SIKU moja baada ya Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza (RPC), Liberatus Barlow (52), kuuawa na kundi la watu wanaosadikiwa kuwa majambazi, taarifa zinasema polisi wa kimataifa watashirikishwa kufanya uchunguzi na kukamata wahusika wa tukio hilo.
Polisi mkoani Mwanza wameapa kupambana kuwasaka waliohusika katika tukio hilo la kinyama, huku idadi ya watu waliokamatwa hadi kufikia Jumapili jioni ikitajwa kufikia watu 15.
Kamanda Barlow enzi za uhai wake
Taarifa kutoka ndani ya jeshi hilo zilizopatikana jijini Mwanza zinaeleza kwamba, idadi hiyo ya watuhumiwa waliokamatwa huenda ikaongezeka maradufu kuanzia kesho Jumatatu, baada ya marehemu Barlow (pichani), kuagwa jijini hapa kesho kisha kusafirishwa hadi nyumbani kwake Dar es Salaam, na baadaye Jumanne kusafirishwa nyumbani kwao mkoani Kilimanjaro tayari kwa mazishi.
Kwa mujibu wa taarifa hizo ambazo baadaye Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Lily Matola pamoja na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Manumba walikataa kutaja idadi halisi ya watuhumiwa waliowakamata, zinadai kwamba upelelezi wa kina na wa hali ya juu unafanyika kote nchini, ikiwa ni pamoja na maeneo ya mipakani ili kuwanasa watuhumiwa wa mauaji hayo.
"Kazi ya kukamata watu wanaoshukiwa inaendelea. Na hadi leo Jumapili zaidi ya watu 15 wameshakamatwa… na upelelezi wa kina unafanyika kila kona ya nchi hii na hadi maeneo ya mipakani.
"Kuuawa kwa Kamanda Barlow si tukio dogo. Inahitajika nguvu ya ziada kuwanasa watuhumiwa, ndiyo maana IGP Said Mwema amemtuma haraka sana kuja Mwanza DCI Manumba. Ninyi subilieni tu mtasikia…wote waliohusika tutawakamata tu", kilisema chanzo cha habari kutoka ndani ya jeshi la polisi mkoani Mwanza (jina tunalihifadhi).
Kuhusu ripoti ya madaktari
Alipoulizwa na FikraPevu iwapo uchunguzi wa madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC), ya jijini Mwanza juu ya mwili wa marehemu Barlow, Kaimu Kamanda wa jeshi la polisi mkoani hapa, Matola alisema jopo la madaktari bado wanaendelea kufanyakazi yao ya uchunguzi.
"Suala la ripoti ya madaktari kuhusu mwili wa RPC Barlow bado wanaendelea huko hospitalini Bugando. Subilieni tutawaambia tu ndani ya siku chache!", alisema Kaimu Kamanda huyo wa polisi mkoani hapa, Matola.
Kufuatia taarifa hiyo ya Matola, habari za awali zilizopatikana kutoka kwa vyanzo vyetu Bugando zinadai kwamba, hadi kufikia leo alasiri tayari jopo la madaktari walikuwa wameshamaliza uchunguzi wao juu ya marehemu Kamanda wa polisi mkoani hapa.
Inadaiwa kwamba, miongoni mwa risasi zilizompata kamanda huyo, risasi moja ilimpiga shingoni kisha kuvunja na kuharibu kabisa shingo pamoja na mfumo wa damu, hali iliyosababisha kuvuja kwa damu nyingi.
Makachero wa Interpol kusaidia
Inadaiwa kwamba ili kufanikiwa kuwanasa watuhumiwa wa mauaji hayo ya RPC Barlow, jeshi la polisi limeomba ushirikiano kutoka Kitengo cha upelelezi cha Interpol.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jijini Mwanza, zinadai kwamba baadhi ya askari kutoka vikosi hivyo vya Interpol hapa nchini na nchi jirani vimeshaanza kuwasili kisha kusambaa katika maeneo tofauti Ukanda wa nchi zote za Maziwa Makuu, na kwamba watuhumiwa wote lazima wakamatwe na kufikishwa mahakamani.
"Polisi imeshaomba msaada wa kikosi cha Interpol ili kusaidia kuwanasa wauaji hawa. Hapana shaka lazima watu waliohusika kummiminia risasi na kupoteza uhai wa RPC Barlow watakamatwa tu. Achana na kazi ya Interpol, maana hata mtu amejificha kwenye handaki atapatikana tu", kilisema chanzo kingine cha habari.
Katika hilo, Kaimu Kamanda wa polisi mkoani Mwanza, Matola alipoulizwa na FikraPevu iwapo ni kweli wameomba msaada na nguvu ya kiupelelezi kutoka kwa askari wa Interpol, alishindwa kukubali wala kukanusha, bali alisema:
"Naomba mambo mengine mtuachie sisi, maana bado tunaendelea kufanyakazi hii ya upelelezi. Na tunachokiamini ni kwamba wahusika wote wa mauaji ya RPC Barlow lazima wakamatwe".
Aidha, Kamanda Matola aliwaomba wananchi wote kulisaidia jeshi hilo la polisi katika kuwabaini wahusika wakubwa wa tukio hilo la kuuawa kwa Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, na kwamba waandishi wa habari nao ni sehemu na nguzo muhimu katika kulisaidia jeshi hilo kufikia malengo yake ya kupambana na wahalifu ndani na nje ya mkoa huo.
DCI Manumba anena
Katika mahojiano yake na mwandishi wa habari hizi jioni hii, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Manumba alisema kazi inayofanywa na jeshi hilo la Polisi lazima itawanasa watuhumiwa wote wa mauaji hayo.
"Nina uhakika wahusika wote wa mauaji ya Kamanda Barlow tutawakamata. Kwa sasa kazi ya upelelezi bado inaendelea kufanyika, lakini tutahakikisha sheria inachukuwa mkondo wake kwa watuhumiwa wote", alisema DCI Manumba kwa njia ya simu yake ya kiganjani.
Alipotakiwa kutaja idadi ya watu waliokwisha kukamatwa tangu mauaji ya Kamanda huyo wa Polisi mkoani Mwanza, DCI Manumba ambaye amejichimbia jijini hapa kwa lengo la kuongeza nguvu ya kiupelelezi alisema:
"Hilo la idadi siwezi kusema. Naomba mtuache kwanza tutawaambia mara baada ya kazi kukamilika. Vuteni subira, kazi bado inafanyika".
Msiba wageuzwa siasa
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, baadhi ya watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa baadhi ya wagombea wa nafasi ya uenyekiti wa CCM mkoani Mwanza, wameugeuza msiba huo kama sehemu ya kufanyia kampeni dhidi ya wagombea wanaowahitaji wao ndani ya CCM, baada ya kampeni kuanza kulindima msibani hapo.
Hali hiyo ilijitokeza jana nyumbani kwa marehemu Barlow maeneo ya Pasiansi, ambapo baadhi ya watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa baadhi ya wagombea nafasi ya uenyekiti wa CCM kuanza kupenyeza maneno ya kampeni wakati walipokuwa wameenda kuhani familia ya marehemu huyo.
Baadhi ya watu waliiambia FikraPevu kwamba, wapo baadhi ya wana CCM waliofika nyumbani kwa marehemu Barlow walikuwa wakipiga kampeni kwa ajili ya wagombea wao, na kwamba kampeni hizo zilikwenda sambamba na kuwapaka matope baadhi ya wagombea wasiofungamana na makundi yao.
"Ama kweli dunia imeisha. Watu wanakuja msibani tukidhani wamekuja kuhani, lakini cha ajabu wanaanzisha kampeni za wagombea wanaowataka CCM. Ni kitendo kibaya sana.
"Watu wana machunguna wengine wanalia, halafu mtu anaibuka kuanza kukueleza mambo ya uchaguzi wa CCM ngazi ya mkoa. Huu ni uendawazimu kabisa", alisikika mwombolezaji mmoja.
Uchaguzi wa uenyekiti wa CCM ngazi ya mkoa wa Mwanza, unatarajiwa kufanyika Oktoba 16 mwaka huu, ambapo wanasiasa watato wanaochuana katika kinyang'anyiro hicho ni pamoja na Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Anthony Diallo, Clement Mabina, Zebedayo Athumani, Hussein Mashimba na Joseph Yared.
Alisikika Juzi Oktoba 13 mwaka huu majira ya kati ya saa 7 hadi saa 8 usiku, RPC Barlow alimiminiwa risasi kadhaa maeneo ya shingoni na kundi la watu watano wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, katika maeneo ya Kitangiri jijini Mwanza, wakati alipompeleka nyumbani kwake mwanamke mmoja Doroth Moses ambaye pia ni mwalimu wa shule ya msingi, Nyamagana jijini hapa.
Katika tukio hilo la kinyama, inadaiwa kabla ya RPC kukumbwa na mauti alikuwa amekwenda kuhudhuria kikao cha harusi cha mtoto wa dada yake, aliyetajwa kwa jina la Sembeli Mareto kilichofanyika Frolida hoteli maeneo ya Kitangiri jijini hapa, na kwamba baada ya kikao hicho marehemu aliwasha gari lake binafsi kisha kumpeleka nyumbani kwake Mareto.
Inadaiwa kwamba, baada ya kumfikisha nyumbani mpwa wake huyo, RPC Barlow aliyekuwa akiendesha gari lake binafsi, akiwa njiani kuelekea nyumbani kwake maeneo ya Pasiansi alikutana na mwalimu Doroth Moses ambapo aliombwa lifti ya kumpeleka nyumbani kwake Kitangiri, na bila ajizi Kamanda huyo alimpatia msaada huo hadi nyumbani alikokwenda kuuawa kinyama na watu wanaodaiwa waliwakuta getini nyumbani kwa mwanamke huyo.
Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – FikraPevu, Mwanza.
jamaa zetu wameishiwa kampeni msibani hii sasa kali na bado mlianza misikitini mkahamia makanisani sasa msibani mtafika mpaka makaburini
Kwanza,
MOLA amrehemu marehemu mtu ambaye alikuwa mtendaji kazi mzuri katika majukumu yake.
Pili,
Wanasiasa acheni uchuro wenu, hayo ndiyo mliyoyaleta kule kwenye msiba wa chacha Wangwe ikawa shida kweli kweli je hamjifunzi jamani?siasa zina sehemu zake kama vile majukwaani nasio sehemu yenye majonzi kama hiyo (msibani)
Ninyi wanasiasa hasa mliokuwa hapo msibani na mkageuza kuhani kuwa nafasi na uwanja wa kampeni mkome.
Tuwe na staha jamani kwani utakuwa hueleweki kwenye jamii unapochanganya mafaili sehemu ambazo sizo.Najua mnapenda sana madaraka lakini sio msibani mnaanza longolongo.
Mbona hamuliweki wazi suala la huyo mwanamke?
Ni na nani kwake?
Na kwanini ampeleke nyumbani kwake?
Je ilikuwa kawaida yake kumpeleka?
Kwanini watu wamsubili sehemu ambayo si mazoea yake kwenda?
Huyo mwanamke ana uhusiano na nani?
Ameolewa au la?
Nikipata hayo majibu yatanifanya niyaelewe vizuri mauaji hayo, vinginevyo mtakuwa mnanichekesha tu.
Je yule ofisa wa Uhamiaji aliyetaka kuuawa na polisi kule Mhandu, Nyakato hana uhusiano na huyo mwanamke? Kwa nini majibu ya Kamanda Barlow kwa mkuu wa Uhamiaji yanaonesha kuwa walikusudia kumwua huyo jamaa (Check Nipashe 12/10/2012).
Hepu naomba Sitta Tumma aingie kwa undani aeleze jambo hilo.
nafunga vifo vyote,vyakutumwa ama vya visasi!
jamaa alikuwa mchapa kazi lkn kwa nn hakuwa na ulinzi
mola ampumzishe kwa amani