China yaendelea kuneemeka kwa rasilimali za Tanzania, yasahau miradi ya mabadiliko ya hali ya hewa

Jamii Africa

Licha ya China kuwekeza mtaji mkubwa katika miradi ya maendeleo katika nchi za Afrika ikiwemo Tanzania, imebainika kuwa nchi hiyo ina mchango mdogo katika mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa na kuiweka Afrika katika hatari ya kukosa chakula.

Inaelezwa kuwa mwaka 2017 China ilikuwa inaongoza kwa utoaji wa hewa ukaa na kuchangia asilimia 23 mpaka 26 ya hewa ukaa yote inayotengenezwa duniani, huku bara la Afrika likichangia asilimia 3.8.  Takwimu hizo zinaiweka China na Marekani miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa uchafuzi wa hewa duniani na kutatiza shughuli za kiuchumi ikiwemo kilimo.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron alipotembelea China mwaka jana aliitaka China kushirikiana na wadau wengine kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa huku ikitekeleza miradi ya maendeleo katika nchi za Afrika.

Hatua hiyo ya Ufaransa inatokana na China kuwa muwekezaji mkubwa  katika nchi za Afrika ambako hujipatia faida kutokana na mafungamano ya kibiashara yaliyopo, hivyo lazima ihusike kwenye mikakati ya kulinda mazingira na kuifanya dunia kuwa sehemu salama ya kuishi.

Licha ya kuchangia asilimia ndogo kwenye joto la dunia na mabadiliko ya tabia nchi, bara la Afrika linabaki katika hatari ya kuathirika zaidi na mabadiliko ya tabia nchi ikizingatiwa kuwa wakazi wengi wa bara hilo wanategemea kilimo ambacho hutegemea mvua za msimu.

Umuhimu wa China kushiriki katika harakati za kupambana na matokeo ya mabadiliko ya tabia nchi yanajitokeza katika sura nyingine ambapo China inatengeneza hewa ukaa nyingi na kusambaa katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Wataalamu wa hali ya hewa na maendeleo wanaamini kuwa Afrika iko kwenye muelekeo mzuri wa kufikia malengo yake, ambapo imetekeleza mkataba wa Paris wa mwaka 2015 juu ya utunzaji wa mazingira kwa asilimia 70 lakini inakwamishwa na uchafuzi wa hewa na uwekezaji ambao hauzingatii utunzaji wa mazingira na uoto wa asili.

Changamoto iliyopo ni kupungua kwa usalama wa chakula na ongezeko la idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa ambapo idadi hiyo imeongezeka kutoka watu milioni 220 hadi milioni 224 mwaka uliopita. Uzalishaji wa mazao katika nchi za Afrika hutegemea mvua za msimu ambazo zinaathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo shughuli za viwanda na ukataji miti.

 

Akihojiwa na jalida la Quartz, Mratibu wa Umoja wa Mataifa kitengo cha Mabadiliko ya Hali ya hewa, Richard Munang amesema, “ Sekta ya kilimo iko kwenye hatari kwasababu inachangia asilimia 65 ya nguvu kazi yote Afrika. Inatia moyo kwamba bara hilo linashughulikia athari za mabadiliko ya hali ya hewa”.

“Haki zetu za msingi hazijadiliwi, kutokana kwamba mabadiliko ya hali ya hewa yanatishia usalama wa chakula”, amesema.

Mapitio ya Shirika la Chakula Duniani (ILO-2017) yanaonyesha kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yaliyotokea mwaka uliopita yamesababisha kupungua kwa mavuno, kupotea kwa mifugo na kuongezeka kwa ukame.

Hata hivyo, Tanzania ilipata mavuno mengi ukilinganisha na miaka iliyopita kwasababu ya kupata mvua za kutosha na juhudi za serikali kuwahimiza wananchi kutunza mazingira kwa maendeleo endelevu.

Usalama wa chakula hutokea ikiwa watu wote, wakati wote wanapata chakula kukidhi mahitaji ya mlo kamili. Wataalamu wanasema ili nchi ihesabike ina usalama wa chakula lazima ijumuishe mambo matatu; upatikanaji, matumizi na uwepo wa chakula cha kutosha

Mauritania, Afrika Kusini, Ghana, Namibia na Senegal zinatajwa kuwa miongoni mwa nchi 10 zenye usalama wa chakula barani Afrika kutokana na uwekezaji mzuri wa mbegu, mbolea na teknolojia ya kisasa inayotoa mazao mengi na uhakika wa soko.

Pia usalama wa chakula kwa nchi husika hutegemea utashi wa kisiasa, umakini wa serikali na mikakati ya kitaifa juu ya sekta ya kilimo na chakula. Inaelezwa kuwa Tanzania ina hali nzuri ya chakula ukilinganisha na nchi zingine za Afrika Mashariki ikiwemo Burundi na Sudan Kusini ambazo ziko kwenye kundi la nchi 10 ambazo hazina usalama wa chakula.

Mathalani, wakulima wa  Ethiopia wamefanikiwa kuongeza mavuno ya ngano kwa asilimia 14 kutokana na matumizi ya teknolojia ya kisasa, huku wakulima wa Rwanda kwa mwaka 2017 walijihusisha katika matumizi ya kilimo cha umwagiliaji ambacho kinaendeshwa kwa  teknolojia ya umeme wa jua.

Kenya pia walitumia zaidi teknoloji ya kuongeza rutuba ya udongo na kujikuta wakipata mavuno mengi. Tanzania imeanzisha mfumo wa stakabadhi ghalani ambao unawawezesha wakulima kupata dhana za uzalishaji za kilimo na ujuzi wa jinsi ya kuongeza mavuno na wanatakiwa kulipa baada ya kupata mavuno.

Hata hivyo, sekta ya kilimo inatishiwa na ongezeko la hewa ukaa inayozalishwa na nchi zilizoendelea kiviwanda ikiwemo China ambayo ina mafungamano ya karibu na nchi za Afrika. Ili kuiwezesha China kufaidika zaidi na rasilimali za Afrika imeshauriwa kuwekeza katika miradi ya utunzaji wa mazingira na kupambana na mabadiliko hasi ya hali ya hewa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *