Muongozo wa matibabu kumaliza tatizo la upatikanaji wa dawa kwenye vituo vya afya?

Jamii Africa

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imezindua Muongozo wa matibabu na orodha ya dawa zote muhimu ili kupunguza tatizo la upatikanaji wa dawa katika vituo vya afya nchini.

Muongozo huo ni hatua ya utekelezaji wa Sera ya Afya (2007) ambayo katika kifungu cha 5.4.3 inatamka kuhakikisha kwamba dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi vinapatikana wakati wote, kwa kiasi cha kutosha na ubora unaotakiwa katika vituo vya afya.

Muongozo huo ulizinduliwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu siku chache zilizopita ikiwa ni mkakati wa serikali kuboresha huduma za afya ikiwemo upatikanaji wa dawa muhimu kwenye vituo vya afya ili kuwaondolea wananchi hadha ya kununua dawa hizo kwenye maduka ya watu binafsi.

"Ni muhimu kila kituo cha afya kuwa na dawa za kutosha, vifaa na vifaa tiba lakini ni lazima tuzingatie muongozo wa matibabu na orodha ya dawa kulingana na ugonjwa fulani ili kuepuka tatizo hili" amenukuliwa Waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema kuwa Muongozo huo umezingatia vigezo vyote vya kuweka dawa ambazo zilikuwa hazipo katika ngazi ya zahanati na vituo vya afya ambazo zimepata uthibitisho kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO).

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Mohammed Bakari Kambi amesema muongozo wa kutibu magonjwa mbambali umezingatia Orodha ya dawa ambazo zitakuwa zinatumika nchini kwetu kama dawa muhimu za kutibu magonjwa hayo.

Muongozo huo umekuja wakati ambao vituo vya afya hasa vinavyomilikiwa na serikali vikikabiliwa na uhaba wa dawa ambapo wananchi walioenda katika maduka ya vituo hivyo hawakukuta dawa na kulazimika kwenda kununua kwenye maduka ya watu binafsi kwa bei kubwa.

Ripoti ya taasisi ya Twaweza ya mwaka 2017 inayoangazia maoni ya wananchi kuhusu huduma za afya na ustawi wa jamii inathibitisha kuwa asilimia 70 ambayo ni sawa na wananchi 7 kati ya 10 waliokwenda kutibiwa katika robo ya pili ya mwaka 2017walikutana na upungufu mkubwa wa dawa.

Upungufu huo wa dawa umeongezeka kwa asilimia 11 ikilinganishwa na 2016 (59%). Pia kulikuwa na ongezeko la asilimia 6 mwaka 2016 ikilinganishwa na asilimia 53 mwaka 2015.

Hali ya upatikanaji wa dawa 2017 inalingana kwa karibu na ile ya 2014 (62%) ambapo ni tofauti ya asilimia 8. Hali hiyo ikashuka katika miaka miwili iliyofuata kabla ya kuongezeka kwa kasi na kufikia asilimia 70 mwaka huu.

Baadhi ya vituo vya afya havina dawa kabisa na wananchi huandikiwa wakanunue mahali pengine yakiwemo maduka binafsi. Na hata kama zipo hazitoshelezi mahitaji ya wagonjwa wote kutokana na mfumo usioridhisha wa usambazaji wa dawa hizo.

 

Ripoti ya Sauti za Wananchi ya Twaweza (2013) inaeleza kuwa “karibu wagonjwa wote (97%) wanaofika katika vituo vya afya huandikiwa dawa au maelezo ya dawa ama kupewa vyote kwa pamoja. Hata hivyo wagonjwa wawili kati ya watano (41%) wanaripoti kutokufanikiwa kupata dawa walizoandikiwa”.

Kwa mujibu wa Waziri Ummy amesema muongozo huo utasaidia wauguzi wa afya kufahamu ni dawa zipi zinatakiwa kwenye vituo vyao na hata zikiisha watatumia muongozo huo kuagiza kwa mamlaka husika ili kuondokana na tatizo la muda mrefu la ukosefu wa dawa katika vituo vya afya.

Inawezekana muongozo wa orodha ya dawa ukatatua kwa sehemu tatizo la dawa ikizingatiwa kuwa changamoto kubwa ya upatikanaji wa dawa katika vituo vya afya ni usambazaji usiorodhisha unaotumia mchakato mrefu kutoka Bohari Kuu ya Dawa ya Taifa (MSD) hadi kwenye vituo vya afya kupitia halmashauri ambao ndio wasimamizi wa vituo hivyo.

Kutatua changamoto hiyo ya usambazaji wa dawa, Waziri Ummy amewapiga marufuku Bohari Kuu ya dawa ya Taifa MSD na Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa (NHIF) kuagiza na kuandika dawa zilizo nje ya muongozo uliozinduliwa na serikali ili kuondoa matumizi ya dawa yasiyo sahihi.

Matumizi ya dawa yasiyo sahihi ni pamoja na kusambaza aina fulani ya dawa kwa wingi kuliko mahitaji ya wagonjwa waliopo katika eneo husika. Hii ni changamoto nyingine ambayo muongozo huo ungezingatia kwa kufanya utafiti wa magonjwa ambayo yanajitokeza sana katika eneo fulani ili kuwa na orodha iliyojitosheleza.

Akichangia kwenye mtandao wa Twitter juu ya uzinduzi wa muongozo wa orodha ya dawa, Mchangiaji mmoja, Enock Lwegalulila ameandika “Hongera. Ila upatikaji wa dawa hizo uzingatie sana aina ya magonjwa katika eneo husika. Hii habari ya kupeleka dawa za kichocho Northern zone (kanda ya kaskazini) na ukapeleka za ‘brucella’ Lake zone (kanda ya ziwa)” kunadumaza huduma. Waziri wewe dili na MSD supply chain (msambazaji mkuu) utasaidia sana kufanikisha program hii”.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *