UKOSEFU wa zahanati na vituo vya afya katika maeneo ya pembezoni nchini Tanzania unachangia wananchi wengi kukosa huduma za afya kwa wakati.
Uchunguzi ulifanywa na FikraPevu umebaini kuwa hata pale penye miundombinu, huduma za afya zimekuwa hazipatikani katika maeneo salama kwa mujibu wa taratibu.
Kadhia hiyo ya ukosefu wa vituo vya huduma za afya haijawaacha nyuma wakazi zaidi ya 8,000 katika Kata ya Mindu iliyopo Manispaa ya Morogoro.
Uchunguzi wa FikraPevu umeonyesha kuwa, wakazi hao wamekuwa wakipata huduma ya kliniki kwa mama na watoto chini ya mti, kutokana na kukosa jengo la zahanati.
Wasemavyo wananchi
Mkazi wa Kata ya Mindu, Maliki Malupu, ameiambia FikraPevu kwamba, ukosefu wa huduma bora za afya katika vituo vya afya wakati wote, ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili Manispaa hiyo.
Anasema kukosekana kwa huduma ya vipimo na utoaji wa huduma katika vituo hivyo hasa siku za Jumamosi na Jumapili pamoja na sikukuu, kunachangia kuwepo kwa msongamano wa wagonjwa siku za kazi.
Ameiambia FikraPevu kwamba, uhaba wa vituo vya afya vya kukidhi mahitaji ya wananchi unasababisha watu wengi kukosa huduma kwa wakati, hivyo kulazimika kutafuta huduma hizo katika hospitali binafsi ambako hutumia gharama kubwa.
“Nikitibiwa katika hospitali binafsi natumia kiasi cha Shs. 25,000 hadi 40,000, inategemea naumwa ugonjwa gani, lakini ikiwa kwenye zahanati ya umma, gharama inakuwa chini na ni nafuu kwa wananchi wengi,” anasema.
Bwende Waziri, mkazi wa Kata hiyo ya Mindu, anasema ahadi zinatolewa wakati wa kampeni za uchaguzi zingekuwa zinatekelezwa, huduma za kijamii nchini zingekuwa kuboreshwa.
Kinyume cha matarajio ya wananchi wengi, Waziri anasema uchaguzi ukishapita tu, kila kitu husaulika.
“Ufike wakati sasa wote wanaotoa ahadi hewa wawe wanachukuliwa hatua kwa ulaghai,” Waziri ameiambia FikraPevu.
Akitoa mfano, anasema maboresho katika huduma za afya yamekuwa yakizungumzwa na viongozi mbalimbali wa serikali, lakini utekelezaji wake unafanywa taratibu, na wakati mwingine kutotekelezwa kabisa.
Kauli ya Mganga Mkuu wa Manispaa
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Morogoro, Dkt. Baraka Jonas, anakiri kubwa changamoto za upatikanaji wa huduma bora za afya ni kubwa, lakini akasema katika maeneo ambayo hakuna vituo vya afya karibu na makazi ya watu wanatumia huduma ya mkoba ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma.
Huduma ya mkoba ilipitishwa na Wizara ya Afya kwa lengo la kutoa huduma karibu na wananchi na kuepusha kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za afya.
Dkt. Jonas ameiambia FikraPevu kuwa, huduma zinazotolewa kupitia “mkoba” ni pamoja na kupima wajawazito, afya za watoto pamoja na kupima uzito watoto ambao bado wanahudhuria kliniki.
Kupitia utaratibu huo, wahudumu wa afya hufika katika eneo husika wakiwa na vitendea kazi, dawa pamoja na vipimo, lakini kutokana na mazingira kutokuwa rafiki huwalazimu kutoa huduma sehemu yoyote.
Anasema kwa vile baadhi ya maeneo yanayochaguliwa kutolea huduma huwa hakuna majengo, watoa huduma hulazimika kutoa huduma hizo chini ya miti, jambo ambalo amekiri kwamba ni la hatari lakini inalazimu.
“Huduma ya mkoba ipo sehemu zote ambazo hakuna vituo vya afya na zanahati, inafanyika kuwapunguzia wananchi adha ya kutumia gharama, muda mwingi wa kutafuta huduma ya afya,” anasema.
Ameiambia FikraPevu kwamba, katika kupambana na changamoto ya huduma ya mkoba, halmashauri inajitahidi kuhimiza viongozi wa Kata na Mitaa kuweka vipaumbele vya kujenga Vituo vya Afya na Zahanati katika maeneo yao kwa njia ya kujitolea.
FikraPevu imebaini kwamba, Kata ambazo hazina Vituo vya Afya hadi sasa katika Manispaa ya Morogoro ni Kauzeni, Lukobe, Tungi, na Mindu ambako wanapata huduma katika Zahanati ya Madanganya inayodaiwa kutokukidhi mahitaji.
Dkt. Jonas ameeleza changamoto kubwa katika Sekta ya Afya kuwa ni ukosefu wa dawa katika zanahati na vituo vya afya, hali inayochangiwa na wingi wa watu wanaohitaji huduma katika vituo vya serikali.
“Tunapokea dawa kutoka Bohari ya Dawa (MSD) kila baada ya miezi mitatu, zikiisha tunaomba tena, hivyo vituo vingi vinakuwa na upungufu wa dawa kutokana na kwisha kabla ya miezi mitatu,” anasema.
Mhudumu wa Afya, Joyce Aaron, anasema changamoto wanazokabiliana nazo wakati wa kutoa huduma za afya ni kutokuwa na jengo maalumu lililopangwa kwa kazi hiyo.
Joyce ameiambia FikraPevu kuwa, kipindi cha mvua huwapasa kutafuta jengo lililo karibu kwa ajili ya kutolea huduma ya kliniki kwa watoto, lakini kipindi cha jua hukaa chini ya miti.
Anasema kutokana na mitaa ya Kata ya Mindu kuwa mbali mbali, hushindwa kufika kwenye kituo kilichopangwa kwa wakati muafaka kutokana na miundombinu ya barabara kuwa mibovu.
Mkurugenzi anasemaje
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, John Mgalula, anasema halmashauri hiyo yenye wakazi 315,248, Kata 29 na Mitaa 295 inazo zahanati 46, Vituo vya Afya 13, hospitali 4 za umma, hospitali 6 zizonamilikiwa na taasisi za dini, na 3 zinamilikiwa na watu binafsi.
Ameiambia FikraPevu kwamba, katika Bajeti ya 2017/2018 halmashauri imekusudia kutekeleza miradi minne ya Sekta ya Afya, ambayo ni pamoja na kujenga chumba cha upasuaji katika Zahanati ya Mafiga na kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya Sinai.
Mradi mwingine ni kuweka umeme na maji safi katika Hospitali ya Wilaya iliyopo Kata ya Kihonda na ukarabati wa Zahanati ya Madanganya iliyopata ufa na kuhamishia huduma katika nyumba ya watumishi.
“Katika kipindi cha mwaka 2017/2018, halmashauri inatarajia kutumia Shs. 7 bilioni kulipa mishahara ya watumishi wa afya, kupokea kiasi cha Shs. 598.3 milioni kutoka kwenye Mfuko wa Afya,” anasema.
Nini kifanyike
Wananchi wengi wameshauri Serikali kuweka mfumo mzuri wa utoaji wa huduma za afya katika maeneo ya vijijini na pembezoni, kuweka mazingira mazuri ya utendaji, vitendea kazi, miundo mbinu ya majengo na barabara.
Aidha, wameshauri kuwepo kwa ushirikishwaji wa wananchi katika uchangiaji wa huduma za afya, na kuwaelimisha umuhimu wa kujiunga katika Mifuko ya Afya Jamii (CHF) kwa lengo la kupata huduma kwa bei nafuu, na kuwaelimisha umuhimu wa kujitolea nguvu kazi katika kuchangia miradi ya afya inayoibuliwa ndani ya mitaa na vijiji.