KATIKA kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika, Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), limesema taifa limepoteza dhana ya uwajibikaji, uzalendo safi na mtazamo chanya wa maendeleo na ustawi wa wananchi, badala yake nchi imetumbukia kwenye vilema vya kifisadi na ubinafsi uliopindukia.
Kana kwamba hiyo haitoshi, TEC imeonya kwamba, kushamiri kwa matabaka ya watu wenye nacho na wasionacho, mmomonyoko wa maadili, ushabiki wa mambo usio na upeo wala kina, unahatarisha usalama na mshikamano mzuri wa nchi ulioachwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Kauli hiyo imetolewa Jijini Mwanza na Rais wa Baraza hilo la Maaskofu Tanzania, Jude Thadaeus Ruwa’ichi, wakati alipokuwa akizungumza kwenye uzinduzi wa kitabu cha Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, uliofanyika Mwanza hoteli.
Ruwa’ichi ambaye pia ni Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mwanza, alikwenda mbali zaidi na kusema, Serikali inapaswa ijitathmini na kutoogopa kuchukuwa maamuzi magumu ambayo ni muhimu, kama ambavyo Baba wa Taifa, Nyerere alivyojiwekea wakati wa kutafuta na baada ya kupata uhuru Desemba 9, mwaka 1961.
Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Jude Thaddaeus Ruwa’ichi (kushoto), akimpongeza mtunzi wa Kitabu cha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, John Kasembo (katikati), jana Mwanza Hoteli. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza, Said Ali Amanzi.
Askofu Ruwa’ichi akisikiliza hotuba ya DC Amanzi.
“Leo tunaposherehekea miaka 50 ya uhuru wa nchi yetu, yapo matatizo mengi yanayotupasa tujitafakari. Taifa letu limesakamwa na vilema vya kutisha vya ufisadi mkubwa na mdogo.
“Dhana ya uwajibikaji na uzalendo safi vinaonekana kuanza kutoweka. Kuzuka kwa matabaka na hata yale ya ulaghai na kushamiri kwa umasikini unatishia na kuhatarisha amani na umoja wa taifa letu”, alisema Ruwa’ichi.
Hata hivyo, kiongozi huyo wa kiroho ambaye alitoa hotuba yake hiyo kali mbele ya Kaimu Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Said Amanzi alisema, Watanzania wote wanapaswa kuielewa miaka 50 ya Uhuru wa nchi kama ngwe ndogo, katika safari ndefu ya kujiimarisha na tunu ya kimaendeleo.
Kwa mujibu wa Rais huyo wa TEC, kila Mtanzania anao wajibu wa kuwa mchangiaji mzuri wa maendeleo ya taifa, na kwamba lazima uwepo utawala wa haki na bora, umoja, uswa na utamaduni unaozingatia maslahi ya watu wote na si kundi fulani.
“Kila mmoja wetu anatakiwa awe mchangiaji hodari wa maendeleo ya taifa letu hili. amani, utawala wa haki na usawa lazima vizingatiwe”, alisema Ruwa’ichi ambaye katika hotuba yake ilionekana kuwaliza baadhi ya watu ukumbini humo.
Aidha, alitumia fursa hiyo kumpongeza mtunzi wa kitabu hicho cha Miaka 50 ya uhuru wa Tanzania Bara, John Kasembo (26), kwa kuandaa kitabu hicho chenye maudhui ya taifa hili lilikotoka, lilipo na linakoelekea.
“Kwa niaba ya watu wote wenye mapenzi mema, nakupongeza kwa moyo wote kijana John Kasembo na nakukaribisha sana katika ulingo wa watafiti mahiri na waandishi bora”, alisema Ruwa’ichi kisha kushangiliwa na umati uliohudhuria uzinduzi wa kitabu hicho.
Naye Kaimu Mkuu wa mkoa wa Mwanza, ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Nyamagana na Kaimu Mkuu wa wilaya ya Ilemela jijini hapa, Said Amanzi katika hotuba yake alikiri taifa kukumbwa na matendo mabaya ya kifisadi.