Mtoto Kudra mfano wa watumia gundi kama kilevi mtaani

Sifa Lubasi

MAISHA ni mtihani ambao unatakiwa kufaulu ndipo usonge mbele.

Unapokutana na Kudra Majuto(20), katika mitaa mbalimbali ya Mji wa Dodoma kama mzazi lazima utakuwa na kuhoji kama si kwa sauti basi ni kimyakimya ndani ya nafsi yako.

Akiwa ni mama wa mtoto wa kiume mwenye umri wa mwaka moja na miezi minne sasa bado hana matumaini na maisha yake.

Kudra ni mtoto maarufu wa mitaani ambapo wanaomfahamu wanasema ameishi mitaani tangu akiwa na miaka sita au saba.

Licha ya sasa kuishi na mama yake lakini maisha yake mengi amekuwa akitumia kushinda mtaani huku akizunguka huku na kule kuomba chochote kwa ajili ya kuendesha maisha yake na mtoto wake.

Kuna wakati mwingine hutembea kwenye mvua akiwa na mtoto huyo na mara kadhaa baadhi ya watu wamemshuhudia akimning’iniza mtoto wake kichwa chini miguu juu  au kukimbia akiwa na mtoto hali inayopelekea mtoto kurukaruka mgongoni huku akilia.

“Nina akili timamu ila maisha ndiyo magumu kwangu nampenda mtoto wangu hata kama watu wakiona namning’iniza si kama simtaki bali namfanyisha mazoezi” anasema

Anasema alijifungua Mtoto huyo Aprili, 20, mwaka jana katika hospitali ya Mkoa wa Dodoma na sasa anatumia njia ya uzazi wa mpango.

Hata hivyo anasema tangu amekuwa na mtoto maisha yanazidi kuwa magumu kwake kwani anapofika mtaani kwa ajili ya kuomba chochote baadhi ya watu wamekuwa wakimtolea kauli za kuudhi na kukera sana.

“Mwingine unamuomba akusaidie  anakutukana huku wengine wakisema twende tukalale kwanza ndipo wanipe hela” anasema

Bado hakumbuki lini alianza kuishi mtaani lakini kitu anachojua alinza kuishi mtaani akiwa  na umri mdogo.

Kudra anasema  mtoto wake aliyempa jina la Juma ni wa pili kwani mimba yake ya kwanza alipata mwaka 2010 hata hivyo alizaa mtoto mfu  huku sababu kubwa ikielezwa ni matumizi ya madawa ya kulevya aina ya gundi.

Madawa hayo ni mchanganyiko wa gundi ya viatu na petroli na mtu anapovuta huonekana kama amevuta madawa ya kulevya.

Binti huyo anasema maisha ya mtaani yamekuwa na changamoto nyingi hasa kwa wasichana kwani kuna watu wengi ambao hupenda kufanya mapenzi nao kwa ahadi au ujira mdogo.

“Mimba yangu ya kwanza nilipata tayari nikiwa nimeshaondoka mtaani na kurudi kukaa kwa mama, nilibakwa na mwanaume ambaye nilimfahamu kwa sura”

Licha ya kumfuatilia mwanaume huyo akajua ofisi yake mpaka nyumbani kwao kazi yake ilikuwa mbeba mbao aliyekuwa akiishi eneo la Majengo Mjini Dodoma na kabila lake ni Mbena.

Hata hivyo mwanaume huyo baada ya kufuatwa alikana mimba hiyo kuwa si yake .

kudra

Kudra Majuto akiwa na mtoto wake muda mfupi baada ya kumaliza kufanya naye mahojiano

Kudra anasema aliendelea kukaa nyumbani mpaka aliposhikwa na uchungu, alijifungua mtoto wa kike, lakini kwa bahati mbaya alifariki kwa vile alikuwa akivuta gundi.

Anasema alikuwa akiambiwa kuvuta gundi ni tatizo kwani ataua mtoto lakini hata hivyo alikuwa akishindwa kuacha.

Anasema  unapoanza kuvuta gundi kuachana na jambo hilo huwa ni kazi kubwa sana  na unatakiwa kuvuta kila siku na usipovuta kichwa kinauma.

Bado analia ugumu wa maisha kwani mtoto aliyenae sasa mwanaume aliyempa ujauzito huo alikuwa ni msukuma mkokoteni  naye aliruka kimanga juu ya ujauzito huo na mwanaume kuamua kuhama kabisa Dodoma na hajulikani mahali alipohamia.

Mratibu wa Kituo cha Watoto wa Mitaani cha Safina Street Network (SSN)  Mchungaji Patrick Kakwaya wa Kanisa la Pentekoste anasema Kudra aliwahi kuhudumiwa kituoni hapo hata hivyo baadaye waligundua  msichana huyo hana nia ya kusaidiwa.

Anasema Kudra alianza kuwa mitaani akiwa na miaka sita au saba na kulikuwa na juhudi za kumsaidia atoke mitaani lakini juhudi zote hazikufanikiwa.

Anasema binti huyo aliwahi kupata nafasi katika Chuo cha masista  Wakatoliki Arusha lakini akawa akikwepa nafasi hiyo mpaka ikapotea.

Pia mama mmoja wa Kiitaliano, ajulikanaye kama Mama Alice wa kituo cha watoto wa mitaani cha Shukrani, alitaka kumsaidia kwa kumsomesha lakini amekuwa akipiga chenga.

Mchungaji huyo anasema sababu kubwa ya watoto kuwa mitaani ni kutokana na familia kushindwa kutumiza wajibu wao kwa watoto.

“Wazazi wengi wanaishi maisha ya kimaskini, hakuna mhimili mzuri wa ndoa, mama anaachika anaolewa na mwanaume mwingine na baba anaona mwanamke mwingine na kuacha watoto wakining’inia” anasema.

Anasema walichogundua ni kuwa  baba akikuta mwanamke ana watoto wa kiume hapendi hata akikubali kukaa nao atawatesa.

Pia  mazingira ya manyanyaso katika familia nayo yamekuwa yana mchango wake katika suala hilo kwani wakati mwingine mtoto wa kiume anataka kukaa na mama baada ya baba kuondoka.

“Watoto wengine huwa wanataka ulinzi wa mama yake mama anapopata mwanaume mwingine kunakuwa na mgogoro mkubwa kati ya mtoto wa kiume na baba wa kambo”

Mchungaji Kakwaya anasema  hali hiyo inaleta watoto wengi mtaani hilo ni tatizo kubwa kwani wanaume wengi ni walevi hawajali familia watoto wengi wanaokuja mtaani wanatumwa kurudi na fedha na wakipata wazazi wao wanachukua na kwenda kunywa pombe.

Anasema ukiangalia Dodoma Mjini utagundua kuna kundi kubwa la watoto wa mtaani  wanaofikia 25 ambao huvuta gundi.

Pia watoto hao wamekuwa wakitumia silaha kama wa njia ya kujihami na  kujitetea awe kama mwehu au wazimu ili aweze kuishi.

Hata unapokutana na watoto wanaotumia gundi katika Manispaa ya Dodoma hutaweza kumuangalia mara mbili kutokana na muonekano wake kwani anakuwa kama mtu aliyechanganyikiwa hata unapomuta hatakujibu kitu huku mwingine anaweza kukuangalia kwa dharau na kuondoka.

Mara kadhaa nimewahi kukutana na watoto wanaotumia gundi lakini unapomuita anakuambia hata shida ya hela kwani ameshiba.

Ni vigumu kumpata mtoto anayetumia gundi kukaa naye na kumuhoji labda awe hajavuta hiyo gundi.

Lakini ukibahatika kuonana na mtoto anayetumia gundi na kubahatika kuongea naye anachoamini ni kuwa gundi humfanya ajisikie huru zaidi kufanya chochote.

“Nisipopata gundi hata kichwa kinaniuma bora nivute nilale siku nzima” anasema mtoto moja wa mtaani ambaye hataki kutaja jina lake.

Kuna wakati mtoto moja wa mtaani alilala siku nzima katika mtaa wa Uhindini akiwa hajitambui kutokana na kuvuta kiasi kikubwa cha gundi ambacho kilimzidi nguvu hali ambayo ilileta hofu kwa wapiti njia huenda alikuwa amefariki.

Lakini hakuna hata moja aliyethubutu kusogelea mtoto huyo kutokana na wenzake wakiwa pembeni huku nao wakiwa wameshika chupa za gundi.

Kuna watoto walikuwa wakiogopa kulala hadi sasa kwa kuogopa kufanyiana vitendo vya ulawiti na pale wanapoamua kulala wenzao huwavua nguo na kuwakamata kwa nguvu na kuwafanyia vitendo hivyo.

Pamoja na hayo,Ofisa Ustawi wa Jamii  Manispaa ya Dodoma,  Eupherezia Antony,  anasema tatizo la watoto wa mitaani kutumia gundi lipo.

Anasema katika Mji wa Dodoma kuna makundi mawili ya watoto  wa mitaani ambapo kundi la kwanza ni lile la watoto wanaoishi mitaani na kundi lingine ni la watoto ambao wanaish kutumia itawadhibiti wazazi ambao hawatimizi wajibu wao kwa watoto hilo linaweza kupunguza ukubwa wa tatizo hili.

Anasema mkakati unaandaliwa wa namna ya kuziwezesha kaya duni kupata kipato kwani watoto wengi wa mtaani Dodoma wanatoka kwenye familia zao hufika mtaani kwa ajili ya kuomba na kisha jioni hurejea nyumbani.

Hata hivyo alisema kuwa, wamekuwa wakiwakamata watoto hao na kuwahoji na kuwaunganisha na familia zao, pia wanaandikishwa shule lakini baada ya muda wanarudi tena mtaani  huku wengi wao wakiacha shule kabisa.

“Watoto wengi wanaozurura wanatoka kwenye  familia zao na wamekuwa wakitumwa kuja kuomba fedha  mitaani hali ambayo inafanya watoto hao wakose fursa ya kwenda shuleni” anasema.

Afisa Ustawi huyo anasema watoto wengi wa mitaani wamekuwa wakitumia gundi hali inayofanya kuwa tishio la uhalifu kwa siku za usoni.

kamanda misime

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, David Misime

Pamoja na hayo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) David Misime anasema anafuatilia suala hilo kwa lengo la kubaini wauazaji, watumiaji wa gundi na baada ya kukamilisha uchunguzi wake atatoa taarifa kamili.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *