Mfumo sahihi unahitajika kuokoa sekta ya madini Tanzania

Jamii Africa

JUMATANO, Mei 24, 2017 Rais John Pombe Magufuli alipokea taarifa kutoka kwa Kamati ya Profesa Abdulkarim Mruma iliyokuwa inachunguza makanikia yaliyokuwemo katika makontena yaliyozuiliwa kwenye Bandari ya Dar es Salaam na bandari nyinginezo ambayo yalikuwa njiani kusafirishwa nje ya nchi.

Taarifa ya Kamati hiyo ilibaini uporaji unaofanywa na wawekezaji wa kibepari kwa kiwango cha hali ya juu na iliwasononesha na kuwashangaza watu wengi juu ya uporaji huo na kuzua mijadala mingi sehemu mbalimbali nchini.

 

Nipongeze jitihada alizozifanya Rais Magufuli kwa kutaka kufahamu ni kiasi gani hasa cha makanikia kinachosafirishwa kwenda nje ya nchi na kujua kiasi cha madini kinachopatikana kutokana na makanikia hayo.

Malori yakisomba mawe na mchanga wa dhahabu katika mgodi wa Buzwagi.

FikraPevu inaona kwamba, uporaji huu haukuanza jana wala juzi, na kwa muda mrefu unafanywa na mabepari tunaopenda kuwaita wawekezaji hali iliyochangiwa kwa kiasi kikubwa na mfumo mbovu unaolinda rasilimali zetu hapa Tanzania.

Tufahamu ya kuwa ubepari ni mfumo dhalimu na unahitaji mfumo imara kuweza kupambana na ujanja wa mabepari hasa katika kutafuta rasilimali duniani kote.

Kwa muda mrefu Tanzania imekuwa na mfumo dhaifu ulioruhusu mianya mingi ya wizi kufanywa na mabepari kwa ushirika wa Watanzania wenzetu ambao walipenda kujinufaisha wao wenyewe.

Rais John Magufuli akipokea Ripoti ya Kamati iliyokuwa ikichunguza makanikia kutoka kwa mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Abdulkarim Mruma (kushoto) Jumatano, Mei 24, 2017.

Katika makala zangu mbalimbali ndani ya FikraPevu nilipenda kusisitiza ya kuwa uwekezaji Tanzania ni uporaji wa rasilimali za wavuja jasho wanyonge ambao huvuja jasho jingi na kuwafaidisha wawekezaji wachache. Madhara mengi tumeona katika sekta ya madini, ardhi, kilimo na kwingineko.

Wizi huu uliotanabaishwa na taarifa ya Kamati ya Profesa Mruma hautoaishia hapa, unaweza kuendelea tena kwa nguvu kama mfumo wetu utabaki kuwa dhaifu kiasi hiki.

Kuwawajibisha wahusika katika idara muhimu ni moja ya namna ya kupambana na tatizo lakini siyo suluhisho la kudumu kama mifumo yetu itaendelea kuwa dhaifu kwani tutafukuza watu kila siku na wizi utaendelea kushamiri.

Ni imani yangu ya kuwa kwa utajiri tulionao Tanzania hatuhitaji wawekezaji katika kila kitu na pale inapobidi kuwa na wawekezaji ni vyema basi serikali ikawa mbia mkuu katika uvunaji wa rasilimali na siyo kujiweka pembeni na kusubiri kodi kutoka kwa wawekezaji hao.

Mifano kutoka nchi zingine za Afrika inaonyesha nchi zilizoweka mifumo imara zinafanikiwa katika madini.

Botswana ni mojawapo ya nchi za Afrika zenye utajiri mkubwa wa almasi ambayo imeifanya nchi hiyo kupiga hatua kubwa ya maendeleo.

Madini ya vito aina ta Tanzanite

Moja ya njia bora walizotumia Botswana ni pamoja na serikali kuwa mmoja wa wamiliki katika uchimbaji wa madini, serikali haijakubali mwekezaji ahodhi umiliki wa madini bali yenyewe ni sehemu ya umiliki wa migodi hiyo.

Kwa ufupi nitajaribu kueleza mifumo ya kuimarisha ili tuweze kunufaika na madini yetu na kuzuia wizi wa hali ya juu tunaoendelea kuushuhudia hadi leo hii.

Sekta ya madini ni lazima iwe chini ya umiliki wa serikali (State Ownership), hii haimaanishi serikali kumiliki madini tu bali pia itajihusisha na uchimbaji moja kwa moja.

Endapo mwekezaji atakuja kutaka kuwekeza katika sekta ya madini atafanya kazi na serikali na mwekezaji kutoka nje atakuwa mbia wa serikali. Huu ni mfumo imara utakaoweza kuzuia wizi lakini pia utawapa imani Watanzania ya kuwa mali yao iko chini ya serikali na itawafaidisha.

Umiliki wa sekta ya madini na serikali si tu utadhibiti wizi, lakini pia utaleta hali ya umiliki kwa wananchi na watenda kazi katika sekta hiyo.

Kwa sasa hali ilivyo watenda kazi wengi wamekuwa hawana uchungu na mali yao kwani wamekuwa wakiamini madini yameshauzwa kwa wawekezaji ambao wao wanajichukulia chao na hivyo wanaona ni fursa kwao kuiba kwa manufaa yao na familia zao.

Mfumo wa pili ni uwazi wa taarifa zote za sekta ya madini kuanzia mikataba inayosainiwa, mapato na matumizi kwa Watanzania. Kwa muda mrefu Tanzania imekosa uwazi katika sekta hii ya madini na kufanya watu kushindwa kuelewa wananufaikaje na madini yao.

Wachimbaji wadogo wakitafuta dhahabu.

Hali hii ya sintofahamu imesababisha kuwa na migogoro isiyokwisha katika migodi ya North Mara, Buzwagi, Bulyanhulu, Geita, Mererani, Mtwara na Lindi kwenye mafuta na gesi ambako watu wengi wanaishi katika umaskini wa kutupwa ilihali wamezungukwa na migodi mikubwa yenye utajiri wa hali ya juu.

Ushirikishwaji wa wananchi katika sekta ya madini (Governance in Mining) ni sehemu nyingine muhimu katika sekta hii ya madini.

Mara nyingi tunashuhudia kuwepo kwa ushirikishwaji hafifu au kutokuwepo na ushirikishwaji kabisa kwani maamuzi mengi hufanyika kutoka juu kwenda chini badala ya kutoka chini kwenda juu.

Hii imedhihirika hasa katika kugawa maeneo ya uchimbaji kwa wawekezaji ambapo watu wamekuwa wakifukuzwa kila kukicha kwenye maeneo yao ili kumpisha mwekezaji.

Jambo hili limeleta migogoro mingi kwani watu hawakushirikishwa katika jambo hili bali maamuzi yalifanyika hotelini, mkataba ukasainiwa chumbani mwekezaji akaja.

Nimalize kwa kusema, rasilimali zetu tutazifurahia kwa kuwa na mifumo imara ambayo itawaongoza na kuwaruhusu watu kutenda vyema kwa uadilifu na kuzingatia mfumo imara uliopo.

Moja ya mfumo imara kwa maoni yangu ni kurudisha rasilimali zote ziwe chini ya umiliki wa serikali na serikali iwe sehemu mojawapo ya wazalishaji ndipo tutakapoona faida ya rasilimali zetu badala ya serikali kuwa mkusanyaji kodi mkuu na mwekezaji kuchuma rasilimali zetu kwa uhuru atakao.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *