- Adaiwa Kulibeba Kanisa lake
- Ashindwa kuelezea ujenzi wa kanisa nje ya taratibu
- Viongozi wa kanisa watupiana mpira na wa serikali
MEYA wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Josephat Manyerere (Chadema), anakabiliwa na kashfa ya kushirikiana na waumini wenzake wa Kanisa la Waadventista Wasabaton(SDA Church) ushirika wa Agano ambao wanajenga kanisa lenye orofa pasipo kibali wala wataalamu.
Chanzo cha habari kimeliambia gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina gazetini kwamba ujenzi huo umeanza zaidi ya mwaka mmoja uliopita, huku kiongozi mkuu wa wazee wengine wanne wa kanisa hilo ambaye pia ni mfanyakazi katika halmashauri ya Jiji la mwanza, Gervas Kataga akiwa ndiye msimamizi wa ujenzi huo.
Kashfa hiyo imetokea huku serikali kuu ikiendelea kuamini kazi zinazofanywa na madhehebu ya dini na kusababisha kutoa msamaha wa kodi katika manunuzi ya bidhaa.
Kwa mujibu wa habari, Manyerere ndiye mwenyekiti wa kamati ya Fedha na Uchumi kanisani hapo.
Meya huyo ambaye ni diwani wa kata ya Nyakato katika jimbo la Ilemela anadaiwa kuwa miongoni mwa washauri wa waumini wenzake zaidi ya 100 ambao wameamua kukiuka taratibu na sheria za ujenzi.
Inadaiwa jengo hilo halina bango(sign board),ramani iliyochorwa na kuthibitishwa na wataalamu wa halmashauri, mkandarasi, Mshauri wala Msimamizi mwenye taaluma; na kwamba kazi hizo zinafanywa na waumini wenyewe.
“ Ni jambo la kushangaza kwamba badala ya kusimamia taratibu pamoja na sheria za nchi, Manyerere ndiye anaokenaka mshauri na kinga ya waumini wenzake kwa kuvunja taratibu na sheria za ujenzi” kilidai chanzo chetu cha habari na kuongeza kuwa
Kwa mujibu wa habari, Manyerere ni muumini wa Agano Seventh Day Adventist Church , hata kabla ya kuchaguliwa kuwa Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza mwishoni mwa mwaka jana.
“ huku akijua fika kwamba kufanya hivyo ni kosa kisheria na mbele za Mungu kwa sababu hata maamndiko matakatifu yanasema kuwa ya Mungu mpeni Mungu na ya Kaisali mpeni Kaisali” .
Habari zinadai kwa kutumia wadhifa wake, Meya amewazuia watendaji wa halmashauri ya Jiji ili wasivunje orofa hilo ili kanisa lianze kufanya taratibu za kupatiwa kibali cha ujenzi.
Habari hizo ambazo pia zimethibitishwa na Manyerere pamoja na Mhandisi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Bonephace Nyambele, zinadai kwamba ujenzi huo unasimamiwa na Mzee wa kanisa hilo, Gervas Richard Kataga ambaye pia ni muumuni wa muda mrefu katika kanisa hilo.
Inadaiwa Kataga hana taaluma yoyoye kuhusiana na ujenzi, isipokuwa ni dereva katika ofisi za Halmashsuri ya Jiji la Mwanza.
Habari zinasema Manyerere kwa kushirikiana na Kataga ndio wahamasishaji wakuu wa ujenzi huo.
“ Ni kwa kutumia wadhifa wake ndio maana wataalamu wa ujenzi kutoka ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji wameshindwa kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuzuia ujenzi huo usiendelee au kubomoa jengo hilo kwa sababu linaweza kusababisha madhara hapo baadaye” chanzo cha habari kilidai.
Gazeti hili limeambiwa kuwa orofa hiyo ni kwa ajili ya kanisa jingine la kisasa ambalo pamoja na mambo mengine litakuwa na uwezo kwa kutumiwa na watu 700 kwa wakati mmoja.
Habari zaidi zinadai kwamba eneo la sehemu ya chini ya jengo hilo litatumika kwa ajili ya watoto na kuongeza kuwa orofa ya kwanza itatumiwa na watu wazima.
Inadaiwa kwamba kanisa linatumia mafundi wa ‘mitaani’ ambao wanalipwa ujira wa kati ya shilingi 4,000 hadi shilingi 5,000 kwa kila mita ya eneo.
Habari zinaendelea kudai kwamba ili kuharakisha ujenzi huo, miezi michache iliyopita Manyerere aliwaalika madiwani wenzake kutoka nje ya Jiji la Mwanza kwa ajili ya harambee.
Alipoulizwa kwa njia ya simu, Manyerere alikiri kuwepo kwa ujenzi huo na kwamba yeye ni miongoni mwa waumini wa muda mrefu katika kanisa hilo.
“ Kwani wewe hizo namba za simu za viongozi wa kanisa umezipata wapi hadi ukawapigia; mmoja wao ameniambia kuwa umempgia kumuuliza habari za ujenzi. Mimi ninakusahauri ukamwone mzee wa kanisa ama mchungaji wa mtaa” alidai Manyerere.
Hata hivyo, Meya huyo hakutaka kutoa ufafanuzi juu ya madai kuwa amewazuia wataalamu wa ofisi ya Mhandisi wa Jiji ili wasichuke hatua kutokana na mapungufu yanayokabili ujenzi huo.
“ … kwani tatizo liko wapi bhwana; hata kama mimi ninasali katika kanisa hilo!. Hebu ninakushauri ukamuone mzee wa kanisa (Gervas Kataga) ama Mchungaji wa mtaa wa Mabatini ambaye ofisi yake iko Mabatini SDA Church” alidai Manyerere wakati alipohojiwa na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu.
Kabla ya kuwasiliana na Mzee wa kanisa hilo, mwandishi wa habari hizi alimtafuta mwenyekiti wa shughuli za ujenzi katika ushirika wa Agape SDA, Yusuf Mwita, kwa njia ya simu ambaye pia alikataa kuzungumzia suala hilo kwamba siyo msemaji.
Mwita alilishaur mwandishi huyo ajaribu kuwasiliana na Mzee wa kanisa hilo ama mchungaji wa mtaa wa Mabatini.
Alidai pia kwamba atawasilaiana na muumini mwenzake ambaye ni Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza ili amweleze kuwa kuna waandishi wa habari wamempigia simu wakihoji kuhusu uhali wa ujenzo wa orofa kinyume na taratibu pamoja na sheria za ujenzi.
“ Sawa ujenzi huo upo; lakini wewe ni Mwandishi wa habari au Injinia wa Halmashauri?. Kwa nini unafuatilia mambo ya ujenzi wa kanisa la Mungu! Tafadhali, kamuulize Meya au Injinia wa Jiji” alisema Kataga..
Mzee huyo wa kanisa alishauri suala hilo aulizwe mchungaji wa mtaa wa Mabatini kwa vile yeye ndiye msemaji.
Katika hatua nyingine, mchungaji wa mtaa wa Mabatini, Daniel Maiga alikataa kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa mtaa hauhusiki na ujenzi huo.
Alidai kuwa kanisa la Agano ndilo lenye uwezo wa kuzungumzia mambo yote yanayohusiana na ujenzi kwa sababu wao ndio wenye jengo.
Mchungaji wa mtaa wa Mabatini, Daniel Maiga pia aligoma kutoa ufafanuzi juu ya ujenzi huo kwa madai kwamba yeye siyo msemaji.
“ Kwanza mimi ni mgeni katika mtaa huu; hebu nenda ukamuulizee Mwenyekiti wa Conference( South Nyanza Conference), Joseph Bulengeya” alisema mchungaji Maiga wakati alipohojiwa ofisini kwake mwishoni mwa wiki iliyopita.
Katika hatua nyingine, Bulengeya hakupatikana ofisini kwake ili aweze kuzungumzia suala hilo kwa madai kwamba alikuwa kwenye kikao.
Mhandisi wa Jiji, Bonephace Nyambele alidai kuwa ofisi yake haina taarifa za kuwepo kwa ujenzi huo.
Hata hivyo, aliahidi kuwa atafuatilia na kwamba ikibainika lazima atachukua hatua za kiuhandisi ikiwemo kuzuia ujenzi huo usiendelee.
Manyerere alichaguliwa kuwa diwani wa kata ya Nyakato kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo katika jimbo la Ilemela kupitia uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 31 mwaka jana.
Na. Juma Ng’oko