Imeelezwa kuwa watanzania watalazimika kusubiri kwa muda mrefu ili kupata huduma bora za afya kutokana na uchache wa vituo vya kutolea huduma hizo ambavyo haviendani na ongezeko la idadi ya watu nchini.
Hali hiyo ni tofauti na matakwa ya Sera ya Afya ya mwaka 2007 ambayo inasisitiza kuwa serikali inawajibika kuinua hali ya afya ya wananchi wote na hasa wale walioko kwenye hatari zaidi, kwa kuweka mfumo wa huduma za Afya utakaokidhi mahitaji ya wananchi na kuongeza umri wa kuishi wa watanzania.
Lakini watanzania wengi hawafaidiki na tamko la Sera ikizingatiwa kuwa idadi ya watu inaongezeka sana kuliko maboresho na ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Vituo hivyo vinajumuisha hospitali, vituo vya afya na zahanati ambazo vinatakiwa kujengwa kwenye vijiji, kata na ngazi ya wilaya na mkoa.
Kwa mujibu wa data za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) za mwaka 2017 zinaonyesha kuwa vituo vya kutolea huduma za afya viliongezeka kutoka 6,321 mwaka 2010 hadi kufikia 7,680 mwaka 2016, ambapo ongezeko hilo ni sawa na vituo 1,359 (14%) tu kwa miaka saba na wastani wa vituo 194 kila mwaka.
Idadi ya vituo hivyo haiendani na ongezeko kubwa la watu. Kulingana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 Tanzania ilikuwa na watu milioni 45 na hadi kufikia mwaka 2016 inakadiriwa ilikuwa na watu zaidi milioni 50.
Kwa mtazamo wa kawaida ni kwamba karibu nusu ya wananchi hawapati na huduma bora za afya ikiwemo upatikanaji wa vituo vya kutolea huduma za afya, jambo linaloweza kuwaweka katika hatari ya kupoteza nguvukazi ya taifa na hata maisha.
Hata hivyo, bado ziko juhudi mbalimbali zinazofanyika kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi katika maeneo yao. Takwimu za NBS zinaeleza kuwa hadi mwaka 2016 kulikuwa na zahanati 6,658 ambazo zilikuwa na kliniki 89 za mama na mtoto. Lakini changamoto ni kwamba zahanati nyingi zinakabiliwa na upungufu wa madaktari, dawa, vifaa tiba na uchakavu wa miundombinu.
Kimsingi Sera ya Afya inaelekeza kuwa kila kijiji kinapaswa kuwa na zahanati yake ili kuhakikisha wananchi hawatembei umbali mrefu kufuata huduma kwasababu afya ni huduma muhimu ya kijamii na inapaswa kupewa kipaombele.
Kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2012, Tanzania ina vijiji 19,200 Ambavyo vinahudumiwa na zahanati 6,658 na hivyo basi kuna upungufu wa zaidi ya zahanati 12,000 ili kukidhi mahitaji ya wakazi wa vijiji vyote.
Kumekuwa na mabadiliko ya kuongezeka na kupungua kwa zahanati nchini. Mathalani mwaka 2013 kulikuwa zahanati 5,680 na mwaka uliofuata wa 2014 zilipungua hadi kufikia 6,002 na sababu kubwa ni baadhi ya zahanati ni kutotimiza masharti na matakwa ya mwongozo wa matibabu nchini na hivyo kulazimika kufungwa. Juhudi zilifanyika na idadi ya zahanati ziliongezeka hadi kufikia 6,549 mwaka 2015 na mwaka uliofuta wa 2016 zilifikia 6,658.
Kinachotokea ni kwamba wingi wa vituo vya kutolea huduma za afya unapungua kutoka ngazi ya kijiji, tarafa, wilaya hadi kitaifa. Hali hii inaweza kusababishwa na uhaba wa rasilimali fedha na watu, ubora wa huduma kwenye hospitali husika.
Mwaka 2016, kulikuwa na vituo vya afya 759 nchini kote ambapo ni sawa na kusema kuwa kila mkoa ulikuwa na vituo takribani 29. Kimsingi huduma zinazotolewa kwenye vituo vya afya zina hadhi ya juu ukilinganisha na zahanati kwasababu vinahudumia watu wengi zaidi na vinatakiwa kuwa na vifaa vya kisasa na huduma kama vile upasuaji na kliniki za mama na mtoto.
Idadi ya zahanati zilizoko nchini ni mara 9 ya vituo vya afya ambavyo vinategemewa kuwasaidia wagonjwa ambao hawajapata matibabu ya uhakika kwenye zahanati. Changamoto inayojitokeza ni kuwa vituo hivyo vinaelemewa na idadi kubwa ya wagonjwa wanaotoka ngazi ya chini na kwa vyovyote vile baadhi yake vitakuwa havina huduma bora za matibabu.
Pia vituo vya kutolea huduma za afya hupungua zaidi katika ngazi ya mkoa hadi kitaifa. Mwaka 2016 kulikuwa na hospitali 263 za wilaya, mkoa na rufani. Hizi ndio hospitali pekee zinazotegemewa na watanzania zaidi ya milioni 50 nchi nzima kupata matibabu.
Pengo kati ya vituo vya afya na hospitali sio kubwa sana ukilinganisha na zahanati ambazo ni nyingi lakini huduma zake hazilingani na hospitali nyingine za ngazi ya wilaya na mkoa.
Na utaratibu uliopo ni kwamba mgonjwa anatakiwa kutibiwa ngazi ya juu ikiwa tu zahanati na vituo vya fya vimeshindwa kumpatia matibabu yanayotakiwa. Kwa utaratibu huo vituo vya afya na hospitali nyingi huelemewa na wagonjwa kutokana na uwekezaji mdogo na huduma zisizoridhisha kwenye zahanati.
Kutokana na hali halisi ya upatikanaji wa huduma za afya nchini, serikali na wadau wanapaswa kuongeza juhudi za kuboresha na kujenga vituo na hospitali ili kukidhi ongezeko la watanzania ambao wanatakiwa kuwa na afya bora zitakazosaidia katika ujenzi wa taifa.
Ujenzi na maboresho hayo ni muhimu yakaenda sambamba na tathmini ya huduma zinazotolewa, idadi ya vituo ili kuyasaidia maeneo yenye uhitaji mkubwa wa huduma za afya.