye Kijiji cha Mchuchuma, lazima ushuke Nkomang’ombe. Kama unakwenda kwenye makaa, utashuka hapo hapo Nkomang’ombe, ndiko watakakochimba makaa hayo.”

Kila aliyekatiwa tikiti aliondoka stendi kuu baada ya kupewa maelekezo na kondakta. “Kasubiri kule kule…” Ndivyo kondakta alivyowaelekeza.

Safari ilianza majira ya saa 8:30 huku gari likiwa limesimamisha abiria kama 10 hivi, mwandishi wetu akajua walau kwa idadi hiyo hali ilikuwa afadhali, hasa kwa kuzingatia shida ya usafiri wa kuelekea huko.

Kitu kingine ambacho kilikuwa cha ajabu ni wingi wa mizigo. Mbali ya gari kusheheni makreti ya bia na soda kwenye ‘carrier’, bado mizigo mingine – hasa viroba vya unga, sukari na bidhaa nyingine, iliwekwa chini ya siti, hivyo kufanya hata walioketi – hususan warefu – kuwa kama wameketi kwenye benchi la kahawa.

Wakati walipomaliza barabara ya lami na kutaka kuingia kwenye ile ya vumbi, yapata umbali wa nusu kilometa kutoka stendi kuu, gari likasimama. Mwandishi wa FikraPevu akashangaa kuona abiria wengi wakiwa wamesimama, wote wakiwa na tikiti zao mikononi.

“Nilikwambia, subiri utaona. Sasa hapa ndipo basi linapopakia abiria wa kusimama,” akasema jirani wa mwandishi wetu.

“He! Wote hawa?” mwandishi akauliza kwa mshangao, maana walikuwa wengi kuliko hata waliokuwa ndani ya gari.

“Ndio usafiri wetu. Una bahati umepata kiti, lakini hata hapa tulipoketi ni mateso tu!”

Abiria wale wakaanza kuingia, gari likajaa pomoni. Walioketi wakabananishwa mno na waliosimama. Hewa ikawa haitoshi na ghafla abiria mmoja akaanza kutapika. Punde na mwandishi wetu ‘akaungana’ naye, ikiwa ni mara yake ya pili kutapika safarini tangu alipotapika aliposafiri kwa meli miaka zaidi ya 20 iliyopita. Bahati yangu mwandishi wetu alikuwa dirishani, hivyo akafungua kioo na ‘kuirudisha chenji’ kupitia dirishani.

 

Gesti ya Shs. 2,000

Waliwasili Nkomang’ombe yapata saa 10:30 jioni, kijiji na kata ambayo eneo lake limechukuliwa kwa ajili ya uchimbaji wa makaa ya mawe ili kuzalisha umeme wa 600MW.

Mahali pa kuulaza ubavu ilikuwa changamoto ya kwanza, lakini mwandishi wa FikraPevu akafanikiwa kupata. Ipo gesti pekee hapo ambayo gharama yake ni Shs. 2,000 tu kwa usiku mmoja. Ni kama nyumba ya kawaida ya familia ambayo haiwezi kuitwa ‘gesti’. Usiulize mazingira ya ndani na nje.

Lakini maji ndiyo changamoto kubwa, kwani kwa siku mbili ambazo mwandishi wetu alala hapo hakuwahi kuoga. Maji ni shida kubwa kwa wakazi wa eneo hili, pengine na vijiji vingi nchini Tanzania. Hata hivyo, usingizi aliupata.

 

Kurudi kinyumenyume

Kama FikraPevu ilipata shida wakati wa kwenda, basi ilikuwa inajidanganya. Wakati wa kurudi Ludewa ndiyo ilikuwa mbinde. Gari pekee kutoka Manda ambalo hupita kijijini Nkomang’ombe saa 2:30 asubuhi, lilikuwa limejaa abiria kiasi kwamba kondakta alikaa kwenye ‘carrier’ pamoja na mizigo.

Kati ya abiria zaidi ya 10 waliokuwa wanasubiri, waliingia watano tu, wakiwa wananing’inia mlangoni. Mwandishi wetu akalazimika kubaki kwa siku hiyo.

Kwa bahati mbaya, miongoni mwa waliobaki alikuwepo mama aliyebeba mtoto mgonjwa akiwa anaharisha. Hakuwa na namna yoyote ya kwenda Ludewa kwa matibabu huku hali ya mtoto huyo ikiendelea kuwa mbaya.

Diwani wa zamani wa Kata hiyo ya Nkomang’ombe, Ananias Haule, akajitolea pikipiki yake kumbeba mama huyo ili kumwahisha Hospitali ya Wilaya ya Ludewa, yapata kilometa 35 kutoka hapo, ambako naambiwa alipofika tu mtoto akagundulika hana maji na upungufu wa damu. Akatundikiwa chupa mbili za maji kunusuru maisha yake.

“Hali ya usafiri ni mbaya sana hapa, kuna gari moja tu kila siku. Kama barabara ingekuwa nzuri naamini magari mengi yangeweza kuja na kuwanusuru wananchi na adha hii,” ndivyo alivyonieleza Haule.

Siku iliyofuata mwandishi wa FikraPevu akaamua kujibana hivyo hivyo kwenye ki-Hiace akiwa ameupinda mgongo kama anacheza pool table.

Ni bora kusimama kwenye gari huku safari ikiendelea kuliko kusimama kituoni ukisubiri usafiri usio na uhakika nao!

Yaliyowapata dakika kumi baadaye hayasimuliki. Gari liliishiwa mafuta wakati likijiaandaa kupandisha Mlima Kemilembe. Abiria wote wakateremka na kulisukuma ili kuligeuza kuelekea kwenye mteremko – walikotokea. Lilipowaka dereva akaliendesha kinyumenyume mpaka stendi ya kijiji hicho.

Mchakato wa kutafuta mafuta ukachukua saa mbili nzima. Wakapata dizeli kwa mfanyabiashara mmoja hapo, lakini gari ilipowashwa wakakimbia wakidhani gari inaungua. Ilitoa moshi mweusi mno na baadaye ikatulia kidogo. Haijulikani mafuta hayo yalikuwa dizeli au ya taa.

Uhakika wa safari ulikuwepo, lakini ulikwisha baada tu ya kufika mlimani. Gari likazimika ghafla. Kazi ya kulisukuma ikaanza upya. Ufinyu wa barabara uliwafanya watumie zaidi ya dakika arobaini kuligeuza gari kuelekea kwenye mteremko. Lilipowaka mwendo ukawa ule ule – kurudi kinyumenyume mpaka kuumaliza mlima huku abiria wakitembea. Lakini walifanikiwa kufika Ludewa, wakiwa wamechoka hoi kana kwamba walikuwa wanabeba vyuma.

Eais mstaafu Jakaya Kikwete alipotembelea eneo la Liganga wakati alipokuwa madarakani.

Naam. Huko ndiko Mchuchuma, kulikobeba matumaini makubwa ya Watanzania kufuatia uwekezaji wa uchimbaji wa makaa ya mawe yatakayozalisha umeme wa 600MW uchimbaji utakapoanza, ambapo 300MW zitaingizwa kwenye gridi ya taifa na nyingine zitatumika kuyeyusha chuma katika machimbo ya Liganga wilayani humo.

FikraPevu inafahamu kwamba, bei ya tani moja ya makaa, kwa mujibu wa Meneja Uhusiano wa NDC, Abel Ngapemba, inatarajiwa kuwa Dola 86.201 na mapato yatakayotokana na mauzo ya umeme yanakadiriwa kuwa Dola 285.981 milioni kwa mwaka wakati Dola 971.28 milioni zitazalishwa kwa mwaka kwa mauzo ya chuma, Dola 424.935 milioni katika mauzo ya titanium na Dola 114.125 milioni kwa mauzo ya vanadium.

 

Ujenzi wa barabara

Pengine adha hiyo itapungua sasa kwani tayari barabara zimeanza kujengwa ili kuboresha miundombinu katika wilaya hiyo na wilaya nyingine za Mkoa wa Njombe.

Kumbukumbu ambazo FikraPevu inazo zinaonyesha kwamba, wakati Mkoa wa Njombe unaanzishwa mwaka 2012 ulikuwa na jumla ya kilometa 6,403.45 za barabara ambazo zilikuwa zimegawanyika katika Halmashauri na TANROADS.

Halmashauri ya Mji wa Njombe ilikuwa na 1,315.3km, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe 848.8km, Halmashauri ya Wilaya Ludewa 963.43km, Halmashauri ya Wilaya Makete 767.8km, Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe 896.9km, Halmashauri ya Mji Makambako 484.8km na TANROADS ina jumla ya 1,123.42km.

Barabara zilizokuwa zinahudumiwa na Mfuko wa Barabara kwa mwaka wa fedha 2015/2016 ni jumla ya kilometa 970 ambapo kwa halmashauri ni 558km na TANROADS 412km.

FikraPevu inafahamu kwamba, wakati huo hakukuwa na barabara za lami katika Mamlaka za Serikali za Mitaa lakini kwa sasa tayari zimekwishaanza kujengwa.

Aidha, inaelezwa kwamba, barabara ya Itoni – Ludewa – Manda yenye urefu wa 211.4km ambayo inapitia Mchuchuma imefanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na Mhandisi Mshauri M/s Crown Tech Consult kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami.

Fedha za kuhudumia barabara zimeendelea kuongezeka ambapo Mwaka wa Fedha 2013/2014 jumla ya Shs. 16.7 bilioni zilipangwa kutumika mkoani Njombe ambapo Halmashauri zilitengewa Shs. 5.0 bilioni na Wakala wa Barabara (TANROADS) Shs. 11.7 bilioni.

Katika mwaka wa fedha 2014/2015 jumla ya Shs. 27.027 bilioni zitatumika ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 11 ukilinganisha na mwaka 2013/2014, ambapo Shs. 17 bilioni zilipangwa kutumika kwenye barabara kuu na za mikoa na Shs. 11 bilioni ni kwa ajili ya kuhudumia barabara zilizo chini ya Halimashauri.

Mwaka 2014, akiwa Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, alisisitiza makandarasi waliokuwa wakijenga barabara za kwenda Liganga kwenye machimbo ya chuma zikamilike ndani ya muda uliopangwa na kuheshimu matakwa ya Mkataba na kwamba kusiwepo na kisingizio cha kuwa wao ni wakandarasi wazalendo. 

Alisisitiza barabara hizo zikamilike mapema tayari kwa kupitisha mitambo yenye uzito wa tani 150 itayaosafirishwa kwenda Liganga. 

Hata hivyo, mpaka sasa miradi hiyo pacha bado haijaanza uzalishaji.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *