UTAFITI wa Taasisi ya Tanzania Horticultural (TAHA) umebaini kuwapo kwa masoko makubwa ya matunda na mbogamboga kwa nchi za Ulaya hususani mji wa Berlin nchini Ujerumani.
Hayo yalibainika hivi karibuni wakati wa utolewaji wa Mada ya kujiendeleza kiuchumi kwa waandishi wa habari iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa TAHA Jacqueline Mkindi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa vyombo vya Habari duniani.
Maadhimisho hayo yaliandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha (APC).
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkindi aliwaambia waandishi wa habari kwamba kama wanataka kujikomboa kichumi basi hawana budi kuingia katika kilimo cha mbogamboga na matunda kwani kinafaida kubwa.
“Tanzania bado tupo nyuma katika kilimo cha horticultural, wenzetu Kenya wanaingiza takribani Dola za Marekani Bilioni mbili kwa mwaka kwa kuuza bidhaa zao nje.
“Wanaofanya biashara hii si wakulima wakubwa kama tunavyodhani bali ni wakulima wadogo wengi ni wanawake, kwanini nyinyi waandishi wa habari mshindwe kuendesha kilimo hiki ili mjikomboe?”alihoji Mkindi.
Mkindi alisema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na TAHA, masoko ya matunda na mbogamboga yamekuwa mengi zaidi kwa nchi za Ulaya hususani mjini wa Berlin.
“Mji wa Berlin pekee unawanunuzi wanaohitaji tani 30 hadi 40 za bidhaa kutoka Tanzania kwa wiki. Katika mazingira haya kwanini msijishughulishe na kilimo cha bustani za mbogamboga ni rahisi kuinuka kiuchumi,” alisisitiza Mkindi.
Kutokana na kuwapo kwa soko hilo Mkurugenzi Mtendaji huyo aliyataja matunda yanayoongoza kwa kununuliwa katika nchi za Ulaya kuwa ni Maparachichi, Maembe, Mananasi na mizabibu.
Alisema moja ya mipango ya TAHA ni kuendesha mtandao wa mawasiliano (marketing and information system) kwa kuwapatia wadau bei za mazao 13 katika masoko 12 nchini.
Kutokana na changamoto hiyo aliyoitoa kwa waandishi wa habari, baadhi walionyesha kuguswa na kilimo hicho na kuahidi kujipanga kwa ajili ya kuanza utekelezaji.
Akizungumzia changamoto hiyo mwandishi wa habari wa Kituo cha Redio cha Redio Five David Rwenyagira alisema, hiyo ni changamoto kwa waandishi kijinyanyua kiuchumi, badala ya kuendelea kutegemea mishiko ya semina na fedha kidogo wanazolipwa kwa habari wanazoziandika.
Habari hii imeandikwa na mwandishi wa FikraPevu aliyeko jijini Arusha – [email protected]
Tunahitaji taarifa zaidi, zilizo kwenye hali ya kutumika, bei na Ubora pamoja na kiwango bora cha malighafi hizi……….Tafadhali TAHA tupatieni taarifa zilizo rahisi kumezeka.
Taarifa kama hizi ndo zinazochangia watanzania kuendelea kuwa maskini.
Hakuna information zozote zitakazomuwezesha mtanzania kuchangamkia taarifa hiyo hapo juu. Kwa mfano taarifa kuhusu viwango vya ubora, bei za bidhaa na jinsi gani mtanzania atatuma hizo bidhaa nje (contact persons).
Kibaya zaidi hakuna hata contact za mwandishi wa habari ili mtu aweze kuulizia kupata taarifa zaidi!
tunajua kwamba nje soko la mazao yatokanayo na horticulture ni kubwa, ila kama members wa TAHA ni makampuni na taasisi peke yake tutafika wapi. TAHA wakifanya vikao na wadau kutoka nchi za nje ada ya kuudhuria ni tsh laki 3 kwa kila mhudhuriaji..!! fikra finyu, amna kitu
Hivi watanzania tunaelekea wapi? kwa sasa sisi vijana tunarudi vijijini kwa ajili ya kufanya kilimo. Lakini serikali bado haitusaidii kabisa kwenye masoko ya ndani na ya nje pia. Sasa kama hawa TAHA wamefanya nini baada ya huo mkutano?
Ukija sokoni kuna madalali wameshikilia masoko, yani mimi siwezi kuja na mzigo wangu nikauza mwenyewe hadi nimkabidhi dalali kweli? Then anauza kwa bei anayojua yeye kisha anakata sijui
1. hushuru wa mazao,
2. posho yake,
3. ushuru wa soko,
4. kushusha, ukiweka na
5. usafiri toka shamba,
6. ushuru wa vijijini,
7.kuvuna na kupack.
Yani kweli ndio maana vijana hawataki kurudi vijijini kwa kuwa wanaona kama wanawafanyia watu wengine wanaotaka hela bila jasho.
tuchangamkie fursa hizi vijana wa kitanzania. tuache kuzunguka mtaani bila kazi.