Maji ya mto huu yana sumu

Albano Midelo

WANANCHI zaidi ya 25,000 wa vijiji 16 vya kata za Tingi na Liparamba katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wapo  hatarini  kukumbwa na magonjwa na hata kupoteza maisha kwa  kunywa maji yenye sumu.

Hao ni wale wanaotumia maji ya mto Lunyere. Humu yanatiririkia  maji yanayotoka migodi midogo ambamo wachimbaji wanaosha dhahabu kwa kutumia zebaki (mercury), ambayo ni kemikali yenye sumu kwa binadamu na viumbehai vingine.

Getruda Payovera afisa maabara Wizara ya Maji, ofisi za kanda ya Songea, ameeleza kuwa zebaki ikinywewa kwenye maji au kunuswa, yaweza kuingia moja kwa moja kwenye damu na “…inakwenda  kutua kwenye ubongo na kusababisha ubongo kusimama…”

Maji ya mto Lunyere, kutoka kitongoji cha Songeapori, yaliyopelekwa Dar es Salaam kati mwaka 2009, na kufanyiwa uchunguzi na taasisi za Water Laboratory Unity na  Chemical and Envromental Service za jijini Dar es salaam, yaligundulika kuwa na “kiwango kikubwa na cha kutisha” cha kemikali ya zebaki.

Alieleza kwa njia ya kitaalam kuwa kiwango cha zebaki kilichokutwa kwenye maji ya Lunyere ni Hg/ug 0.02 ambacho alisema “ni kingi na cha kutisha.” Tayari wataalam wameamua kuwa maji ya Lunyere hayafai kwa matumizi ya binadamu na viumbe hai.

Maji ya mto Lunyere ambao unaanzia nchini Msumbiji na kuingia nchini Tanzania kupitia kata za Tingi na Liparamba wilayani Mbinga mkoani Ruvuma  maji yake  yana sumu mbalimbali ambazo zinaweza kuleta madhara makubwa kwa viumbehai .Hapa ni ndani ya hifadhi ya wanyamapori ya Liparamba ambako mto huo unapita  ndani ya hifadhi hiyo .Vipimo vya maabara kutoka wizara ya maji makao makuu jijini Dar es salaam vilivyochukuliwa mwaka 2009 vinaonesha kuwa viwango vya uchafuzi vimezidi viwango vya kitaifa na kimataifa.

Maji salama kwa matumizi ya binadamu na viumbe vingine hai alisema, yanapaswa kuwa na kiwango cha mg/n.m (mercury not mentioned) yenye maana kwamba hakuna kabisa kemikali ya zebaki katika maji.

Taasisi hizo za uchunguzi zilibaini pia kuwa maji ya mto Lunyere  yana kiwango taka  ambacho kitaaluma zinaitwa “ turbidity,” ambazo zinavuka kiwango kinachokubalika kitaifa pamoja na kile cha Shirika la Afya Duniani (WHO).

Kiwango cha taka kinachokubalika kitaifa  kwenye maji kinaelezwa kitaalam kuwa ni etu 30; kiwango  cha kimataifa ni  etu 5 – 25. Lakini maji ya Lunyere yana etu 1,141, jambo ambalo Payovera ameeleza kuwa “ni hatari sana.”

Kwa mujibu wa rekodi zilizopo wilayani Mbinga, shughuli za uchimbaji zinazofanywa na wachimbaji wadogo, zilianza tangu mwaka 2004 katika kijiji cha Darpori.

Matumizi ya zebaki kwa ajili ya kusafishia dhahabu yameenea katika vyanzo vya maji vya mto Lunyere vilivyopo kwenye milima ya Sufuri A na Namba Tisa, nchini Msumbiji na katika kijiji cha Darpori kilichopo mpakani, upande wa Tanzania.

Mto Lunyere hupita katika hifadhi ya wanyamapori ya Liparamba inayounganisha Tanzania na Msumbiji, kisha kuungana na mto Ruvuma na kumwaga maji yake katika Bahari ya Hindi.

Mwandishi aliingia nchini Msumbiji hadi kijiji cha Mpapa kilichopo kata ya Lupilichi mkoa wa  Lichinga hadi  kuona vyanzo vya mto Lunyere katika vilima vya Sifuri A. Mkondo wote wa mto kupitia vijiji vya Mpapa, Kitonga na Namba Tisa, wachimbaji wanasafisha dhahabu kwa kutumia zebaki na maji yenye kemikali hii yanaingia katika mto huu.

Wilbert Mahundi, anayejitambulisha kuwa mtaalum wa  madini  na ambaye hivi sasa ni katibu wa mtandao wa mazingira mkoa wa Ruvuma(RUNEA) na mwenyekiti wa asasi ya Tanzania Mineral Mining Trust Fund(TMMTF), anasema  zebaki siyo kemikali ya kuchezea.

Anasema zebaki kwa binadamu inaweza kusababisha ugonjwa wa moyo, kansa ya tumbo,ini, koo na ngozi.zebaki  ni nzito, haiyeyuki kwa urahisi na hugota chini ya vyanzo vya maji kama mto na kuvutia viumbehai kama samaki kuila.

Mkuu wa chuo cha maofisa tabibu Songea Dk.Salla Paul  na mkufunzi mwandamizi wa chuo hicho Dk.Joseph Mapunda wanazitaja dalili za mtu aliyeathirika kwa zebaki kuwa ni  mwili kuwa na vidonda vya mara kwa mara, ukurutu, kupoteza kumbukumbu, macho kupoteza uwezo wa kuona na homa za matumbo.

Dalili nyingine mama mjamzito hutokwa  maji sehemu za siri isivyo kawaida ,viganja vya mikono na mwili mzima kuwa na rangi ya njano,mwili kukosa nguvu,kukosa hamu ya kula, kuongezeka kwa mapigo ya moyo,mifupa inakuwa laini,kutapika ,maumivu ya kichwa ya mara kwa mara kwikwi na kiu.

Kuhusu samaki Mahundi anasema Mfumo wa chakula wa samaki hauna uwezo wa kuyeyusha zebaki, kwa hiyo kama amekunywa kemikali hiyo, matokeo yake inaendelea kubaki mwilini  mwake siku zote;

Amesema mtu ambaye atakula samaki mwenye zebaki, anaweza kupata madhara  kwa kuwa “utayarishaji samaki kwa ajili ya chakula, iwe kwa kupika au kuchoma, hauna uwezo wa kuondoa zebaki ndani ya samaki,” .

Mtaalamu kutoka  shirika la utafiti na maendeleo ya viwanda Tanzania  yaani TIRDO Anselimo Moshi anatahadharisha kuwa mazao ya mizizi kama vile muhogo yasilimwe karibu na maeneo ya machimbo ya madini au mabondeni ambako yanatiririkia maji kutoka mabondeni.

Anasema zebaki  inayotumika kusafishia madini  inaingia kwenye maji na kunyonywa na mimea kama  muhogo na  kwamba waepuke kutumia maji yaliathirika na zebaki kwa kuloweka mihogo  pamoja na mazao mengine  ya mizizi.

Mbali na binadamu, maji yenye kemikali ya zebaki kutoka vijito vya Mkurusi na Mihomba na yanayoingia Lunyere, yanatumiwa na wanyama katika hifadhi ya wanyamapori ya Liparamba na viumbe hai walioko katika mito hiyo.

Miongoni mwa wachimbaji  dhahabu wanaochangia sumu katika mtu Lunyere na mto Ruvuma, ni Watanzania wapatao 10,000 walio katika machimbo madogo ya dhahabu nchini Msumbiji.

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Darpori kilichopo kata ya Tingi, wilayani Mbinga, Rafael Mapunda anasema tangu ameanza kutoa vibali vya kuruhusu Watanzania kuingia nchini Msumbiji kwa ajili ya kuchimba na kununua dhahabu, “takwimu zangu zinaonesha wamevuka wachimbaji wanaokaribia  10,000.”

Awali, wachimbaji wengi walikuwa katika kijiji cha Darpori chenye vitongoji vya Lunyere, Songeapori, Tanzania One na Njarambe.  Serikali ya Tanzania ilipotumia nguvu za sheria kuzuia matumizi ya zebaki, wananchi wengi wakakimbilia Msumbiji ambako hakuna katazo la uchimbaji kwenye vyanzo vya mito.

Shughuli zote za uuzaji na ununuzi wa madini  kutoka Tanzania na Msumbiji  zinafanywa na raia wa nchi zote mbili katika kijiji cha Darpori ambako wameweka makazi yao ya kudumu.

Hata hivyo, mwandishi aliwakuta wachimbaji, mmoja mmoja, kwenye kitongoji cha Songeapori upande wa Tanzania, ambao wanaendelea kuchimba dhahabu na kuisafishia mtoni Lunyere tena kwa kutumia zebaki.

Anderson Haule ni mwenyekiti wa kijiji cha Darpori, Anasema ameahidi kupeleka katika vikao vyao vya ujirani mwema kati ya Tanzania na Msumbiji, ajenda ya uchafuzi wa mto unaofanywa kwa kiwango kikubwa katika machimbo ya Msumbiji na “athari zake kutokea hapa nchini.”

Ngwatura Ndunguru, afisa mkuu mstaafu katika wizara ya maliasili na utalii na aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo la Mbinga Magharibi anasema tatizo la mto Lunyere linapaswa kutatuliwa na pande mbili za nchi zinazopakana.

“Ufumbuzi sharti uhusishe nchi zote mbili, ikiwa ni pamoja na kuangalia mkataba wa maji kimataifa na kwa nchi za Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC); pia kuangalia makubaliano ya Ukanda wa Mtwara (The Mtwara Coridor),” anaeleza Ndunguru jinsi ya kukabiliana na uchafuzi wa mto Lunyere.

 

1 Comment
  • Jamani serikali ya Tanzania tunaamini kuwa serikali yetu ni sikivu sana ebu angalieni wananchi wenu wanavyo umiaaaaaaaaaaaa! serikali yetu kupitia viongozi wetu tunaomba wasaidieni hawa wenzetu jamaniiiiiiiiiii!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *