Maji ya Visima ni kichocheo cha Kipindupindu jijini Dar es Salaam

Jamii Africa

MOJA ya njia kubwa ambayo inaweza kueneza magonjwa kama kipindupindu ni matumizi ya maji machafu. Maji machafu yanaweza kuwa ya visima, bomba- kama hayawekwi dawa kuua vijidudu na kama hayatachemshwa kabla ya kutumika.

Katika Tanzania, Jiji la Dar es Salaam linatajwa kuongoza kukumbwa na magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya maji machafu.

Hali hiyo inatokana na jiji hilo kuwa na idadi kubwa ya visima venye vimelea ambavyo vinaweza kusababisha magonjwa ya milipuko, hasa kipindupindu na homa za matumbo.

Kipindupindu ni ugonjwa unaoambukizwa kupitia maji au chakula chenye vimelea ambavyo kitaalamu hujulikana kwa jina la ‘Vibrio Cholerae.’  Vimelea hivi huishi katika maji yaliyochafuliwa hasa na kinyesi

Katika mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu uliotokea mwaka 2015 katika jiji hilo, maeneo mengi yanapata huduma hafifu ama kutofikiwa kabisa na maji ya Shirika la Kusambaza Maji Dar es Salaam, (Dawasco) yanaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa kipindupindu.

Maeneo hayo ni Buguruni, Kigogo na Yombo ambayo hutegemea zaidi maji ya visima virefu kama mbadala wa huduma za Dawasco, lakini visima hivyo havina maji salama.

Hili linathibitishwa na kauli ya Waziri wa Maji na Umwagilia, Mhandisi Gerson Lwenge wakati wa bunge la bajeti 2016/2017 alipoelezea kuhusu uchunguzi wa visima 108 ambapo visima 66 vilikuwa sio salama na maji yake yalikuwa na vimelea vya ugonjwa wa kipindupindu. Visima virefu vilikuwa 40 na vifupi ni 26.

Utafiti wa Chuo Kikuu cha Ardhi, unaonesha maji ya visima vingi sio salama na kushauri wachimba visima kupata ushauri wa kitaalamu ili kuepusha jamii na magonjwa kwa kutumia maji yasiyokuwa salama.

Gharama za kuchimba kisima hutegemea maelewano baina ya mchimbaji na anayetaka huduma hiyo.

Katika eneo la Buguruni Madenge ambapo FikraPevu ilitembelea, ilikuta visima virefu vikiwa vinapeleka maji moja kwa moja kwenye matenki na kisha wahusika kuuzia wakazi wa maeneo hayo bila maji hayo kutibiwa.

Kijana mmoja aliyekutwa katika eneo hilo akiuza maji hayo, Hussein Magema, alisema yeye amepewa tu kazi ya kuuza maji, lakini hajui kama yanawekwa dawa au la.

“Mimi nimeajiriwa tu hapa kuuza maji, lakini bosi wangu sijui kama anaweka dawa au vinginevyo,” anaongeza kijana huyo anayeuza ndoo moja ya lita ishirini kwa Sh. 400

FikraPevu ilimtafuta na kumpata mmiliki wa biashara hiyo, lakini aligoma kuzungumza wala kutaja jina lake.

Hata hivyo, wakazi wengi wanaotumia maji hayo, walikiri kuwa hawajawahi kuona maji yanayoingia kwenye tanki na kuuziwa yakiwekwa dawa ili kua vimelea.

Hii ni tofauti kabisa na jinsi ambavyo mamlaka za maji hutakiwa kutibu maji kabla ya kuwafikia wananchi, ambapo maji hupitia hatua tofauti -tofauti na kisha kuwekwa dawa kwa ajili ya kuuwa vimelea.

Kufikia Septemba 2016, Dar Es Salaam ilikuwa na visima virefu 676 huku Wilaya za Temeke na Ilala zikiongoza kutokana na kutofikiwa na maji ya DAWASCO. Kinondoni, kwa kuwa na mtandao mkubwa wa maji ya Dawasco, hali ya kipindupindu sio mbaya.

Hali ya upatikanaji wa maji kutoka Dawasco ni mbaya kwani kwa wilaya ya Kinondoni ni asilimia 20 hupata maji kwa saa kati ya 16-24, wakati asilimia 40, hupata maji kwa saa tatu huku Temeke ikiwa ni ailimia 10 na Ilala ni asilimia 30.

Wataalamu wanaeleza kuwa visima vingi huchimbwa bila kufuata utaratibu na kusababisha kuwepo kwa vimelea vya magonjwa.

FikraPevu imeelezwa na Mekizedeck Malosha, mmoja wa watu wanaojishughulisha na uchimbaji visima virefu, kuwa kabla ya kuanza kuchimba kisima ni lazima kutembelea eneo husika, kulikagua, kuchukua sampuli ya maji eneo hilo na kwenda kuyapima maabara.

Maji ya visima virefu na vifupi ni njia nzuri ya kutatua tatizo la maji, endapo hatua stahiki zitafuatwa.

Wizara ya Maji na Umwagiliaji inatakuwa kuweka utaratibu wa lazima kwa kupima ubora wa maji kila mwaka katika visima vilivyopo na kuhakikisha vipya vinachimbwa baada ya kukamiisha taratibu zote na siyo kuacha kila mmoja kuchimba na kuuza maji holelaholela

Tunaweza kutibu tatizo la maji na kuibua tatizo jingine, tena baya zaidi, la vifo vitokanavyo na magonjwa kama kipindupindu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *