Katika mfumo wa vyama vingi hasa vyama vikubwa vyenye ushawishi katika jamii, migongano na malumbano ya ndani kwa ndani ni jambo la kawaida. Na hii hujidhihirisha kwa kuibuka vikundi vya wanachama wachache wenye mawazo mbadala kupaza sauti zao pale wanapoona baadhi ya mambo hayaendi sawa au wakiwa na nia ya kupigania maslahi ya uongozi ndani ya chama.
Hili limetokea na linatokea katika nchi za Afrika ikiwemo Tanzania ambayo ni mdau mkubwa wa siasa za vyama vingi. Hali hii imekuwa ikitafsiriwa kuwa ni mapinduzi dhidi ya mwenyekiti na uongozi wake. Na kwasababu kila mtu anapenda kuendelea kuongoza na kuwa na ushawishi katika chama, kila jitihada hufanyika kuwasulubisha wale wote wenye mawazo mbadala pasipo kuangalia madhara kwa chama husika.
Migogoro ya namna hii imeviathiri vyama vingi na kuvifanya vipoteze ushawishi mbele ya jamii, lakini kwa upande mwingine migogoro hiyo imekuwa ni faida kwa wale wanaofukuzwa na hata kwa wananchi wasio na vyama ambao viongozi wanaowaongoza katika jamii, wengi wao wanatokea kwenye vyama vya siasa.
Mfano mzuri ni migongano ya kiungozi katika Chama cha African National Congress (ANC) cha Afrika Kusini ambacho kwa sasa kinaongozwa na Rais Jacob Zuma. Mwaka 2012 Rais Zuma ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho aliingia katika mgogoro wa kisiasa na Julius Malema, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Tawi la Vijana katika chama cha hicho.
Kwa mujibu wa duru za kisiasa, Malema alionekana kutishia uenyekiti wa Rais Zuma, kwa kuleta mawazo mbadala katika chama na kukitaka chama kirejee katika misingi yake ya kuwatumikia watu wa hali ya chini kama sera yake inavyokitaka.
Baadhi ya viongozi wa chama hicho wanatajwa kuhusika katika ufisadi, kuwakumbatia mabwenyenye na wafanyabiashara wakubwa, jambo ambalo lilizua minong’ono na hisia tofauti miongoni mwa wanachama hicho na wananchi wa Afrika Kusini.
Kwa kutambua hilo Malema na baadhi ya wenzake katika chama walitumia fursa hiyo kukemea mambo hayo ya kifisadi yaliyokuwa yakiendelea katika chama hicho. Kutokana na ushawishi wa hoja zake, Malema alipata umaarufu ndani na nje ya chama na kutishia kukigawa chama, ndipo Rais Zuma akiwa Mwenyekiti aliitumia Kamati Kuu (Central Committee) ya chama kumuundia zengwe Malema na kufikia hatua ya kumuondoa katika chama ili kurejesha utulivu miongoni mwa wanachama.
Kiongozi wa Chama Cha Economic Freedom Fighters (EFF), Julius Malema akiwa katika moja ya mikutano ya chama chake
Kwa kutokujua madhara yatakayotokea baada ya kuondoka Malema na kundi lake, chama cha ANC kilipoteza baadhi ya viti vya uwakilishi katika bunge. Kutokana na tuhuma alizozitoa Malema, wabunge na wananchi wameendelea na jitihada za kumshinikiza Zuma kuondoka katika nafasi ya urais, baada ya kuhusishwa na ufisadi ikiwemo kujenga makazi yake binafsi kwa kwa fedha za umma.
Malema alipoondoka ANC aliunda chama chake kinachoitwa Economic Freedom Fighters (EFF) ambacho katika uchaguzi uliopita wa 2014 kilijipatia viti 25 vya Uwakilishi Bungeni na bado kinazidi kupata umaarufu mkubwa miongozi mwa jamii kutokana na sera yake ya kuwatetea wanyonge dhidi ya sera za unyonyaji na ubaguzi, ambazo baadhi ya viongozi wa ANC wanatajwa kuzikumbatia.
Matukio kama haya yameendelea kutokea katika nchi yetu, hasa kwa vyama vikubwa vya CCM, CUF na CHADEMA. Migogoro hiyo ya ndani ya vyama imekuwa na faida katika ustawi wa demokrasia hasa pale kundi la wanachama linapoondoka katika chama, huunda vyama vingine ambavyo hutoa ushindani wa kisiasa vikiwa na mawazo mbadala katika maendeleo ya taifa. Ili mfumo wa vyama vingi uendelee kuwa na maana ni lazima vyama vikongwe vikumbwe na migogoro kama hii ili kuzalisha vyama vingine.
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho ndio chama kikuu cha upinzani kwa sasa nchini, ni matokeo ya migongano ya kimaslahi iliyotokea katika chama cha CCM miaka ya nyuma.
Baadhi ya wanachama wakiongozwa na Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Edwin Mtei walitoka CCM na kuunda chama cha demokrasi na maendeleo ambacho tangu uanze mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 kimekuwa kikitoa ushindani mkubwa kwa chama tawala CCM.
Hata baadhi ya wanachama wake mara kadhaa wameingia katika migongano na serikali kutokana na kugusa maslai ya watawala ambayo yanatajwa kukiuka misingi ya utawala bora na haki za raia.
Kwa sasa CHADEMA kimejiimarisha katika maeneo mengi kutokana na ushirikiano uliopo kati yake na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), ambapo kimefanikiwa kupata Viti vya Ubunge na kuongoza baadhi ya Halmashauri za Wilaya nchini.
Kuondoka kwa Mtei na kundi lake kutoka CCM kuliteta maana katika siasa za vyama vingi. Huenda CHADEMA tunayoiona leo isingekuwepo, ikiwa watu wachache wenye mawazo mbadala ambao walikuwa wanatafuta sehemu sahihi ya kuyasemea wasingeondoka CCM.
Ni faida kuwa na chama kinachotoa ushindani kwa chama tawala kwa sababu kinaongeza uwajibikaji na uwazi miongoni mwa viongozi wa serikali na kuifanya itimize majukumu yake ipasavyo kuwatumikia wananchi.
CHADEMA kama CCM, kinakumbana na mikinzano na mitafaruku ya ndani kwa ndani ambayo ni kundi la watu wachache kuleta mawazo mbadala. Mfano mzuri ni mgogoro wa kiungozi uliojitokeza baina ya Mwenyekiti wa Chama hicho Freeman Mbowe na Naibu Katibu Mkuu wa wakati huo Zitto Kabwe uliotokea mwaka 2014 wakati chama kikijiandaa kufanya uchaguzi wa ndani kuwapata viongozi wapya.
Wakati harakati za maandalizi ya uchaguzi zikiendelea zilizuka tuhuma kuwa Zitto na baadhi ya wanachama akiwemo Profesa Kitila Mkumbo waliandaa waraka unaodhaniwa ni mapinduzi ya uongozi ndani ya chama. Zitto na wenzake walihojiwa na Kamati Kuu (CC) juu ya waraka huo na walikiri kuuandaa lakini walidai haukulenga kuupindua uongozi uliokuwepo, na ilikuwa ni mbinu za kupata ridhaa ya kuongoza chama.
Kutokana na umaarufu aliokuwa nao Zitto Kabwe ndani na nje ya chama ilionekana dhahiri akiachiwa aendelee na mpango wake wa kugombea nafasi ya Uenyekiti atakigawa chama na baadhi ya viongozi watapoteza nyadhifa zao.
Mwenyekiti Freeman Mbowe kama alivyofanya Zuma dhidi ya Malema, aliamua kuitumia Kamati Kuu kumsulubu Zitto kwa nia ya kukinusuru chama. Zitto akavuliwa nyadhifa zake zote ndani ya chama na kilichofuata ni kusimamishwa uanachama, na hivyo kutishia kutenguliwa ubunge wake.
Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe akiwa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, bungeni hivi karibuni.
Ilimlazimu akimbilie mahakamani kutafuta haki baada ya jitihada za ndani ya chama kushindikana na wanachama wengi kukosa imani naye. Wakati kesi ikiendelea mahakamani, chama kupitia Mwanasheria wake, Tundu Lissu kilitangaza kumvua uanachama Zitto na wenzake akina Profesa Kitila Mkumbo na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Arusha Samson Mwigamba.
Mwaka 2015 Zitto akaunda chama chake cha Accountability and Transparency (ACT) na baadaye kubadilisha jina na kuwa ACT Wazalendo kikisimamia falsafa ya ujamaa na kujitegemea. Zitto mwenyewe aliteuliwa kuwa Kiongozi Mkuu wa chama na Mwenyekiti wa sasa ni Jeremiah Maganja. Kwa muda mfupi chama hicho kilifanikiwa kupata wanachama na kushiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015 huku kikiwa ni chama pekee kilichomsimamisha mwanamke kugombea nafasi ya urais.
Hata hivyo akikupata mafanikio makubwa katika uchaguzi wa mwaka 2015, lakini kilipata kiti kimoja cha uwakilishi bungeni na kufanikiwa kuongoza halmashauri ya mji wa Kigoma Ujiji.
Baadhi ya wachambuzi wa siasa wanaitaja ACT Wazalendo kama chama mbadala cha upinzani baada ya CHADEMA kwa miaka ijayo kutokana na falsafa yake ya ujamaa na kujitegemea ambayo inatetea zaidi maslahi ya wanyonge na kupingana na sera za kibebari ambazo sio rafiki kwa mtu wa hali ya chini.
Migogoro ndani ya vyama vya siasa itaendelea kuwepo na kufukuzana pia kutaendelea kwasababu kila siku zinaibuka fikra mpya ambazo ndio zinatoa muelekeo mpya katika maendeleo ya nchi. Na hapo ndipo dhana ya mfumo wa vyama vingi hujidhihirisha kwa uwazi ili kuendeleza ushindani baina ya vyama, kutafuta ridhaa ya kushika dola na kuwatumikia wananchi.