Mchanga wa dhahabu wamng’oa Profesa Muhongo Nishati na Madini. Bodi ya TMAA yavunjwa, mkurugenzi asimamishwa

Jamii Africa

RAIS Dkt. John Magufuli, amemtaka Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ajiuzulu mara moja kufuatia upotevu wa mabilioni ya fedha katika usafirishaji wa mchanga wa dhahabu (makenikia).

Akizungumza leo Jumatano, Mei 24, 2017 wakati wa kupokea ripoti ya kamati ya kwanza aliyoiunda kuchunguza shehena ya makontena yenye mchanga huo wa dhahabu (makenikia) yaliyozuiliwa katika bandari mbalimbli nchini tangu mwezi Machi 2017, Rais Magufuli amesema ingawa Profesa Muhongo ni rafiki yake na anampenda, lakini kwenye hilo ni lazima ajitafakari na kujitathmini.

Rais Dkt. John Magufuli akipokea ripoti ya Kamati ya Uchunguzi wa Mchanga wa Dhahabu kutoka kwa mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Abdulkarim Hamisi Mruma (kushoto) leo Jumatano, Mei 24, 2017. Katikati ni Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Profesa Sospeter Muhongo.

“Ripoti hii ikipita hivi hivi tutakuwa watu wa ajabu sana, tutafanya kitu, tunasubiri ile ripoti nyingine… Nampenda sana Profesa Mhongo lakini pia ni rafiki yangu, lakini kwenye hili, ajifikirie, ajitathmini na bila kuchelewa nilitaka aachie madaraka,” alikaririwa akisema.

Uzembe wa Wizara na Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) umeelezwa kuchangia upotevu wa mabilioni ya fedha ambapo katika uchunguzi wa kamati hiyo katika makontena 277 pekee imeelezwa kuwa yalikuwa na madini ya thamani ya jumla ya Shs. 261.5 bilioni.

FikraPevu, ambayo ilifuatilia kwa karibu tukio hilo, imemnukuu Rais Magufuli akitamka bayana kuyakubali mapendekezo yote ya kamati hiyo ya kwanza, ambapo mbali ya kuivunja rasmi Bodi ya Wakurugenzi ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), lakini pia amemsimamisha kazi mara moja Mkurugenzi Mkuu wa TMAA, Gilay Shamika huku akiiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwachunguza wafanyakazi wote wa wakala huo.

Rais Dkt. John Magufuli.

Makontena yenye mchanga wa dhahabu yaliyozuiliwa katika Bandari ya Dar es Salaam. 

“Shughuli zote zinazohusu madini, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vianze kutumika sawasawa. Wizara wameshindwa kusimamia TMAA, ujenzi wa Smelter (mtambo wa kuchenjua mchanga) pia imeshindwa kuweka utaratibu wa kufuatili haya makinikia, mbona huwa wanakwenda Ulaya? Kamishna wa madini anafanya nini? Waziri anafanya nini?” alihoji Rais Magufuli.

Aidha, amevitaka pia vyombo ya dola kuwachunguza watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini wanaoshughulikia madini.

Akizungumzia uamuzi wa uchunguzi huo, Rais Magufuli alisema kwamba vifaa vyote katika ulinzi vilitumika japokuwa wapo waliojitokeza kutaka kuingilia uchunguzi huo huku akibainisha kwamba majina yote ya waliotaka kuvuruga uchunguzi anayo.

“Wapo wengine mnawajua wenyewe wakibwatuka, wengine kwenye mitandao, wamepewa fedha.

“Ndugu zangu, tuko kwenye vita na vita ya uchumi ni mbaya sana, mabilioni ya fedha haya ambayo nchi yetu imepoteza, dhahabu tani 7.8 hadi 13.16 kwa kontena 277. Tani 15.5 ni malori mawili na Land Rover moja. Malori mawili ya tani 7 yanaleta tani 14, labda na pick-up zote umezipaki pale na hio ni kwa makontena 277.

Rais Magufuli akihesabu makontena yenye mchanga wa dhahabu baada ya kuzuru ghafla bandarini Dar es Salaam.

“Kuna kamati inayotaka kujua makontena yanasafirishwa mangapi, haraka haraka ni makontena 250 na 300 kwa mwezi, kwa mwaka zaidi ya makontena 3,600.

“Ni kitu cha kuumiza mno na kwa hili Watanzania wote tushikamane, hospitali watu wanakosa madawa, mashuka, shule watu wanakosa madawati, fedha za treni mpaka tukope kumbe kuna fedha zinamwagika hapa.

“Nilimfukuza Katibu Mkuu wa Nishati na Madini alipoulizwa na Kamati ya Wabunge kiasi cha dhahabu kilichopo, ni aibu kwa mtu aliyesomeshwa na Watanzania such a stupid comment (kutoka kauli ya kipuuzi kama ile).

“(Shilingi) Bilioni 676 hadi trilioni 1.5 tunazipoteza Watanzania, madini mengine hawakujali hata kuyarekodi (Nipe ile document). Tunaweza tukaona kwa miaka 17, tulipaswa kuwa donor country (nchi hisani) kwa vitu tulivyopewa na Mungu.

“Huwezi ukashangaa katika wizara hizi ndio nilichagua watu wazuri wa kuziendesha, kuna tume iliundwa miaka ya nyuma, walidanganya kuna smelter ziko nchi fulani, walipokwenda wakaishia hotelini. Smelter sio tatizo kwenye ripoti, inaonyesha kampuni nyingi zinazoweza kuuza smelter, viongozi hawakuchukua juhudi za kununua smelter.

“Sera ya Taifa ya Madini ya mwaka 2009 inasema haja ya kununua smelter, viongozi wa hizo wizara hawakufanya juhudi, kwanini TMAA wapime kidogo halafu wanakuja kuweka tu seal (lakili) wakati hujui kilichowekwa ndani, kwanini?

“Kwanini wasimamizi wa TMAA ambao ni wizara hawakushtukia? Kwanini bodi ya TMAA haikuwashtukia? Inawezekana nikajiuliza maswali mengi majibu yasipatikane. Inawezekana yakaletwa na tume nyingine, nilikwenda na wenzangu kuteta kidogo. Haiwezi kupita hivi hivi,” alisema Rais Magufuli.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akisisitiza jambo wakati alipozuru ghafla bandarini na kuzuia usafirishaji wa makontena 20 yenye mchanga wa madini.

Awali, mwenyekiti wa kamati hiyo ya kwanza, Profesa Abdulkarim Hamis Mruma, kabla ya kukabidhi ripoti hiyo, alisema kwamba walianza kuandaa mpangokazi, kupitia mafaili yote ya usafirishaji, kutembelea maeneo yote yenye makontena ili kuyachunguza na kuweza kuchukua sampuli.

“Katika kuchukua sampuli tulifuata taratibu za kisayansi ili kufanya sampling (ulinganishaji) na kufanya uchunguzi wa materials zote,” alisema Profesa Mruma.

 

Matokeo ya Uchunguzi

Profesa Mruma alisema kwamba, jumla ya makontena 277 yalifanyiwa uchunguzi ambapo Kamati yake imebaini kuwepo kwa viwango vingi vya juu vya madini ya dhahabu, copper (shaba), chuma na mengine ndani ya makenikia (mchanga) yaliyobebwa kwenye makontena.

Ripoti ya kamati hiyo imeeleza kwamba, baada ya uchunguzi imebainika kuwa makontena yote hayo yalikuwa na jumla ya tani 1.2 za dhahabu yenye thamani ya Shs. 7.5 bilioni, madini ya fedha (silver) gramu 202.7 – 351 kwa tani, lakini iliripotiwa nusu tu ya gramu zilizomo kwenye kila kontena.

“Madini ya Sulphur ni 16.7 – 50.8 kwa tani (kwa tani zilizopatikana 2,161 kwa makontena 277) ambazo zina thamani ya Shs. 1.4 bilioni,” alisema.

Aidha, madini ya Chuma ni 13.6 – 30.6 kwa tani (kwa makontena yote 277) yakiwa na thamani ya Shs. 2.3 bilioni, na madini ya Copper (shaba) ni 17.6 – 23.3 kwa tani (kwa makontena 277) ambayo yana thamani ya Shs. 13.6 bilioni.

 

Tthamani ya jumla

Profesa Mruma amesema kwamba, Kamati imebaini kuna upotevu mkubwa wa mapato ya serikali katika ukokotoaji wa mirabaha.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimsikiliza Profesa Abdulkarim Hamis Mruma, Mwenyekiti wa Kamati ya Kwanza, baada ya kumwapisha kuchunguza mchanga wa dhahabu unaosafirishwa nje ya nchi.

“Bahati mbaya madini haya (sulphur na chuma) hayahusishwi katika kukokotoa mirabaha. Ni Silver, Shaba na dhahabu pekee ndiyo yanayoripotiwa,” alisema.

Aidha, aliongeza kwamba, kuna madini mkakati (strategic metals) ambayo yanalingana na dhahabu, lakini hayakuhusishwa pia japo yanahitajika sana duniani kwa sasa na yana thamani kubwa.

“Madini yote haya yalikuwa na thamani ya jumla ya Shs. 261.5 bilioni,” alisema. “Mheshimiwa Rais, hivyo ndivyo viwango na mapato tuliyopoteza.”

Alisema pamoja na kuchunguza makenikia, kamati ilichunguza pia shehena ya mbale za shaba ambapo iligundulika kuna kiwango cha dhahabu cha gramu 38.9.

“Katika kufuatilia utendaji wa TMAA, Kamati ilibaini kuwa wakala huo ulikuwa haufungi utepe wa kudhibiti makontena (ufungaji unafanywa wakati kusafirisha tu). Hii inatoa fursa ya watu kuchezea viwango. Tunapendekeza wakala wafunge utepe mwanzo.

“Uwezo wa scanner inayoangalia yaliyomo kwenye makenikia ndani ya kontena ni hafifu. Mfano, tulijaribu kuficha vipande vya chuma, scanner haikuona. Hivyo, mtu akiamua kuficha vitu kwenye makenikia haviwezi kubainika,” alisema.

 

Mapendekezo ya Kamati

Kamati hiyo ilipendekeza yafuatayo:

1. Serikali isitishe usafirishaji wa mchanga mpaka mrabaha stahiki utakapolipwa serikalini kwa kuzingatia thamani halisi ya makenikia.

2. Kuhakikisha ujenzi wa smelter unafanyika haraka ili makenikia hayo yasafishwe ndani ya nchi ili madini yote yaweze kufahamika na kutozwa mrabaha sahihi.

3. Tepe za udhibiti zifungwe mara moja ili kuepuka udanganyifu unaoweza kufanyika wakati wa kuchukua sampuli.

4. TMAA ipime metali zote zilizomo kwenye makenikia ili kupata thamani halisi ya metali hizo (mrabaha).

5. Kutokana na kuwepo madini mbalimbali kwenye mbale za shaba, TMAA ipime viwango vya metali zote muhimu katika mbale zinazosafirishwa bila kujali kilichoandikwa kwa msafirishaji.

6. Serikali iwachukulie hatua watendaji wa TMAA na wale wa wizara inayohusika.

7. Pamoja na vyombo vya uhakiki, serikali iweke mfumo wa kushtukiza ili kuepuka watendaji kufanya kazi kwa mazoea.

8. Serikali itumie wataalam wa mionzi ili kufunga scanner zenye uwezo sahihi (kwa ajili ya makenikia na mizigo mingine).

“Mhe. Rais, nichukue fursa hii kukushukuru kwa kuwa na imani na sisi na kututeua kutekeleza jukumu hili muhimu ili kuepusha nchi kupata hasara. Ni imani yetu kuwa matokeo ya uchunguzi huu yatatoa msaada mkubwa kwa serikali.

“Shukrani kwa vyombo vya ulinzi na usalama, Wakala wa Jiolojia (Maabara ya Mkemia Mkuu), TPA, TRA, TMAA, Vyuo vya UDSM na MUM (kwa kutoa wataalamu). Kamati hii iko tayari kutoa ufafanuzi pale utakapohitajika. Asante,” alimalizia Profesa Mruma.

Wajumbe wengine wa akamati hiyo walikuwa Profesa Justianian Rwezaura Ikingula, Profesa Joseph Bushweshaiga, Dkt. Yusuf Ngenya, Dkt. Joseph Yoweza Philip, Dkt. Ambrose Itika, Mohamed Zengo Makongoro na Hery Issa Gombela.

Profesa Mruma ndiye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) iliyo chini ya Wizara ya Nishati na Madini, ikiwa na makao yake makuu Dodoma.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *