Kilimo ni sekta ya uzalishaji ambayo huchangia kukuza pato na kuimarisha uchumi la taifa. Tanzania ikiwa ni nchi inayotegemea kilimo kama uti wa mgongo wa uchumi wake, mipango na mikakati mbalimbali imetekelezwa na serikali ikishirikisha wadau wa maendeleo kuboresha kilimo ili kiwe cha manufaa.
Changamoto iliyopo sasa ni kupata teknolojia na nguvukazi ya kuendeleza rasilimali za nchi na kutengeneza mazingira mazuri ya kukuza kilimo nchini. Nguvu kazi ya kilimo kwa sehemu inaathiriwa ugonjwa wa UKIMWI ambao haujapata dawa wala kinga. Idadi kubwa wanaoathirika na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI ni vijana na wanawake ambapo hali hiyo huathiri ukuaji wa sekta ya kilimo nchini
Kulingana na Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi Tanzania (THIS) ya mwaka 2016/2017 unaonyesha vijana wenye umri wa miaka 15-24 wanapata maambuki ya ugonjwa huo kwa asilimia 1.4, kwa wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 64 maambukizi hayo yako juu kwa asilimia 6.5.
Kutokana na maambukizi hayo mapya, uwezekano wa nguvu kazi kwenye ya kilimo ikapungua hasa kwa wanawake ambao wanachangaia asilimia 43 ya nguvu kazi katika sekta hiyo.
Maambukizi ya Viruzi vya UKIMWI yanavyoathiri kilimo
Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Sayansi ya Kijamii ya Afrika Mashariki na Kusini (OSSREA) mwaka 2012 unaeleza maambukizi ya VVU katika mikoa ya Mbeya, Lindi, Kigoma, Morogoro, Tabora na Kagera yamechangia kwa sehemu kubwa kurudisha nyuma maendeleo ya kilimo Tanzania.
Prof. Honest Ngowi ambaye alishiriki katikia utafiti huo anasema matokeo makuu yanaonyesha kwamba janga la VVU/UKIMWI linaathiri sekta ya kilimo katika mikoa iliyochunguzwa kwa namna mbalimbali, “ Namna mojawapo ni upotevu wa nguvukazi mashuhuli, zalishi na yenye nguvu moja kwa moja au namna isiyo ya moja kwa moja ambayo hutokea mda mfupi na mrefu”.
Anasemaa kuwa nguvukazi inapotea kwa njia ya maradhi na hatimaye vifo; muda unaotumika katika kutoa huduma na msaada na kuhudhuria misiba. Pia watu wanaokimbia makwao kutokana na unyanyapaa na ubaguzi na kuepuka kuwahudumia wagonjwa, yatima na wajane
Utafiti huo uliolenga kutafuta njia ya kukuza nguvu kazi ya taifa kwenye kilimo unaeleza kuwa athari nyingine ni mazao pungufu kutokana kupungua kwa eneo linalolimwa na mifugo. Pamoja na mambo mengine, ukosefu wa rasilimali watu, fedha na halisi za kutosha kutumia ardhi iliyopo kwa ajili ya kilimo kwa sababu ardhi hutumiwa zaidi kwa mazishi kwa kuwa idadi ya vifo inaongezeka kila mwaka.
Kupungua kwa mifugo ni matokeo ya wananchi kuuza mazao ili kulipia gharama za matibabu, matunzo na msaada kwa ndugu walio na maambukizi ya VVU au ugonjwa wa UKIMWI. Hali hii hupunguza uzalishaji hasa katika jamiii za wafugaji ambao hutegemea machungo kwa kutembea umbali mrefu kutafuta marisho na maji kwa ajili ya mifugo.
Ukataji wa Miti
Miongoni mwa athari za mda mrefu ni mabadiliko ya hali ya hewa na mazingira. Kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya majeneza yaliyotengenezwa kwa miti, miti mingi zaidi bado inakatwa kutoa malighafi kwa utengenezaji wa majeneza.
Utafiti huo unabainisha kuwa athari za mda mrefu na haziwezi kuonekana mapema lakini hali hii ikiendelea bila kuthibitiwa mapema kwa namna nzuri inaweza kusababisha uharibifu wa mazingira ambao kwa upande wake utaathiri mazao katika sekta ya kilimo kwa sababu kilimo cha Tanzania kinategemea zaidi mvua ambayo inaathiriwa na ukataji wa miti na maendeleo ya viwanda duniani.
Njia Mahususi kuongeza tija
Prof. Ngowi anaendelea kusema njia mahususi zinahitajika kupunguza athari hasi za VVU na UKIMWI katika sekta ya kilimo ni kupunguza athari ya muda unaotumiwa na nguvukazi ya kilimo kwenye masuala yanayohusiana na UKIMWI. badala ya kutumia muda huo kwenye kilimo, kuna haja ya kuwa na watu wenye ujuzi maalumu wanaotoa huduma ambazo zinatolewa na wakulima wadogowadogo.
“Kwa mfano, watoa huduma za matunzo wenye ujuzi maalumu walioajiriwa majumbani wanapaswa kuchukua nafasi ya wakulima wanaotoa huduma kwa msingi wa kujitolea’, ameshauri.
Anapendekezwa kwamba kadri inavyowezekana shughuli zinazolenga kushughulikia masuala mbalimbali ya VVU zinapaswa kutekelezwa wakati zinapokuwa athari hasi ndogo kabisa kwenye sekta ya kilimo, kwa mfano, katika njia muhimu za shughuli za UKIMWI kama vile semina na maonyesho ya kuigiza zinapaswa kuepukwa kadri inavyowezekana.
Watu wanashauriwa kuzika maiti kwenye ardhi ya uzalishaji mdogo wa mazao na kuepuka kutumia nafasi kubwa kupita kiasi cha makaburi. Lakini kutokana na utakatifu wa suala lenyewe la kuzika wafu katika jamii nyingi za Tanzania, inatambuliwa wazi kwamba katika kuzika mwili kinachofanyika kwanza ni kuipa heshima kubwa ikiwa ni pamoja na kuzika katika ardhi nzuri ya kilimo katika uwanja wa kaya kama inavyotumiwa zaidi na wakazi wa Kilimanjaro na Bukoba.
Anaeleza kuwa kiasi cha nguvukazi kinachaoathiriwa na janga hili kinapaswa kidhibitiwe kuongeza juhudi za kusambaza dawa za kurefusha maisha kwa waathirika ili kupunguza athari katika sekta ya kilimo na kupata watu ambao watanufaika na uzalishaji wa mazao.
Athari za Kisaikolojia
Imegundulika kuwa watu walio na maambukizi ya VVU pia hupata athari za kisaikolojia na hivyo kushindwa kufanya shughuli nyingine za uzalishaji. Juhudi za wataalamu wa kutoa ushauri na nasaha zinapaswa kuongezwa ili kuwaelimisha watu kuwa UKIMWI sio mwisho wa maisha na mtu anaweza kuendelea na shughuli za kilimo ambacho kitamuingizia kipato na kuimarisha afya yake.
Wakati wote tumekuwa tukisikia viongozi na wadau wa afya wakitaja athari hasi za Ukimwi lakini upande wa pili kuna athari chanya ambazo zinahitaji ulinganifu ili kuleta matokeo yaliyo na tija katika maendeleo ya taifa.
“Athari chanya zinaweza kutokea kwa njia ya uwekezaji wa mapato yanayotokana na sekta ya kilimo. Katika muktadha
wa mambo kujizidisha, sehemu ya mapato kutokana na ushiriki katika shughuli za VVU na UKIMWI, kama zilivyo aina nyingine za mapato zinatumiwa katika kununua mazao mbalimbali ya kilimo hasa chakula kutegemea muelekeo alionao mtu. Wanaopata mapato kwa njia hii huwa soko kwa wale wanaozalisha katika sekta ya kilimo na hivyo kuchangia ukuaji wa sekta hii”, anaeleza Prof. Ngowi katika utafiti huo.
Pia athari chanya za moja kwa moja huwa kitega uchumi katika uzalishaji wa mazao ya chakula yanayohitajika kama lishe maalumu kwa waathirika wa VVU. Zinaweza kuwa kitega uchumi kwa malengo ya kibiashara katika kilimo cha mimea inayoweza ikawa na ubora wa lishe au dawa katika muktadha wa tiba ya UKIMWI.
Nguvu ya pamoja baina ya wadua wote wa kilimo na masuala ya jamii ili kuwa na takwimu za kutosha katika kupima ukuaji wa kilimo nchini kwa kuwa athari za Ukimwi huwakumba wakulima ambao idadi yao ni kubwa katika nchi na wanategemewa kuzalisha mazao kwa ajili ya viwanda, chakula na matumizi mengine.
Watunga sera hawana budi kuitazama sekta ya kilimo kwa mtazamo mpana ili kukabiliana na changamoto za janga la UKIMWI ambazo zinaligharimu taifa rasilimali nyingi. Kazi hii sio ya watunga sera pekee bali ni ya kila mwananchi kutazama
mabadiliko yaliyoletwa na janga hili katika kilimo na kuchukua hatua stahiki.