Mauzo ya Dangote Cement yapaa kwa 12.6% ndani ya miezi sita

Jamii Africa

MAUZO ya saruji ya Dangote Cement, inayoongoza kwa uzalishaji wa saruji barani Afrika, yamepaa kwa asilimia 12.6 barani humo katika kipindi cha miezi sita kilichoishia Juni 30, 2017.

Kampuni hiyo inayomilikiwa na mfanyabiashara tajiri namba moja barani Afrika, Alhaj Aliko Dangote wa Nigeria, katika kipindi hicho imeuza kiasi cha tani za ujazo 400,000 nchini Tanzania pekee.

Hata hivyo, FikraPevu inafahamu kwamba, mauzo hayo hayajafikia hata nusu ya uzalishaji katika kiwanda chake cha Mtwara ambako malengo ya uzalishaji wake ni tani za ujazo milioni 3 kwa mwaka.

Uzalishaji nchini Tanzania unaweza kuongezeka kufuatia kampuni hiyo kupewa leseni ya kuchimba makaa ya mawe kwa ajili ya nishati na kuepukana na kukwama kwa uzalishaji kutokana na kukati kwa umeme mara kwa mara.

Mnamo Desemba 2016, kampuni hiyo ilisitisha uzalishaji kwa muda, ikilalamikia matatizo ya kiufundi na gharama kubwa za uzalishaji, lakini Mwezi Machi 2017 serikali ikaipatia kampuni hiyo eneo la kuchimba makaa hayo ya mawe huko Ngaka, Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma lenye ukubwa wa kilometa za mraba 9.98.

Eneo ambalo Dangote alipewa katika Bonde la Ngaka ni sehemu ya eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 840 zilizo chini ya leseni ya kampuni ya Tancoal Energy Ltd, kampuni tanzu ya Intra Energy Corp, ambayo imeandikishwa katika Soko la Hisa la Australia.

Hata hivyo, Intra Energy ilikwisharidhia kuachia sehemu ya eneo hilo kwa Dangote.

Dangote Cement ambayo ni kampuni tanzu ya Dangote Group, inazalisha saruji katika nchi 10 barani Afrika ambapo mapato ya mwaka 2016 pekee yalifikia Dola za Marekani bilioni 2 huku kampuni hiyo ikiwa imeajiri wafanyakazi zaidi ya 17,000.

Nchi nyingine mbali ya Tanzania, ni Nigeria, Cameroon, Congo, Ethiopia, Ghana, Senegal, Sierra Leone, Afrika Kusini, na Zambia.

Taarifa zilizotolewa kwenye Soko la Hisa la Nigeria (NSE) leo hii zimeonyesha kwamba, kuongezeka kwa kiwango cha mauzo kumedhihirisha kukubalika kwa saruji hiyo katika mataifa ya Afrika. 

Mapato katika viwanda vyake vya Nigeria yameongezeka kwa asilimia 34.5 ndani ya miezi sita iliyopita na kufikia Dola za Marekani 943.9 milioni wakati mapato ya jumla katika mataifa mengine tisa, ikiwemo Tanzania, yameongezeka kwa asilimia 63.7 kufikia Dola za Marekani 403 milioni kutoka Dola 246.2 milioni.

Uchambuzi wa mauzo ya nusu mwaka 2017 yanaonyesha kwamba uzalishaji wa jumla barani Afrika umeongezeka kwa asilimia 12.6 kufikia tani milioni 4.7 huku Sierra Leone ikichangia pakubwa.

Rekodi za mauzo katika nchi mbalimbali barani Afrika zinaonyesha kwamba jumla ya tani milioni 1.1 za saruji ziliuzwa nchini Ethiopia, takriban tani 700,000 ziliuzwa Senegal, tani 600,00 ziliuzwa Cameroon, tani 500,000 ziliuzwa Ghana, na tani 300,000 ziliuzwa Zambia.

Hata hivyo, mauzo ya saruji nchini Nigeria yameshuka kutoka tani za ujazo milioni 8.8 milioni hadi tani za ujazo 6.9 milioni, hali ambayo inatajwa kuchangiwa na mvua kubwa zilizonyesha ambazo zilikwamisha miradi mingi ya ujenzi nchini humo.

Akielezea kuhusu matokeo ya nusu ya mwaka, Mtendaji Mkuu wa Dangote Cement, Onne van der Weijde ameeleza kufurahishwa na mapato ya kampuni hiyo licha ya kuporomoka kwa mauzo ya Nigeria.

Alikaririwa akisema: “Mapato yetu yameendelea kukua licha ya kushuka kwa mauzo nchini Nigeria, hususan kutokana na mvua kubwa zilizonyesha karibuni. Miradi yetu katika nchi nyingine za Afrika inaendelea kukua. Tumeona mauzo yetu ya kwanza nchini Sierra Leone katika robo ya kwanza na kiwanda chetu kipya nchini Congo kitaanza kuzalisha hivi karibuni.”

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *