Mradi wa Maji Ziwa Victoria washindwa kutatua kero wilayani Misungwi

Jamii Africa

UKAME wa kutisha uliotokea mwaka 2015 katika maeneo kadhaa nchini ulisababisha wananchi wengi kupata taabu ya maji safi na salama na kulazimika kunywa maji ya madimbwi, baadhi wakichangia na wanyama.

Miongoni mwa maeneo yaliyokumbwa na kadhia hiyo ni Kijiji cha Usagara kilichoko wilayani Misungwi katika Mkoa wa Mwanza ambacho kilishuhudia kisima pekee kilichokuwa tegemeo kukauka kutokana na ukame huo, FikraPevu inaripoti.

Kwa miaka 65 kisima hicho, ambacho kilichimbwa tangu mwaka 1950, kilikuwa mkombozi mkubwa kwa wakazi wa kijiji hicho, lakini ukame, ambao kwa kiasi kikubwa umesababishwa na mabadiliko ya tabianchi yanayochangiwa na uharibifu wa mazingira, haukuwa na msalie baada ya kukausha kisima hicho.

Lakini Kijiji cha Usagara ni miongoni mwa vijiji vingi vya Wilaya ya Misungwi vinavyokabiliwa na kero kubwa ya maji ya muda mrefu licha ya ukweli kwamba wilaya hiyo iko kilometa chache tu kutoka Ziwa Victoria.

Maeneo mengi ya vijiji vya wilaya hiyo yamekuwa yakitegemea maji ya visima ambavyo kipindi cha kiangazi hukauka na kusababisha watu kutumia maji yaliyotuwama kwenye madimbwi, jambo ambalo ni hatari kwa afya za wananchi.

Licha ya wilaya hiyo kuwa jirani na Ziwa Victoria, lakini Mradi Mkubwa wa Maji wa Ziwa Victoria ambayo uligharimu mabilioni ya fedha kutoka Shirika la WaterAid umepita katika baadhi ya vijiji vya wilaya hiyo ingawa hakuna utaratibu wowote wa kuviwekea miundombinu ili kusambaza maji hayo.

FikraPevu inafahamu kwamba, Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria unalenga kusambaza maji katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Tabora, hivyo Misungwi ilipaswa kuwa miongoni mwa maeneo ya wanufaika, lakini badala yake bomba hilo kuu limekuwa kama pambo kwa wakazi wa vijiji vya wilaya hiyo linakopitia.

Ingawa vipo vijiji katika Wilaya ya Misungwi ambavyo viko pembezoni mwa Ziwa Victoria, lakini ni vigumu kutumia maji hayo moja kwa moja kwani si salama kutokana na uchafu unaomwagwa kuelekea ziwani, ambao umeyafanya maji hayo kuwa na kemikali hatari.

Katika Hotuba yake kwa Bunge la Bajeti 2016/2017, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Injinia Gerson Lwenge, alisema serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya maji katika vijiji 100 vilivyopitiwa na bomba kuu linalotoa maji Ziwa Victoria, na huu ulikuwa ni uboreshaji wa vijiji vya awali 40 vilivyotambuliwa na halmashauri mbalimbali ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi.

Mpaka kufikia mwaka 2017 hali ya upatikanaji wa maji wilayani misungwi imeendelea kuwa si ya kuridhisha kwa vijiji vingi vilivyopitiwa na bomba hilo, hili linathibitishwa na taarifa za hivi karibuni za baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo kutaka kuvamia miundombinu ya bomba hilo kwa kile kinachoonekana kutokuwa na faida nalo.

Hatu hiyo ilifanya waziri wa maji kuutaka uongozi wa Wilaya ya Misungwi kuacha kuhamasisha wananchi kuvamia miundombinu ya bomba hilo.

Waziri Lwenge aliyasema wakati wa hafla kusaini makubaliano ya utekelezaji wa miradi ya maji na wahisani mbalimbali.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Misungwi, Anthony Masele, alithibitisha kuwa bomba la maji linalopita wilayani humo halina faida kwao jambo linaloamsha wananchi kufanya maandamano kuvamia miundombinu ya bomba hilo.

Taarifa ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji inasema kufikia mwaka 2025 bomba hilo linatarajiwa kuhudumia watu milioni 1.

Lakini miaka 8 kabla ya kufikia mwaka huo bomba hilo limeshindwa kuwa msaada kwa watu 351,607 wa Misungwi huku wilaya hiyo ikiwa na ongezeko dogo la watu la 2.8%.

Kwa kadiri hali ilivyo, idadi ya watu watakaohudumiwa na bomba hilo inaweza isifikiwe katika kipindi hicho katika mikoa hiyo mitatu kutokana na kutokuwepo kwa jitihada za makusudi na usambazaji wa maji hata katika maeneo ambayo tayari bomba hilo linapita, achilia mbali yaliyo mbali.

Katika Mkoa wa Mwanza, FikraPevu inatambua kuwa, ni 53% tu ya wakazi wake ndio wanaopata maji safi, huku idadi kubwa ya wapatao maji safi ni wale wanaoishi mijini hasa wilaya za Nyamagana na Ilemela.

Walio wengi, hasa wanao kwenye mwambao wa ziwa, wanakunywa moja kwa moja maji ya ziwa hilo, ambayo hivi karibuni FikraPevu kupitia tafiti mbalimbali ilionyesha kuwa maji hayo yana kemikali hivyo si salama.

Hatua hiyo ndiyo iliwafanya wakazi wa Wilaya ya Misungwi kuhamaki na kutaka kuvamia miundombinu ya maji ya bomba linalosambaza maji kutoka Ziwa Victoria, kwani hawapo tayari kuona maji safi yakiwa yanapita kwao huku wenyewe wakihangaika na maji yasiyo salama ambayo yanahatarisha afya zao.

Kumekuwa na kauli zenye mikamganyiko juu ya utekelezaji wa miradi ya maji wilayani humo, kwani katika hafla ya kusaini mikataba ya usambazaji maji, Waziri Lwenge aliwaambia wananchi wa wilaya hiyo kuwa serikali imetenga kiasi cha Shs. 30 bilioni kwa ajili ya wilaya hiyo.

Lakini kabla ya hapo kuilikuwa na nukuu kutoka kwa Mhandisi wa Maji wa Mkoa wa Mwanza akitaja kiwango cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji Misungwi ambacho ni Shs. 5.6 bilioni.

Hali hiyo inatia mashaka iwapo utekelezaji huo wa miradi ya maji kama unaweza kutatua kero ya maji mkoani Mwanza, hususan wilayani Misungwi.

Ushauri kwa serikali ni kwamba, pindi miradi mbalimbali inayotekelezwa inapofanyika basi hakuna budi kufanya makadirio ni kwa kiwango gani wananchi wanaozungukwa na huo miradi husika wanaweza kufaidika, vinginevyo matatizo mengi yanaweza kutokea kutokana na uzembe ambao unasababishwa na serikali juu ya utatuzi wa matatizo mbalimbali kwa wananchi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *