MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza, wamehoji matumizi mabaya ya zaidi ya sh. milioni 73.62 za Mifuko ya Majimbo ya Sumve na Kwimba, ambapo wamedai fedha hizo huenda ‘zimechakachuliwa’ na kushindwa kutekeleza miradi ya maendeleo wilayani hapa kama inavyotakiwa.
Kufuatia hali hiyo, Diwani wa Kata ya Hungumalwa, Shija Malando (CCM), ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari, alisema kama angelikuwa na uwezo angeagiza kukamatwa na kuwekwa ndani Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, kutokana na kile alichokiita kushindwa kubainisha wazi matumizi ya fedha hizo na miradi yake ya maendeleo iliyotekelezwa.
Wakizungumza kwa jazba jana kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani, kilichoketi chini ya uenyekiti wake, Zephania Masangu, madiwani hao walieleza kushtushwa na matumizi ya fedha hizo za mifuko ya majimbo, na kusema hakuna miradi iliyoteklezwa kupitia fedha hizo, lakini fedha hizo zimeoneshwa kwenye makablasha ya halmashauri kwamba zimetumika zote.
Diwani wa Kata ya Hungumalwa, Shija Malando akizungumza jana kwa jazba kwenye baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, juu ya madai ya kuchakachuliwa sh. milioni 73.62.
Diwani wa Kata ya Lyoma, Julius Samamba, ndiye aliyeibua hoja hiyo ambapo aliuliza ni miradi ipi ya maendeleo imetekelezwa kupitia fedha hizo za mifuko ya majimbo ya Sumve na Kwimba ambazo ujumla wake ni sh. 73,623,000, na kusema anamashaka huenda fedha hizo zimetumika vibaya kuliko malengo halisi.
“Mheshimiwa mwenyekiti, kwenye kablasha hili tunaambiwa sh. milioni 73,623,000 zimetumika zote kwenye miradi, bila mchanganuo wa miradi husika. Hivi ni miradi ipi imetumika kwa fedha hizi?.
“Hapa tunataka majibu kutoka kwa Mkurugenzi, hizi fedha zipo wapi?. Kwa nini wanatuambia zimetumika bila kuainisha michanganuo ya miradi yenyewe?”, alihoji Diwani Samamba, ambapo alionekana kama amemwagia petroli kwenye moto baada ya madiwani wengine kuchachamaa na kuanza kuhoji.
Katika kikao hicho kilichoanza majira ya saa 6 mchana na kumalizika saa 2:08 usiku, madiwani wengi waliijia juu ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo, huku wengine wakitaka fedha hizo zirudishwe haraka ili zipangiwe matumizi yanayoeleweka katika miradi ya maendeleo, kwa lengo la kutatua kero nyingi zinazowakabili wananchi wa wilaya hiyo kongwe.
Diwani wa Kata ya Hungumalwa, Shija Malando aliinuka na kusema: “Hizi fedha inaonekana zimetumika ovyo hovyo. Mkurugenzi tunataka majibu sahihi, ulishindwa nini kumwambia Ofisa Mipango atoe mchanganuo wa miradi iliyotekelezwa kwa fedha hizi?.
Diwani huyo machachari wa Hungumalwa, Malando alisema, bila majibu ya kuridhisha kuanzia juzi, madiwani hawatakuwa na imani na Mkurugenzi wao (Shaban Ntarambe), na kwamba kama angelikuwa na uwezo angeagiza akamatwe na kuwekwa ndani, jambo ambalo madiwani wengine, watendaji pamoja na wananchi waliohudhuria kikao hicho walijikuta wakiangua kicheko, kabla ya diwani huyo kufuta kauli yake hiyo ya kukamatwa na kuwekwa ndani kiongozi huyo.
“Bila kutupa majibu mazuri kwa fedha hizi Mkurugenzi, kuanzia leo hatutakuwa na imani na wewe. Na kama ningekuwa na uwezo ningeagiza kamata weka ndani huyu mtu”, alisema Diwani Malando kisha ukumbi mzima ukalindima vicheko ambapo mwenyekiti Masangu alimtaka diwani huyo kufuta kauli yake hiyo, ambapo aliifuta huku akiendelea kulalamikia matumizi mabaya hayo ya fedha za mifuko ya majimbo.
Kwa upande wao, Diwani wa Kata ya Mwakilyambiti, Budila Luduka (CCM), na diwani wa viti maalumu kata ya Ngula, Ester Soboka (CCM), walilalamikia matumizi mabaya hayo ya fedha na kwamba, hakuna miradi iliyotekelezwa kupitia fedha hizo za mfuko wa majimbo zilizotolewa mwaka 2010/2011, lakini Mkurugenzi Ntarambe alijitetea kwa kusema kwamba fedha hizo zimetumika vema katika kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo, na wala fedha hizo si zake binafsi.
Hata hivyo, baada ya vuta nikuvute hiyo, mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo ya Kwimba, Masangu alitoa ushauri kwa madiwani akitaka fedha hizo zirudishwe kwenye akaunti na zipangiwe utaratibu mzuri wa matumizi ya miradi ya maendeleo, jambo ambalo lilikubaliwa na madiwani wote hivyo kuwa azimio la kikao hicho cha baraza la madiwani wa Kwimba.
Habari hii imendikwa na Sitta Tumma – Mwanza
hakika tatizo la rushwa kwenye jamii zetu bado ni kubwa.
Swala ili lina mizizi miefu ndani ya jamii,na kwakua viongozi wetu wanaendekeza sarakasi hizi za kiasa..uku wakiacha mambo yajiendeshe yenyewe..tutasikia mengi na kuona mengi lakini dhana ya uwajibikaji kwa maana halisi haitatekelezwa.hali hii ni janga lingine kitaifa.